Polisi yawaonya wanaojitokeza kila Jumapili Ubungo Kibo kwa nia ya kufanya vurugu

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewatahadharisha na kutoa onyo kwa kundi la watu wanaojitokeza kutoka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Afrika Mashariki (KKAM) kila Jumapili kwa nia ya kuingia barabarani na kufanya vurugu.

Onyo hilo limetolewa leo Jumamosi, Julai 5, 2025 na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala ya usalama katika jiji hilo.

Wiki tatu mfululizo, waumini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima wamekuwa wakiendesha ibada karibu na eneo la kanisa hilo lililofutiwa usajili na Serikali Juni 2, 2025.

Akizungumza bila kulitaja moja kwa moja jina la waumini wa Gwajima wala KKAM, Kamanda Muliro amesema kwa wiki mbili mfululizo zilizopita, kundi la watu limekuwa likitoka kanisani Ubungo Kibo baada ya ibada, wakiwa na mabango.

 “Kundi hilo limekuwa likitoka na mabango baada ya ibada, wakati wenzao wakitawanyika kwa amani kuendelea na kazi nyingine. Lakini wao huanza kupiga makelele na kutaka kuingia barabarani kwa nguvu kwa lengo la kufanya vurugu,” amesema Kamanda Muliro.

Ameongeza kuwa, Jeshi la Polisi linawatakia wananchi wote wema waendelee na ibada katika maeneo yaliyo rasmi kisheria, bila kuwa na nia ya kuvunja sheria za nchi.

Related Posts