::::::
Katika hali isiyokuwa ya kawaida Watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na Uongozi wake wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Bw. Mussa Uledi na Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda wamesimama na kupiga Makofi kwa Dakika Moja mfululizo ili kuonyesha Shukrani kwa Walipakodi waliowawezesha kuandika historia ya kuvuka malengo ya makusanyo kwa miezi 12 mfululizo ya mwaka wa fedha 2024/2025.
Tukio hilo la aina yake limefanyika Julai 01.2025 kwa nchi nzima baada ya Kamishna Mkuu Mwenda kuwasilisha taarifa ya makusanyo iliyoonyesha kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025, TRA imekusanya jumla ya Sh. Trilioni 32.26, sawa na ufanisi wa asilimia 103 ya lengo la Sh. Trilioni 31.5, na ukuaji wa asilimia 16.7 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Kamishna Mkuu Mwenda, amesema TRA inawathamini na kuwajali Walipakodi wote nchini ndiyo maana wameamua kuwaonyesha heshima maalum ya kusimama na kuwapigia makofi kwa Dakika Moja mfululizo na kuahidi kuwa TRA itaendelea kuwahudumia na kutatua changamoto zinazowakabili.
“Nguzo yetu kubwa ni Wafanyabiashara, ndiyo maana tumekuwa tukiweka mazingira mazuri ya ulipaji Kodi kwa hiari kwa lengo la kuwezesha biashara nchini, na hii ni sehemu ya kutekeleza maagizo ya Rais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan aliyetuelekeza kuweka mazingira rafiki ya kukusanya Kodi ” amesema Bw. Mwenda.
Bw. Mwenda amesema kwa miezi yote 12 ya mwaka wa fedha 2024/2025, TRA ilivuka malengo ya makusanyo jambo ambalo halijawahi kutokea tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo na ni matunda ya mahusiano mazuri na Walipakodi.
Kwa mujibu wa Bw. Mwenda, wastani wa makusanyo ya kila mwezi umefikia Shilingi Trilioni 2.69 – kiwango cha juu zaidi kuwahi kufikiwa, kikiwa ni ongezeko kutoka Shilingi Trilioni 2.30 ya mwaka uliopita. Rekodi ya juu zaidi ya makusanyo kwa mwezi ni ya Desemba 2024 ambapo zilikusanywa Shilingi Trilioni 3.58, ikifuatiwa na Juni 2025 (Shilingi Trilioni 3.42) na Septemba 2024 (Shilingi Trilioni 3.02).
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRA Bw. Mussa Uledi ambaye pia alihudhuria hafla hiyo alisema kuwa kuongezeka kwa mapato ya ndani kupitia TRA kunatoa matumaini ya Tanzania kujitegemea kifedha, ikizingatiwa kwamba kuna mifano ya nchi kadhaa zilizokuwa tegemezi lakini baada ya kuimarisha makusanyo ya kodi kwa mapato ya ndani, zimepunguza utegemezi wa misaada kutoka nje.
“Kuvuka malengo haya ni matokeo ya utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais Samia kwa vitendo, yanayolenga kukuza biashara na kuimarisha uhusiano kati ya TRA na walipakodi. Tunawashukuru walipakodi wote kwa mchango wao mkubwa kwa taifa letu,” alisema Bw. Uledi..
Kwa upande wa Walipakodi akiwemo Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA), Bw. Edward Urio, Bi. Mariam Athuman kutoka Kariakoo iliyopelekea amani na utulivu katika soko la Kariakoo.
Mwenyekiti wa Jumuia ya Wamachinga Bw. Yusuph Mamoto wameahidi kuendelea kushirikiana na TRA.
Mwisho.