BAADA ya uongozi wa Tanzania Prisons kufanya kikao cha tathimini ya timu hiyo ilichofanya msimu uliomalizika na kipi wakifanye ujao, wameanza mazungumzo ya kuwaongezea mikataba wachezaji wa kikosi chao.
Katibu wa timu hiyo, John Matei amesema kwamba katika kikosi hicho kuna wachezaji ambao mikataba yao imeisha na wanahitaji kuendelea nao, hivyo kabla ya kuanza kusaka sura mpya wanataka kumalizana nao wasije wakawahiwa na timu nyingine.
Kiongozi huyo aliwataja wachezaji hao ni Beno Ngassa (mabao manne), Marko Mhilu, Haruna Chanongo (mabao manne), Samson Mwaituka, Mussa Haji na wale ambao walikuwa hapo kwa mkopo wanaona kuna umuhimu wa kuendelea nao.
“Kuna wachezaji ambao tuliwachukua kwa mkopo kama Adam Adam akitokea Azam alikuwa na mkataba wa miezi sita, sasa yupo huru, Amade Momade raia wa Msumbiji alitoka Singida Black Stars na bado ana mkataba nao, tunataka kuwaomba upya, Kelvin Saboto (Singida Black Stars) na Rabin Sanga (Singida Black Stars) na wao pia wana mkataba na timu hiyo, hivyo tunarudi nao mezani kufanya mazungumzo mapya,” alisema na kuongeza.
“Msimu ujao lazima tujipange na kuhakikisha kikosi kinakuwa cha ushindani ili kukwepa karaha za kucheza mtoano, ndiyo maana kila kitu kinakwenda kwa kuzingatia mahitaji muhimu yanayoendana na ripoti ya kocha,” alisema kiongozi huyo.