Mwanza. Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando imesema magonjwa ya ngozi yameongezeka kwa wananchi kutokana na mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa hali ya hewa na wananchi kupuuza dalili na mabadiliko yanayotokea kwenye ngozi wakidhani ni sehemu ya ukuaji wa mwili.
Kupitia kliniki ya ngozi, nywele na kucha, Bugando inahudumia wagonjwa wasiopungua 50 kila siku wanaofika kufanya uchunguzi na kupata matibabu.
Kutokana na ongezeko hilo, katika kuadhimisha siku ya afya ya ngozi duniani ambayo huadhimishwa Julai 8 ya kila mwaka, Bugando imeandaa kliniki na kutoa huduma za uchunguzi, ushauri na matibabu ya magonjwa ya ngozi bure kutoka kwa madaktari bingwa.
Hayo yamesemwa leo Jumanne Julai 8, 2025 na Mkuu wa Idara ya magonjwa ya ngozi Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Dk Nelly Mwageni wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye kliniki ya uchunguzi, ushauri na matibabu, ambayo imefanyika eneo la Nera jijini Mwanza.
Dk Mwageni amesema katika kliniki zao wanabaini zaidi magonjwa ya pumu ya ngozi, maambukizi hasa fangasi kwenye ngozi, kucha na nywele, magonjwa ya upele na muwasho, bakteria hasa kwa watoto wadogo na virusi.
Amesema kutokana na changamoto hiyo imewalazimu kuandaa kliniki hiyo ili kuongeza uelewa kwa wananchi na kuendelea kuelimisha kwamba magonjwa ya ngozi yapo, hivyo waathirika wafike mahali sahihi ili kupata huduma sahihi.
”Mpaka sasa wagonjwa wengi tunaowaona hapa wanalalamika muwasho kwenye ngozi, vipere vinavyowasha na sehemu kubwa tumeona ni sababu ya mazingira magonjwa kama ya pumu ya ngozi, maambukizi kwenye ngozi, vipere vya kuambukiza, lakini pia tumeona walio na shida kwenye nywele na kucha,” amesema Dk Mwageni na kuongeza;
“Magonjwa ya ngozi ni kama mengine yasipotibiwa kwa haraka yanaweza kuleta changamoto kubwa katika mwili wa binadamu, wayachukulie kwa uzito na wafike kupata matibabu sahihi kwa wakati na mahali sahihi.”
Ili kuepuka athari na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa zinazoweza kuleta madhara kwenye ngozi, Dk Mwageni ameshauri wananchi kuvaa nguo ndefu zinazofunika sehemu kubwa ya ngozi na kuvaa kofia katika kipindi cha jua kali.
“Jua pia linaweza kusababisha ngozi ipoteze uwezo wa kujikinga, kuzeeka kwa haraka, kuwa dhaifu na kushindwa kudhibiti changamoto kwenye mazingira yetu.”

Baadhi ya wakazi wa jiji la Mwanza waliojitokeza katika kliniki ya uchunguzi, ushauri na matibabu ya magonjwa ya ngozi bila malipo iliyoandaliwa na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando katika kliniki yake ya mjini iliyopo Nera, Mwanza. Picha na Damian Masyenene
“Nashauri kujikinga na jua kali wakati mwingine kuvaa nguzo zinazofunika sehemu kubwa ya ngozi yetu bila kuiacha ngozi ipigwe na jua, kuvaa kofia na kutofanya majukumu yetu kwenye jua kali sana,” amesema Dk Mwageni.
Mkazi wa Kitangiri wilayani Ilemela, Kalelo Maregesi amesema; “Ninapopata jasho muwasho unakuwa mkali ninajikuna unakuwa unasikia tu muwasho ndani ya ngozi lakini vipere havitokei, ninapokaa na watu ninakosa amani na raha kwa sababu ya kujikuna, daktari amesema ni mchafuko wa damu na amenishauri dawa za kutumia.”
Naye, Mimi Masesa, Mkazi wa jijini Mwanza ambaye anasumbuliwa na mzio wa ngozi kwa miaka saba ameipongeza Hospitali ya Bugando, kwa huduma ya vipimo na ushauri bila malipo kwani wananchi wengi wamekuwa wakiishia kwenye maduka ya vipodozi kwa kushindwa kumudu gharama za kuwaona madaktari bingwa.
“Tatizo ni uelewa wa wananchi na kutokuwa na imani kwani wakiambiwa kuna madaktari wanakuwa wazito hawaamini, naomba tukisikia huduma hizi tuchangamke tujitokeze kupata tiba,” amesema Masesa.
Kwa upande wake, Abdul Shija amesema, “kwa miaka miwili sasa ngozi yangu huwa inabanduka sasa wengine wanasema ni fangasi wengine aleji (mzio) lakini nilipoona tangazo la Bugando nikaona nije niwaone wataalamu kwa sababu watu wengi wanapopata maradhi hupuuzia na kutafuta mitishamba.”