Serikali yachunguza waziri aliyejipiga risasi Urusi

Serikali ya Urusi imeanza uchunguzi kutokana na kifo cha aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi wa Urusi, Roman Starovoit  ambaye amekutwa amefariki dunia karibu na gari lake katika eneo la Moscow saa chache baada ya Rais Vladimir Putin kumfuta kazi jana.

Taarifa iliyoripotiwa na Al Jazeera leo Julai 8, 2025, imeeleza kuwa waziri huyo wa aliyepita ambaye mara ya mwisho  alihudhuria kikao huko Mineralnye Vody Mei 6, 2025, kifo chake kimeibua utata na kuzilamu mamlaka kuanzisha uchunguzi wa kina.

Shirika la Uchunguzi wa Jinai la Urusi linachunguza kifo cha Roman Starovoit, waziri wa zamani wa uchukuzi ambaye mwili wake ulikutwa na jeraha la risasi karibu na gari lake, saa chache baada ya Rais Vladimir Putin kumfuta kazi.

Mamlaka zinasema kuwa mwili wa mwanasiasa huyo mwenye miaka 53, ulipatikana jana Julai 7,2025 karibu na gari la Tesla lililokuwa jirani na bustani katika eneo la Moscow, huku bastola iliyosajiliwa kwa jina la Starovoit ikipatikana eneo hilo alipokutwa amefariki dunia.

Kamati ya Uchunguzi ya nchi hiyo imefungua kesi ili kubaini mazingira kamili ya kifo chake, ikieleza kuwa huenda ilikuwa ni kujiua. Vyombo vya habari vya Urusi, vikinukuu vyanzo vya usalama vikisema jeraha hilo la risasi linaonekana kuwa alijijeruhi mwenyewe.

Awali, Rais Putin alitoa amri Jumatatu kumfuta kazi Starovoit kama Waziri wa Uchukuzi, nafasi aliyokuwa ameshikilia kwa zaidi ya mwaka mmoja. Hakuna sababu iliyotolewa kwa uamuzi huo.

Wachambuzi wa kisiasa waliunganisha haraka uamuzi huo na uchunguzi wa muda mrefu wa ufisadi katika Mkoa wa Kursk, ambako Starovoit aliwahi kuwa gavana.

Uchunguzi huo unaotajwa unahusu kubaini iwapo Dola milioni 246 zilizotengwa mwaka 2022 kuimarisha ulinzi wa mipaka ya Kursk zilifujwa.

Fedha hizo zilikuwa zimeelekezwa kuimarisha mpaka wa Urusi na Ukraine, lakini wanajeshi wa Ukraine walifanya shambulio la kuvuka mpaka katika eneo hilo miezi mitatu baada ya Starovoit kuteuliwa kuwa waziri.

Related Posts