Maonesho ya Sabasaba Yatumika Kutoa Elimu ya Sheria kwa Wananchi, Naibu Waziri Sagini Atemblea Banda la Katiba na Sheria

WIZARA ya Katiba na Sheria ambayo ni mshindi wa kwanza wa jumla kati ya wizara zote zilizoshiriki katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam, maarufu kama Sabasaba, yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa.

Kupitia maonesho hayo, wizara hiyo imefanikiwa kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa elimu ya sheria na upatikanaji wa msaada wa kisheria, hatua inayotajwa kusaidia kukuza uelewa wa wananchi kuhusu haki zao za kikatiba na kisheria.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Sagini (Mb), alitembelea banda la wizara hiyo na kupongeza kazi kubwa inayofanywa na wataalamu wa sheria waliopo kwenye banda hilo. Alieleza kuwa mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa na umeonyesha kiu yao ya kupata elimu ya sheria.

 “Wananchi wengi wamefika kupata msaada wa kisheria na elimu kuhusu Katiba. Nawapongeza wataalamu wetu na mawakili waliopo hapa kwa kujitolea kutoa huduma muhimu kwa jamii. Wameonyesha uzalendo wa hali ya juu,” alisema Sagini.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri Sagini alipata nafasi ya kuzungumza na baadhi ya wananchi waliotembelea banda hilo, ambapo wengi wao walieleza kuridhishwa na huduma walizopokea, hususan ushauri wa kisheria bila malipo.

Aidha, Mhe. Sagini alitumia fursa hiyo kupongeza timu nzima ya wizara kwa kuibuka washindi wa kwanza wa jumla katika maonesho hayo, na kusisitiza kuwa ushindi huo ni matokeo ya juhudi, weledi na kujituma kwa watumishi waliowakilisha wizara katika maonesho hayo.

 “Tuzo hii si tu heshima kwa wizara yetu, bali ni kiashiria kuwa wananchi wanathamini huduma zetu. Hili ni jambo la kujivunia,” aliongeza.

Akizungumzia uzoefu walioupata katika utekelezaji wa Kampeni ya Mama Samia Legal Aid, Sagini alisema kuwa kampeni hiyo imekuwa na mafanikio makubwa katika kuwafikia wananchi wengi, hasa wale walioko vijijini na pembezoni mwa huduma rasmi za sheria.

 “Kampeni hii imeonyesha jinsi gani Watanzania wanavyohitaji msaada wa kisheria. Kupitia programu hii, wananchi wamepata fursa ya kuelewa haki zao, namna ya kushughulikia migogoro ya ardhi, ndoa, mirathi na masuala mengine ya kisheria,” alifafanua.

Wizara ya Katiba na Sheria imeendelea kutumia jukwaa la Sabasaba sio tu kama sehemu ya kuonesha huduma zake, bali kama njia ya moja kwa moja ya kuwahudumia wananchi kwa elimu na msaada wa sheria – jambo ambalo limewavutia wananchi wengi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

Related Posts