Majaliwa: WCF jengeni tabia ya kutembelea maeneo ya kazi

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka watendaji wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kujenga tabia ya kutembelea maeneo ya kazi ili kuona mazingira ambayo wafanyakazi wanafanyia kazi.

Sambamba na hilo, amewaagiza waajiri kutoa taarifa za wafanyakazi wao kwa wakati pindi wanapopatwa na madhila ili waweze kuhudumia na kutoa michango yao kwa wakati.

Majaliwa ameyasema hayo leo Julai 4, 2025 katika kilele cha maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa mfuko huo yaliyofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam ambapo alimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema kwa WFC kujenga tabia ya kutembelea maeneo ya kazi kutasaidia kuhakikisha hapatengenezi changamoto mahala pa kazi kwa wafanyakazi.

“Wakati WCB ikipasawa kuyafanya haya na nyie wadau hakikisheni mnakuwa na maeneo mazuri ya ufanyaji kazi ili kuepusha ajali kazini,” amesema Majaliwa.

Kuhusu uwasilishaji michango, amesema moja ya changamoto iliyotajwa katika kuendesha mfuko huo ni pamoja na waajiri kutowasilisha michango na kutotoa taarifa za wafanyakazi wao kwa wakati, na kubainisha kuwa kufanya hivyo ni kutotimiza wajibu na kutowatendea haki wafanyakazi wao.

Wakati kaulimbiu ya maadhimisho hayo ikiwa imebeba ujumbe usemao: “Miaka 10 ya fidia kwa wafanyakazi iendelee”, Majaliwa amesema imebeba ujumbe mzito unaoakisi mafanikio ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa mfuko huo.

“Pia, kaulimbiu hiyo inatoa wito kwa wadau wote wakiwemo waajiri na wafanyakazi wenyewe, lakini na Serikali kuhakikisha kazi inayoendelea kwa tija lakini wakati huohuo wafanyakazi wanalindwa kutokana na madhila yanayowakumba katika maeneo yao ya kazi.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuimarisha utekelezaji wa sheria ya fidia kwa wafanyakazi ili waajiri wengi wajisajili na kuchangia mfuko huo.

“Sio hilo tu pia, kutoa taarifa za ajali, magonjwa na vifo vya wafanyakazi kwa wakati kwani hii itawezesha taasisi yetu kuchukua hatua stahiki kuwahudumia waathirika kwa haraka, kwa imani tunapoitekeleza kauli hii tutaendelea kuishi ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea wananchi maendeleo na kuboresha maisha yao,” amesema Ridhiwani.

Awali, Mkurugenzi wa WCF, Dk John Mduma amesema maadhimisho hayo yamelenga kujadili mambo matano ikiwemo kuenzi mazuri yaliyofanyika hadi sasa, kuwashukuru wadau mbalimbali na kuonyesha kuwa wanathamini mchango wao katika safari yao hiyo ya miaka 10.

Jingine ni kuchochea ari ya kuendelea kutoa huduma bora zaidi, kuongeza ushirikiano na wadau wao na kupanua wigo wa kuhamasishana na kubadilishana maarifa na taarifa katika taasisi wanazofanana.

 “Pia, tunaipongeza Serikali kwa kupunguza kiwango cha riba kwa waliokuwa wanachelewesha michango kutoka asilimia  10 kwa mwezi hadi mbili  hatua ambayo imeongeza imani kwa wawekezaji wa WCF na kwa Serikali kwa ujumla,”amesema Dk Kaduma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Suzane Ndomba amesema huduma WCF hazijawa tu na faida katika kutoa fidia bali pia kutatua changamoto.

Mwakilishi kutoka Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Rehema Ludanga amesema: “Pamoja na kuwa na vifurushi mbalimbali lakini kuna hili la kifurushi cha utengamano ambacho mfanyakazi akipata  ulemavu atasaidiwa kupata ujuzi, ambao utamrudisha kwenye hadhi yake ya kujikimu kimaisha na familia yake lakini kuweza kuleta tija katika Taifa,” amesema.

Related Posts