Dar es Salaam. Mfanyabiashara Saad Saad (56) na wenzake wawili wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka sita likiwemo la kujipatia lita 500 za mafuta ya petrolo na kutakatisha fedha kiasi cha Sh403 milioni.
Mashtaka mengine ni kuongoza genge la uhalifu, kughushi ripoti ya uthaminishaji viwanja, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha.
Mbali na Saada, ambaye ni mkazi wa Usagala mkoani Tanga, washtakiwa wengine ni Fabian Mazali(56) mkazi wa Goba na Rashida Mohamed(44) mkazi wa Usagala mkoani Tanga.
Washtakiwa hao ambao wote ni wafanyabiashara, wamefikishwa mahakamani hapo leo, Julai 3, 2025 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 16238 ya mwaka 2025.
Wakili wa Serikali, Titus Aron akishirikiana na Tumaini Mafuru waliwasomewa mashtaka hayo.
Hata hivyo, mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, Fabian Mazali hakuwepo mahakamani hapo kwa sababu yupo rumande anakabiliwa na kesi nyingine yenye mashtaka ya kutakatisha fedha ambayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

Mshtakiwa Rashida Mohamed(aliyevaa hijab) anayekabiliwa na mashtaka sita yakiwemo ya kughushi ripoti ya uthaminishaji wa viwanja, akiwa chini ya ulinzi wa askari kanzu. Picha na Hadija Jumanne
Katika shtaka la kwanza, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kuongoza genge la uhalifu, tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Mei 2022 na Septemba 2024 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Shtaka la pili, ni kughushi tukio wanalodaiwa kulitenda katika kipindi hicho ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa pamoja wanadaiwa kughushi ripoti ya uthaminishaji wa makazi katika kiwanja namba 112 kilichopo kitalu namba 6 kilichopo Tuangoma, manispaa ya Temeke kwa kuonyesha kuwa ripoti hiyo hilali wakati wakijua kuwa ni uongo.
Iliendelea kudaiwa kuwa katika shtaka la tatu, washtakiwa kwa nia ovu walighushi ripoti ya uthaminishaji wa kiwanja namba 501 kilichopo kitalu H eneo la Goba Manispaa ya Ubungo kwa kuonyesha kuwa imetolewa na kugongwa mhuri na Chisemeji Kome, wakati wakijua kuwa ni uongo.
Mahakama iliendelea kueleza kuwa katika shtaka la nne ni kughushi ambapo washtakiwa katika kipindi cha mwaka 2022 na mwaka 2024, kwa nia ovu walighushi ripoti ya uthaminishaji wa kiwanja namba 37, kitalu KBV kilichopo eneo la Viwandani barabara ya Korogwe mkoani Tanga kwa kuonyesha kuwa ripoti hiyo ni halali na imetolewa na Juma Said Jingu, wakati wakijua kuwa ni uongo.
Wakili Aron amedai katika shtaka la tano ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Mei 2, 2023 na Disemba 20, 2023 katika Jiji la Dar es Salaam.
Washtakiwa wanadaiwa kwa nia ovu, walijipatia lita 500 za mafuta ya Petrol zenye thamani ya Sh403milioni kwa kutoa nyaraka za kughushi wakionyesha kuwa zimelewa na kampuni ya Vivo Energy Tanzania Limited, wakati wakijua kuwa ni uongo.
Shtaka la sita ni kutakatisha fedha tukio wanalodaiwa kulitenda Mei 2, 2023 na Disemba 20, 2023 Jijini Dar es Salaam ambapo walijipatia lita 500 za mafuta zenye thamani ya Sh403milioni, wakati wakijua fedha hizo ni mazalia ya kujipatia bidhaa kwa njia ya udanganyifu.
Mafuru alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo wanaomba terehe nyingine ya kutajwa.
Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yao, hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama ya Kisutu haina Mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalumu kutoka kwa DPP.
Hakimu Nyaki alisema pia shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili washtakiwa hao halina dhamana kwa mujibu wa sheria, hivyo watarudishwa rumande hadi Julai 15, 2025 kwa ajili ya kutajwa.