Ruvuma. Abiria 30 wamenusurika baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutumbukia kwenye korongo jirani na daraja la Ruvuma wilayani Songea mkoani hapa.
Basi hilo lililokuwa linaelekea mpakani mwa Tanzania na Msumbiji, limepata ajali hiyo leo Ijumaa Julai 4, 2025, huku ikielezwa kuwa watu 14 wana hali mbaya kutokana na majeraha na wamelazwa Hospitali ya Rufaa Songea kwa matibabu zaidi.
Akizungumza na Mwananchi Digital, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya amesema basi hilo lijulikanalo kwa jina la Karim, lilikuwa likitokea Stendi ya Majengo kuelekea Mkenda.
“Dereva alipofika daraja, kutokana na ufinyu wa daraja hilo, alitaka kupishana na dogo aina ya Toyota Hilux ndipo likatumbukia kwenye korongo darajani hapo,” amesema kamanda huyo.
Hata hivyo amesema hakuna kifo kilichotokea mpaka sasa kutokana na ajali hiyo na tayari abiria 16 wamepatiwa matibabu na kuruhusiwa kuendelea na safari.
Shuhuda wa ajali hiyo, askari mgambo wa Kata ya Ruvuma, Kachitawe Kachitawe, amesema alifika mapema eneo la ajali na kutoa taarifa kituo cha polisi na viongozi wa usalama barabarani walifika kwa wakati kutoa msaada kwa abiria.
“Abiria walipata msaada wa haraka ndiyo maana wamenusurika, binafsi nilishukuru Jeshi la Zimamoto na Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma, nilipowapa taarifa tu wakafika mara moja kuwasaidia majeruhi kuwapeleka hospitali na kuokoa mali zao, yaani mizigo yote iko salama,” amesema shuhuda huyo.