Bulyanhulu. Kampuni ya Barrick imewekeza Dola 4.79 bilioni za Marekani(Sh12 trilioni) katika uchumi wa Tanzania katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Barrick imeeleza hayo Jumatatu ya Julai 7, 2025 huku ikisisitiza dhamira yake ya kutoa thamani shirikishi na maendeleo ya muda mrefu nchini.
Kwa mujibu wa Barrick kati ya kiwango hicho Dola 558 milioni (Sh1.4 trilioni) ziliingizwa katika nusu ya kwanza ya mwaka 2025, wakati kampuni hii kubwa ya madini ikiongeza juhudi zake za kujipambanua kama mshirika wa mfano katika mageuzi ya kiuchumi ya Tanzania.
Uwekezaji huu unafuatia kuanzishwa kwa Kampuni ya Twiga Minerals mnamo Januari 2020. Twiga ni ubia kati ya Barrick na Serikali ya Tanzania uliolenga kusimamia shughuli za uchimbaji wa madini za kampuni hiyo nchini.
Kwa makubaliano hayo, Serikali inamiliki hisa asilimia 16 huku Barrick ikimiliki asilimia 84, na manufaa ya kiuchumi yakigawanywa kwa usawa baada ya kampuni kurejesha uwekezaji wake.
“Wakati tulipoanzisha Twiga, haikuwa tu kwa ajili ya kutatua changamoto za zamani. Ilikuwa ni kujenga mustakabali mpya kwa kufungua utajiri wa dhahabu wa Tanzania kwa namna inayohakikisha kugawana faida kwa haki na kuunda thamani ya muda mrefu,” amesema Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa Barrick, Mark Bristow, wakati akiwasilisha taarifa ya kampuni hiyo kwa robo ya pili ya mwaka 2025.
Bristow amebainisha kuwa, Barrick imekuwa mchangiaji mkuu wa sekta ya madini katika uchumi wa Tanzania, ikitambuliwa kufanya vizuri katika maeneo kama usalama, matumizi ya bidhaa na huduma za ndani, elimu, ulipaji kodi, gawio na uboreshaji wa miundombinu.
Asilimia 90 ya ununuzi wa kampuni unafanywa kwa wasambazaji wa Kitanzania, asilimia 83 kati yao ni wazawa kabisa na Watanzania wanaunda asilimia 95 ya wafanyakazi wote wa Barrick, huku karibu nusu wanatoka kwenye jamii zinazozunguka migodi.
Kadhalika Bristow alizungumzia miradi kadhaa ya kijamii, ikiwamo mpango wa upanuzi wa miundombinu ya shule wenye thamani ya Dola 30 milioni za Marekani na ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 73 inayounganisha Bulyanhulu na Kahama.
Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa, amesifu uwazi na mchango wa Barrick, akibainisha kuwa, Serikali inapanga kuhitaji kampuni zote za madini kutoa taarifa za matokeo ya uendeshaji kila robo mwaka.
“Serikali inaridhishwa na mchango wa Barrick katika uchumi wa taifa na uwazi wake. Inatoa mfano kwa wadau wengine katika sekta hii,” amesema.