Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kumuombea heri Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika maisha yake mapya, kufuatia uamuzi wake wa kutangaza kupumzika rasmi kutoka kwenye majukumu ya kiserikali.
Dkt. Mwigulu alitoa kauli hiyo leo wakati wa Kikao Kazi cha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa AICC, jijini Arusha, kikihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, watendaji wa TRA, na wadau wa sekta ya mapato.
“Tunamuombea heri Mheshimiwa Waziri Mkuu katika maisha yake mapya. Ameitumikia nchi kwa uaminifu mkubwa na nidhamu ya hali ya juu. Tunamtakia baraka na mafanikio katika kila hatua anayochukua baada ya kulitumikia taifa kwa moyo wote,” alisema Dkt. Mwigulu.
Kauli hiyo imekuja siku chache tu baada ya Kassim Majaliwa, ambaye amehudumu kama Waziri Mkuu tangu mwaka 2015, kutangaza kwamba hatagombea tena wala kuendelea kushika wadhifa wowote wa kiserikali baada ya kipindi chake cha sasa kumalizika.