Dira 2050 yakamilika, Rais Samia kuizindua Julai 17 Dodoma

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, Alhamisi ya Julai 17, 2025 katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Dira hiyo inayoitwa ‘Dira 2050’ inakwenda kuzinduliwa baada ya kupitia hatua 12 zinazotakiwa huku ikiwa ni dira ya  pili ya ya maendeleo ya Taifa ambayo haina uelekeo wa kiitikadi ya chama.

Hayo yamesemwa leo Jumanne, Julai  8, 2025 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais- Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo katika mkutano wake na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF)  jijini Dar es Salaam akielezea mchakato mzima wa Dira 2050.

Profesa Mkumbo amesema hadi dira hiyo inakamilika watu milioni 1.17 walifikiwa na kutoa maoni yao ambapo njia saba zilitumika ikiwemo utafiti katika ngazi ya kaya ambapo watu zaidi 15,000 walifikiwa.


Njia nyingine ambazo zilitumika ni kukusanya kwa njia ya simu nchi nzima ambapo wananchi walipigiwa na kuulizwa vitu tofauti, ujumbe kwa njia ya simu (USSD) ambapo watu 1.19 milioni walifikiwa na asilimia 82 wakiwa vijana chini ya miaka 36.

“Pia kupitia tovuti maalumu na hadi Desemba mwaka jana watu 13,459 walitoa maoni, tulifanya makongamano 12 ambapo watu 22,779 walihudhuria,  viongozi waliopo madarakani na wastaafu 44 walihojiwa kutoa maoni yao.

Semina mbalimbali zilifanyika, kukusanya nyaraka 33 zinazoelezea historia ya maendeleo ya Tanzania na zilichambuliwa ,” amesema Profesa Mkumbo.

Mchakato rasmi wa maadalizi wa Dira 2050 ulizunduliwa ramis Aprili 3, 2023 na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ambapo baada ya kuzinduliwa mchakato wa kuunda vyombo vya kitaasisi vya kusimamia uandishi wa dira ulianza.


Hapo iliandaliwa sekretarieti ya kuandika Dira kupitia Tume ya Mipango chini ya aliyekuwa Katibu Mtendaji wake, Marehemu Lawrence Mafuru, timu kuu ya kitaalamu ya kuandika Dira.

“Baadaye tulifanya tathmini ya utekelezaji wa Dira 2025 kabla ya kuanza uandishi wa dira 2050 ambapo tuliangalia mafanikio na changamoto zilizoonekana,” amesema Profesa Mkumbo.

Baada ya hayo kufanyika ripoti ya thamini hiyo ilizindukiwa Desemba 9, 2023 kwenye mkutano wa kwanza wa kitaifa wa Dira uliofanyika mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan na hapo nyenzo za kukusanya maoni ya wananchi na wadau zilizinduliwa ili kupata maudhui ya dira.

“Baadaye tukaanza kazi ya kukusanya maoni ya wananchi na wadau wa maendeleo juu ya matarajio yao ya nini kiingie katika dira 2050 lilikuwa zoezi pana na shirikishi nchi nzima na liligusa wadau na wananchi,” amesema huku akieleze njia zilizotumika na waliofikiwa.

Mbali na kukusanya maoni pia walijifunza kutoka nchi zilizopiga hatua za kimaendeleo katika bara la Afrika, Asia na Ulaya  huku baadhi ya nchi walizojifunza ni Botswana, Moroco, Mauritius, Afrika Kusini na Kenya.

Katika hatua ya saba, ulifanyika uchambuzi, uandishi na uhariri wa taarifa mbalimbali na kutoa rasimu ya kwanza ya dira ambayo ilizinduliwa Desemba 2024 na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi.

Baadaye rasimu hiyo ilirudishwa kwa wadau ili kupata maoni ya kiuhariri, kukutana na wadau mbalimbali, waandishi, vyama vya siasa 19 ili kuhakikisha kunakuwa na sauti ya pamoja na naadaye walipitia maoni ya wadau yaliyotolewa na kuyafanyia kazi.

“Hatimaye Machi 28, 2025, rasimu ya pili ya dira ya taifa ya maendeleo ilikabidhiwa kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na baadaye nikakabidhiwa mimi (Profesa Kitila Mkumbo) na kumtaka aingize katika mchakato wa serikali wa kufanya maamuzi,” amesema Profesa Mkumbo.

Kwa mujibu wake, Dira hiyo kwa mara ya kwanza katika baraza la mawaziri kwa Juni 22, 2025 kwa ajili ya kuidhinishwa kabla ya kuwasilishwa bungeni Juni 26, 2025 ambapo Bunge liliridhia rasmi ikiwa ni hatua ya kuiwekea ulinzi wa kikatiba kwa ajili ya utekelezaji wa muda mrefu.

“Rais alisisitiza dira hii ipelekwe bungeni ili iwe na uhalali wa kitaifa na kulindwa na mihimili ya dola. Hii ni kwa sababu itatekelezwa na marais wasiopungua wawili, watatu au wanne,” amesema Profesa Mkumbo.

Licha ya Profesa Kitila kusema Bunge lilipitisha azamio la kuilinda Dira 2050 yenye kauli ‘Tanzania Tuitakayo’, maswali mengi ya wahariri miongoni wametaka itungwe sheria ya kuilinda dira hiyo.

Profesa Kitila amesema amechukua ushauri huo wa wahariri na Serikali inakwenda kulifanyia kazi kwani utekelezaji wake wa Dira 2025/2050 utaanza Julai 1, 2026.

Profesa Kitila amesema siku ya uzinduzi, wataeleza mambo mengi yaliyomo kwenye Dira 2050.

Profesa Mkumbo amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeonyesha mfano kwani Ilani yake imeshabihiana na kile kilichoainishwa katika Dira 205 huku akitamani na vyama vingine kuiga mfano huo.

 “Tunatamani kuona tunakuwa na sauti ya pamoja kama vyama vingine, hivyo hatutarajii kuona ilani ya vyama vya siasa vingine inayoenda tofauti na maudhui ya dira hii,” amesema Profesa Mkumbo.


Ujumbe wake uliungwa mkono na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini Tanzania (TEF), Deodatus Balile ambaye amesema ni muhimu vyama vya siasa nchini vyenye kushiriki uchaguzi mkuu kuwa na Ilani za uchaguzi zenye kuakisi malengo na mipango iliyopo kwenye Dira 2050.

Hiyo itasaidia kuwa na mtazamo wa pamoja wa Tanzania ambayo inatazamisa kufikia 2050.

“Niseme sisi tumejipanga kutangaza habari zinazohusiana na Dira ya Taifa ya mwaka 2025/50 na dira hii si kwaajili ya Chama Cha Mapinduzi pekee maana baadhi ya watu wanaweza wakachanganya kuwa hii Dira ni ya CCM,” amesema Balile.

“Vyama vyote vya siasa vinavyoenda kuandika ilani zao inapaswa kuakisi Dira hii,” amesisitiza.

Related Posts