BAADA ya kufanikiwa kubaki Ligi Kuu msimu ujao, benchi la ufundi la Tanzania Prisons limesema halitakurupuka kupangua kikosi, badala yake litachambua mchezaji mmoja mmoja kuhakikisha msimu ujao wanakuwa bora.
Hata hivyo, limesisitiza kuwa lazima mabadiliko yawepo kwa kwa kuingiza sura mpya kutegemea na mipango yake ya msimu ujao kuhakikisha wanaondokana na presha kama ilivyowakuta msimu uliomalizika hivi karibuni.
Prisons imefanikiwa kubaki Ligi Kuu baada ya kushinda mchezo wa mwisho wa playoffs dhidi ya Fountain Gate kwa jumla ya mabao 4-2, ambapo kwa sasa imeanza tayari mipango ya msimu ujao.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha mkuu wa timu hiyo, Aman Josiah ambaye hata hivyo mkataba wake umemalizika, amesema iwapo atabaki kikosini, hatamuonea mtu wala kupendelea yeyote bali namba za kila mmoja ndio zitaamua.
Amesema anachojivunia ni heshima aliyopewa na Prisons kwa kumuamini kumpa majukumu na kumtambulisha Ligi Kuu kwa mara ya kwanza, hivyo msimu ujao hatahitaji tena presha iliyotokea msimu huu uliomalizika.
“Pamoja na kucheza playoffs, lakini nashukuru timu imebaki salama na ndio ilikuwa mpango na sharti nililopewa, natarajia baada ya siku tatu nitawasilisha ripoti yangu kwa menejimenti.
“Kwa ujumla lazima mabadiliko yawepo japokuwa itategemea kama nitarudi kikosini ila sitampendelea au kumuonea yeyote badala yake namba za kila mchezaji ndizo zitaamua,” alisema Josiah.
Kocha huyo amekiri ligi kuwa ngumu akieleza kuwa wachezaji kila mmoja kwa nafasi yake alionyesha uwezo na juhudi binafsi na kwamba iwapo angeanza mapema na timu hiyo wangefanya makubwa zaidi.