Shinyanga. Watu wanaofanya kazi katika maeneo yanayozalisha vumbi ikiwemo migodini, mashineni na maeneo mengine kama hayo wametajwa kuwa hatarini kuugua ugonjwa wa Silicosis.
Ugonjwa huo husababishwa na chembechembe za silica zinazopatikana kwenye miamba, udongo na vumbi.
Daktari wa magonjwa ya ndani kutoka Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga, Yohana Bunzari amesema kuwa kitaifa hakuna takwimu halisi zinazoonyesha wagonjwa wa ugonjwa wa Silicosis, lakini utafiti uliofanywa mwaka 2023 katika mgodi wa Mererani yanakochimbwa madini ya Tanzanite ulionyesha kati ya wafanyakazi 80 asilimia 30 walibainika kuwa na ugonjwa huo.
Akizungumza na Mwananchi Julai 07, 2025 kwa njia ya simu Dk Bunzari ameeleza namna ugonjwa huo unavyoweza kusababisha kuugua magonjwa mengine yakiwemo ya kuambukiza kama kifua kikuu.
“Mtu anapovuta hewa yenye vumbi ambayo huwa na chembechembe za silica dalili zake huanza kuonekana baada ya miaka 10 hadi 20 kutoka kipindi ambacho amevuta hewa hiyo, ambayo huathiri mapafu kwa kutengeneza kovu ambalo huathiri mfumo wa upumuaji na kusababisha kifua kikuu” amesema Dk Bunzari.
Athari nyingine za Silicosis
“Kutokana na kuathirika kwa mfumo wa upumuaji, Silicosis inaweza kusababisha magonjwa mengine kama moyo, kansa ya mapafu na kudhoofisha kinga ya mwili,” amesema Dk Bunzari.
Imeelezwa kuwa baadhi ya wanaofanya kazi katika maeneo yaliyoainishwa na wanaoponda kokoto hawana uelewa wa ugonjwa huo.
“Hatuna jinsi inabidi tupambane kujipatia kipato kuna familia zinatuangalia, nina wajukuu watatu nyumbani wananitegemea, malipo ya kuponda yanategemea na makubaliano na muajiri wako na kiasi ulichoponda,” amesema Aisha Hamis.
“Kazi hii tunafanya kama bahati nasibu, kwa sababu unaweza chimba unaambulia madini kidogo sana hata vifaa vyetu si vya kisasa, lakini unatokea tu bahati kwenye kuosha mchanga unaweza bahatisha,” amesema William Shija.
“Tunashauriwa kujinga na vumbi kwa kuvaa barakoa isiyopitisha vumbi lakini barakoa yenyewe gharama utanunua ngapi, na zinawahi kuharibika na wakati mwingine unaamua kuivua hasa nikiwa nazungumza,” amesema Hamida Hamidu.
“Sijui chochote kuhusu ugonjwa huo (Silicosis) ninachofanya nikimaliza kazi zangu huwa napita kwa wauza tangawizi nakunywa hata kikombe kimoja cha mia mbili kisha naenda zangu nyumbani,” amesema Bashiru Juma.
Kwa mujibu wa Dk Bunzari ugonjwa huo hauna tiba yoyote kwa sababu unakuwa ni wa muda mrefu na hadi kugundulika kwake unachukua miaka mingi, kwa kipindi hicho chote unakuwa umeshakuwa sugu ndiyo maana watu hushauriwa kuwa na tabia ya kufanya vipimo, kujua afya zao ili kama kuna magonjwa mengine yajulikane mapema.
Baadhi ya wadau wametoa maoni yao yanayolenga katika kulinda afya za wafanyakazi hao katika maeneo ya kazi ikiwa pamoja na kuweka mfuko unaowahudumia na sheria inayowalinda.