MABOSI wa Yanga hawataki utani. Hilo limeonekana baada kuamua jambo kuhusiana na kiungo mshambuliaji raia wa Ivory Coast.
Yanga imeshinda mataji yote ya ndani iliyoshiriki msimu uliomalizika na sasa inaanza mapema kujipanga kwa ajili ya kufanya makubwa zaidi msimu ujao.
Na katika hilo, mabingwa hao mara 31 wa Ligi Kuu Bara wanaendelea kufanya usajili wa kimya kimya kwa kumpa mkataba wa miaka miwili kiungo mshambuliaji raia wa Ivory Coast aliyekuwa amefichwa katika kambi ya timu akijifua hata kabla ya Dabi ya Kariakoo kama Mwanaspoti lilivyoripoti mapema.
Mbali na kumsainisha kiungo huyo, Mohamed Doumbia aliyekuwa akicheza soka la kulipwa katika klabu ya FC Majestic y Burkina Faso na Slovan Liberec ya Jamhuri ya Czech, lakini mabosi wa Yanga wameendelea kumbakisha kiungo mkabaji, Khalid Aucho kwa kumpa mkataba wa mwaka mmoja.
Tuanze na Doumbia. Ile kauli ya Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said kwamba katika kikosi cha klabu hiyo, akitoka mchezaji mzuri anaingia bora zaidi imeanza kutekelezwa, kwani tayari imemsajili kiungo fundi mwenye uwezo wa kucheza zaidi ya nafasi moja.
Kiongozi huyo alitoa kauli hiyo wakati wakisherehekea mafanikio yao ya msimu uliyoisha, yaliyofanyika kwenye makao makuu ya klabu hiyo Jangwani, Kariakoo.
Yanga imemsainisha mkataba wa miaka miwili Doumbia mwenye umri wa 26 akitokea SC Majestic ambaye ana kasi na uwezo wa kucheza namba nane na 10.
Usajili wa Doumbia unakuja kuongeza nguvu eneo hilo ambalo limeondokewa na Stephane Aziz KI aliyesajiliwa Wydad Casablanca.
Chanzo cha ndani kutoka katika klabu hiyo kilisema:”Doumbia bado umri wake ni mdogo na mchezaji mzuri, tunaboresha kikosi kuhakikisha tunaendeleza mafanikio ambayo tumeyapata miaka minne mfululizo pia kufanya vizuri Ligi ya Mabingwa Afrika.”
Huu unakuwa ni usajili wa kwanza rasmi kwa Yanga kwa ajili ya msimu wa 2025/26 na kwamba Doumbia anasifika kuwa na uwezo mkubwa wa kupiga pasi za mwisho, kumiliki mpira na kusaidia safu ya ushambuliaji.
Siku moja kabla ya Dabi, Mwanaspoti lilinasa taarifa za kiungo mshambuliaji huyo kufichwa kambini Yanga akijifua na nyota wa kikosi hicho kutokana na kuwa nje ya uwanja tangu Machi mwaka huu alipoachana na Majestic, lakini akiwa ameshapita Slovan Liberec ya Czech, Dukla Pague na Ekana IF ya Finland.
Nyota huyo amenukuliwa katika mahojiano na vyombo vya habari vya Ivory Coast akisema; “Najivunia kujiunga na timu kubwa kama Yanga. Lengo langu ni kutwaa makombe na kufanya historia Tanzania.”
Ukiachana na Doumbia, Yanga pia imemaliza utata kwa kiungo mkabaji, Khalid Aucho kwa kumpa mkataba wa mwaka mmoja ili aendelee kusalia klabuni hapo.
“Tunaheshimu mchango wa Aucho ambaye uzoefu wake unaonekana uwanjani, hivyo yeye na Doumbia mwenye kasi uwepo wao, kuna kitu kikubwa kitaongezeka katika eneo hilo,” kilisema chanzo hicho.
Aucho alikuwa ni miongoni mwa wachezaji waliomaliza mikataba na klabu hiyo na mabosi wameanza naye kwa kumpa mkataba huo mpya, wakiendelea kuzungumza na wengine ili kuwabakisha wakati, ikielezwa kocha mpya atakayechukua nafasi ya Miloud Hamdi tayari yupo nchini akiwa amesaini mkataba na bado kutambulishwa tu. Ingawa Yanga amefanya siri, lakini kocha huyo mpya ni Mfaransa Julien Chavelier aliyekuwa akifundisha Asec Mimosas.