Mbunge wa Nkasi anayemaliza muda wake kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Aida Kenani amewaaga wapiga kura wake leo Jumatano Julai 02, 2025 na kuwaambia sababu za kuwaaga.
Aida ametumia muda mwingi kuwafafanulia kwa nini hagombei tena mwaka huu na amisema: “Ndugu zangu, leo Julai 2, 2025 nimekuja hapa kuwashukuru lakini pia kuwaaga najua wengi mtajiuliza, wengine walinipigia simu, Aida tunasikia unahama, Aida tunasikia umeenda CCM, Aida tunasikia sijui unaenda wapi?
“ Leo Aida mwenyewe nipo hapa. Nataka niwaambie mpaka leo nazungumza na ninyi ni mashahidi, mtu wa kushindana na mimi na akanishinda kwenye jimbo hili la Nkasi hayupo! Uchaguzi huru na haki kwenye jimbo hili na akaja wa kunishinda hayupo!, Nazungumza kwa kujiamini CCM wanajua, labda waniibie.”
Akazidi kufafanua, “Sasa kwa nini nawaaga? Najua nikigombea mimi wapo ndugu zangu wataamini huyu ameibiwa na wapo ambao hawatakubali kwamba Aida ameibiwa kwa sababu wa kunishinda hayupo.
“Sasa hao watakaopigania haki na watakaong’ang’ania kuwa Aida ameibiwa wanaweza kupigwa risasi, wanaweza kupigwa panga, wanaweza kuuawa – sasa kwa nini niwe Mbunge wa kumwaga damu?
“ Kwa nini nikubali ndugu zangu wafe kwa sababu ya uchaguzi? Hali inayoendelea, kwa ajili ya heshima ya ndugu zangu, Mimi Aida nilizaliwa Nkasi, Kitovu changu kipo hapa na sina mahali pengine pa kwenda, sitaki ndugu zangu wafe ndio niwe mbunge, haiwezekani.
“Naamini inawezekana Mungu alinileta nioneshe nini maana ya uongozi kwa miaka mitano. Anayetoa uongozi ni Mungu, hatuwezi kulazimisha, mimi mtoto wenu nitapumzika niruhusu wakati wa Mungu ulio sahihi kuja kurudi kwenye mapambano.” Alisema Aida Kenani, Mbunge wa Nkasi anayemaliza muda huku akishangiliwa.