-Mkurugenzi Mtendaji Twange amkabidhi Jiko Janja
-Ni katika kuhamasisha Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi leo tarehe 07 Julai, 2025 ametembelea Banda la Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayoendelea katika Viwanja vya Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam na kujionea namna TANESCO inavyoelimisha umma kuhusu kazi inazozifanya.
Rais Mwinyi ameangalia utekelezaji wa Miradi mbalimbali ya Kimkakati inayofanywa na TANESCO kwa njia ya video katika chumba cha sinema kilichopo Bandani hapo ambapo miradi mingi imekamilika na kupata maelezo ya kazi zinazofanywa na Idara mbalimbali zikiwemo yaHuduma kwa Wateja, Uwekezaji na Miradi.
Rais Mwinyi pia amejionea namna TANESCO inavyotekeleza kwa kasi uelimishaji umma kuhusu Kampeni ya Kitaifa ya Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na kuona vifaa mbalimbali vya kupikia vinavyotumia umeme kidogo.
Rais Mwinyi pia ametembelea Banda la Wizara ya Nishati, Kampuni Tanzu ya TANESCO ya Ujenzi wa Miundombinu ya Umeme (ETDCO) na Kampuni ya Tanzu ya TANESCO ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) na kupata maelezo kuhusu kazi mbalimbali wanazozifanya.
Akihitimisha ziara yake katika Banda la TANESCO, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Lazaro Twange, amemkabidhi Rais Mwinyi zawadi ya Jiko Janja ikiwa ni alama ya kuhamasisha matumizi ya umeme kama Nishati nafuu zaidi jikoni.
Mkurugenzi Mtendaji Twange amesema, TANESCO imepata heshima kubwa ya kutembelewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na kupata fursa ya kumueleza kazi zinazofanywa na TANESCO.