Wanawake Waliowezeshwa na CAMFRED Wabadilisha Jamii kwa Vitendo

Baadhi ya Wasichana na wanawake waliowezeshwa na shirika la CAMFRED hadi kufikia ujasiliamali.

Picha ya pamoja.

KATIKA jamii nyingi za Kitanzania, wanawake na wasichana wamekuwa wakikumbana na changamoto za kiuchumi, kielimu, na kijamii. Hata hivyo, kupitia uwezeshaji wa shirika la CAMFED, baadhi yao sasa wamekuwa mfano wa kuigwa kwa kuleta mabadiliko chanya si tu katika maisha yao binafsi bali pia kwa jamii inayowazunguka.

Winfrida Kihali kutoka Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro, ni mmoja wa wanawake waliopitia mabadiliko hayo. Anasema CAMFED ilimuwezesha kujiamini, kujitegemea na kufanya biashara kwa mafanikio.

Hayo ameyasema leo Julai 08,2025 Katika Maonesho ya 49 ya Biashara Kimataifa yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Sabasaba) jijini Dar es Salaam.

“Kupitia mafunzo ya ujasiriamali na mikopo isiyo na riba, nimeweza kujitegemea na kusaidia familia yangu. Leo hii nina biashara tatu: nauza pumba na mahindi kwa wafugaji, viungo vya chakula, na pia natengeneza unga wa lishe,” anasema kwa kujiamini.

Mbali na mafanikio yake binafsi, Winfrida amekuwa msaada kwa wengine pia. Ameweza kuwahamasisha wanawake wenzake kuingia kwenye biashara na pia kushiriki katika maonesho ya Sabasaba kupitia ushirikiano kati ya CAMFED na Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TWCC).

“Tulipewa mafunzo kuhusu jinsi ya kupakia bidhaa, namna ya kuwakaribisha wateja, na kuboresha chapa ya bidhaa. Ujuzi huu si wangu peke yangu, nimewashirikisha wenzangu kijijini kwetu,” ameongeza.

Faudhiati Simba kutoka Temeke jijini Dar es Salaam naye ni mfano hai wa msichana aliyewezeshwa na CAMFED na sasa anawasaidia wengine. Baada ya kukumbwa na changamoto ya kifamilia ambayo ilimnyima mahitaji muhimu ya shule, alisaidiwa na shirika hilo kuendelea na sekondari, kujiunga na chuo, na hatimaye kuwa mjasiriamali.

“Nilianza kuoka keki kwa kutumia jiko la mkaa. Sasa ninamiliki bakery yangu ndogo kwa Ziziali na nawasaidia wasichana wengine kujifunza ujuzi wa kuoka na kujiajiri,” anasema kwa fahari.

Kupitia CAMFED, Faudhiati pia amepata fursa ya kuunganishwa na taasisi mbalimbali kwa ajili ya mafunzo na mikopo. Anaamini kuwa msichana mmoja anapowezeshwa, jamii nzima inanufaika.

 “Tunapotolewa mfano, tunawavuta na wengine waamini kuwa wanaweza. Serikali inapaswa kusaidia mashirika kama CAMFED ambayo yanasaidia kundi kubwa la vijana na wanawake kufikia ndoto zao,” amesema.

Jamila Masesa kutoka Tabora anakiri kuwa kuwezeshwa kwake na CAMFED kumemjenga kuwa mjasiriamali na mkulima, lakini pia kiongozi katika jamii yake. Anaamini kuwa familia, hasa wazazi na walezi, wana nafasi ya kipekee ya kulinda na kukuza ndoto za watoto wa kike.

“Msichana akipewa nafasi na kuaminiwa, anaweza kuvuka mipaka ya umasikini na kuwa msaada mkubwa kwa jamii. Wazazi wasione mtoto wa kike kama mzigo bali kama nguzo ya maendeleo,” anasema.

Jamila sasa ni sauti ya matumaini katika jamii yake, akiwahamasisha wasichana kushiriki kwenye afua mbalimbali na kuwaamini kuwa wanaweza kuleta mabadiliko.

Mafanikio ya wanawake hawa si ya kwao binafsi tu, bali ni baraka kwa jamii nzima. Wamegeuka kuwa mfano wa kuigwa, walimu wa vitendo, na washauri kwa wasichana wengine. Uwezeshaji wa wanawake una nguvu ya kuleta mabadiliko endelevu kwa jamii kwa kuongeza kipato, kuimarisha afya ya familia, na kukuza uchumi wa taifa.

Ni wakati sasa kwa serikali, sekta binafsi na mashirika ya kiraia kuendelea kuwekeza kwa wanawake kwa sababu mwanamke aliyewezeshwa ni jamii iliyoimarika.

Related Posts