Simba yavamia dili la Ecua Yanga

HUENDA hii isiwe taarifa nzuri kwa mashabiki wa Yanga ambao walikuwa wakianza kuchekelea chinichini baada ya kuwahabarisha juu ya dili la straika wa ASEC Mimosas na MVP wa Ligi Kuu ya Ivory Coast (Ligue 1), Celestin Ecua lililobaki hatua chache kabla ya kutua Jangwani.

Ndio, Yanga inadaiwa kuwa ipo hatua nzuri ya kumnasa Ecua aliyehusika na mabao 27 katika mechi 30 za ligi msimu ulioisha akifunga mabao 15 na kutoa asisti 12, lakini ghafla watani wao, Simba imedaiwa wameingiza mkono na kuibua utata mkubwa.

Ipo hivi. Utata umeibuka katika mchakato wa mshambuliaji huyo baada ya kudaiwa, Simba imeamua kuingiza mkono katika dili la kujiunga na Yanga na wakati wowote sakata hilo linaweza kutua FIFA.

Inadaiwa kuwa, Yanga na Simba zote zimefanya mawasiliano ya kutaka saini ya Ecua aliyekuwa akiitumikia Asec kwa mkopo kutoka Zoman FC na ilielezwa Yanga ilikuwa katika hatua nzuri ikiwamo kumtangulizia kabisa mkataba ili ausome kabla ya kuusaini.

Mwanaspoti, imejiridhisha kuwa, mabosi wa klabu ya Yanga na Simba kwa vipindi tofauti wamekuwa wakifanya mazungumzo na kampuni ya uwakala wa wachezaji na makocha ya WA Football.

Hata hivyo, wakati mazungumzo hayo yakiendelea inaelezwa ghafla mabosi wa Yanga wakapita njia nyingine kuwahi saini ya Ecua na mambo yakaanza kutibuka na hasa baada ya menejementi hiyo kushtuka inataka kuzidiwa akili, lakini ikiendelea kuwasikilizia Simba wanaoendelea hadi sasa.

Inadaiwa, Ecua alisaini mkataba Machi, 2025 na kusimamiwa na kampuni hiyo inayomilikiwa na raia wawili wa Morocco ambayo pia katika ukurasa wake wa Instagram ameandika anasimamiwa na Waarabu hao.

Yanga ilikuwa kwenye hatua za mwisho kumpa mkataba mshambuliaji huyo baada ya kufikia makubaliano na Zoman, lakini kampuni inayommiliki imeliambia Mwanaspoti kuwa endapo maku-baliano yatakamilika wataiburuza klabu hiyo na mchezaji FIFA kwa kumshawishi nyota huyo mwenye mkataba.

Wakati Yanga iliwekewa mtego huo, Simba nayo inaendelea kusukuma dili hilo ikiwatumia Wamorocco hao ambao pia wanahusika na umiliki wa kiungo mshambuliaji wa Wekundu hao, Ellie Mpanzu.

Simba inawatumia Waarabu hao kama fimbo ili kuwabadilisha akili Zoman na kuwageuza kisha kuinasa saini ya Ecua kirahisi kupitia mgogoro huo, ikizingatiwa kuwa katika pendekezo la kocha Fadlu Davids anahitaji straika wa maana ili kuimarisha eneo la ushambuliaji.

Mwanaspoti jana Jumatatu lilifanikiwa kumpata mmiliki wa kampuni hiyo ya WA Football, Anas El Amran aliyekiri kuwepo kwa mgogoro huo akisema wameshangazwa na hatua ya Yanga kutaka kuwazunguka kwenye mazungumzo ya usajili wa mshambuliaji huyo.

“Ni kweli kuna hiyo shida, tulianza vizuri mazungumzo na kiongozi mmoja wa Yanga (anamtaja) lakini hapa kati akawa kimya, baada ya muda mchezaji akatufuata na kutueleza kumbe mazungumzo yanaendelea na Yanga wanamtumia meneja mwingine,” alisema Amran na kuongeza;

“Tulimtafuta yule kiongozi (anamtaja), lakini bahati mbaya sana majibu yake hayakuwa mazuri kwetu, tukamwambia mchezaji awe makini maana tukishasikia ameshasaini Yanga tutafungua kesi dhidi yake na hiyo klabu.

“Tuna mkataba na Ecua wa miaka miwili, ndio maana hata kwenye Instagram yake ameweka jina letu, kufanya mazungumzo yoyote nje na sisi sio sawasawa tutawashtaki Fifa na watatulipa fedha nyingi.”

Alipoulizwa kuhusu kufanya na mazunguzo na Simba ili kumnasa nyota huyo, alisema; “Ni kweli tunaendelea na mazungumzo na klabu, nyingine mbili ni za hapo Tanzania na nyingine za Afrika Kaskazini, tutakazokubaliana nazo tutamshirikisha mchezaji na klabu yake tutamalizana dili.”

Related Posts