Camara ajadiliwa Simba, mabosi watoa msimamo

KIKAO cha mabosi wa Simba kimefikishiwa makosa aliyofanya kipa Moussa Camara yalivyoigharimu timu msimu uliomalizika, kisha ukafanyika uamuzi juu ya nyota huyo raia wa Guinea.

Camara ambaye alitua Simba mwanzoni mwa 2024-2025 akitokea Horoya ya Guinea ndiye amekuwa kipa namba moja kikosini baada ya Ayoub Lakred kuwa na majeraha ya muda mrefu na kuondolewa kwenye usajili wa msimu huo.

Licha ya kuonyesha kiwango bora, lakini kuna makosa aliyofanya katika baadhi ya mechi za ligi yaliyoigharimu Simba na kujikuta ikiukosa ubingwa msimu wa nne mfululizo kwa tofauti ya pointi nne. Taarifa za ndani zimeliambia Mwanaspoti kuwa: “Makosa ya Camara hata mabosi wameyaona na ndio yaliyofanya benchi la ufundi kutafutiwa kipa bora zaidi yake kwa ajili ya msimu ujao.

“Lakini kama atakosekana ambaye atakuwa bora zaidi, basi hakutakuwa na namna ataendelea kuitumikia Simba kwa msimu ujao lakini lazima abadilike.”

Camara ambaye alicheza mechi zote za kimataifa za Simba ikicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kupoteza mbele ya RS Berkane ya Morocco.

Katika ligi Camara aliyecheza mechi 28 kwa dakika 2,520 kati ya mechi 30, ndiye ameibuka kinara wa clean sheet akimaliza na 19, huku akiruhusu mabao 13.

Miongoni mwa makosa aliyofanya yaliyoigharimu Simba ni mechi mbili za ligi dhidi ya Yanga Oktoba 19, 2024 mpira wa faulo uliopigwa na Clatous Chama dakika ya 86 ukionekana kwenda nje aliufuata na kujikuta anaurudisha ndani Maxi Nzengeli akaupiga haraka Kelvin Kijili akajifunga, likawa bao pekee lililoipa Yanga ushindi wa 1-0.

Pia Juni 25, 2025 alitoka golini na kwenda kumfanyia faulo Pacome Zouzoua Simba ikaruhusu bao la kwanza na kupoteza kwa mabao 2-0.

Kabla ya hapo, katika sare ya 2-2 dhidi ya Coastal Union, Oktoba 4, 2024 alifanya makosa mawili yaliyozaa mabao wakati Simba ikiwa mbele kwa 2-0 na mwisho mchezo ukaisha sare ya 2-2.

Related Posts