Sifa kuwa mbunge inavyotikisa, wadau wanataka mabadiliko

Bunge ni chombo cha kutunga sheria katika nchi na ndiyo chombo cha uwakilishi wa wananchi na kuisimamia Serikali katika mambo mbalimbali yanayofanyika na mwisho wa siku, ni kuhakikisha kwamba kila uamuzi unaofanyika unazingatia maslahi mapana ya umma.

Chombo hicho kinahitaji watu wenye kuelewa wajibu wao na kuwa tayari kusimamia maslahi ya umma bila hofu wala kuingiliwa na mihimili mingine. Hilo litasaidia ufanisi wake katika kutekeleza majukumu yake.

Hata hivyo, sifa za ubunge zimekuwa zikimulikwa ambapo wadau tofauti wanapendekeza kwamba Katiba ibadilishwe ili kuweka sifa zinazoendana na mazingira na nyakati za sasa ambapo wanahitajika watu wenye uwezo mkubwa wa kuisaidia nchi.

Hivi karibuni kumekuwa na mjadala mpana kuhusu wananchi wengi kujitokeza kuutaka ubunge kwenye mchakato wa ndani wa kupata wagombea watakaowakilisha vyama vyao kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

Wakati vyama vingine vikiendelea na hatua ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimekamilisha hatua hiyo huku maelfu ya watu wakiwa wamejitokeza kutia nia katika nafasi ya ubunge.

Julai 3, 2025, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla alisema takwimu za haraka waliochukua fomu kwa majimbo Tanzania Bara wako 3,585 na Zanzibar katika majimbo wako 524, jumla katika majimbo tu walioonyesha nia wako 4,109 na majimbo yako 272.

Alisema upande wa uwakilishi Zanzibar waliochukua fomu za kutia nia ni wanachama 503 wakati Umoja wa Wanawake (UWT) wako 623 Tanzania Bara na ndani yake wako 61 wa makundi maalumu lakini Zanzibar wamechukua wanane.

Kwa viti maalumu uwakilishi kule Zanzibar, alisema wako tisa, kwa hiyo jumla ya UWT waliojitokeza ni 640 lakini umoja wa vijana wamechukua 161 na Zanzibar wako saba na Jumuiya ya Wazazi Tanzania Bara wako 55 na Zanzibar pamoja na uwakilishi jumla wapo 575.

Mwitikio huo unajumuisha watu wa makundi tofauti na watu wenye kaliba tofauti wakijiamini kwamba wana uwezo wa kuwa wabunge kulingana na sifa zilizoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hatua hiyo ilikosolewa na aliyekuwa Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe ambaye Julai 3, 2025, akiwa ziarani mkoani Tabora alitaka Bunge lisidogoshwe kwa kuonekana ni chombo ambacho hata machawa na wachekeshaji wanapaswa kwenda kukitumikia.

Zitto alitahadharisha Bunge kudogoshwa kiasi cha kwamba hadi machawa na wachekeshaji wanaona ni mahala pa kwenda.

Msisitizo wa Zitto katika hoja hiyo ni Bunge kupewa hadhi yake, kwa kuwa ni chombo cha kutunga sheria na kinawawakilisha wananchi, lisichukuliwe kuwa chombo ambacho kila mmoja anaweza kufanya anavyotaka.

Ibara ya 67(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inabainisha sifa tatu za mtu kuwa mbunge. Katiba inaeleza kwamba bila ya kuathiri masharti yaliyomo katika ibara hii, mtu yeyote atakuwa na sifa za kustahili kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa mbunge endapo:

“(a) ni raia wa Jamhuri ya Muungano aliyetimiza umri wa miaka ishirini na moja, na ambaye anajua kusoma na kuandika katika Kiswahili au Kiingereza; (b) endapo ni mwanachama na ni mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa; (c) katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya Uchaguzi hakuwahi kutiwa hatiani katika mahakama yoyote kwa kosa lolote la kukwepa kulipa kodi yoyote ya Serikali.”

Hata hivyo, rasimu ya Katiba iliongeza sifa ikipendekeza mtu huyo angalau awe na elimu ya kidato cha nne. Pia, iliongeza sifa nyingine kwamba mtu huyo awe mwadilifu na anayeheshimu haki za binadamu na asiye dharau au kubagua kwa misingi ya kabila, dini au jinsi.

Licha ya Katiba kuainisha sifa hizo, wadau tofauti waliozungumza na Mwananchi wameeleza kwamba kuna haja ya kubadilisha kifungu hicho ili kuongeza sifa zitakazochuja wabunge ili Taifa lipate watu wenye uwezo wa kuchanganua mambo.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk George Kahangwa anasema mbunge sharti awe mtu mwenye angalau shahada ya pili na hao wanaojua kusoma na kuandika wapangiwe kazi nyingine.

“Maoni yangu kulingana na mazingira ya nchi yetu tunapaswa kuwa na mbunge mwenye sifa angalau awe mtu mwenye shahada ya pili na hao wanaojua kusoma na kuandika wapangiwe kazi nyingine,” anasema.

Anasema Tanzania inastahili kupata wabunge waliokuwa bora katika uchanganuzi wa mambo kwa weledi wa hali ya juu na uzalendo ndani yake na awe anayeweza kuisimamia serikali.

“Tuwe na mbunge makini ambaye hata tukija kutunga sheria bila kujali yale yanayoletwa na serikali kama mapendekezo au mswada ili tupate sheria nzuri hata bajeti zipitiwe na watu wenye ufikiri mzuri,” anasema Dk Kahangwa.

Kwa mujibu wa Dk Kahangwa, awe mbunge ambaye hata akienda jimboni anawatumikia wananchi akiwa na mipango dhabiti yenye kulipeleka Taifa mbele kuliko kuwa na wabunge ili mradi.

“Watu wenye sifa za namna hiyo ni jukumu la vyama vya siasa vinavyosimamia wagombea kuhakikisha wanatuletea watu wa namna hiyo, kwa sababu vyenyewe vina dhamana ya kuchuja wagombea,” anasema.

Dk Kahangwa anasema ubunge ni moja ya kazi zinazolipa vizuri katika nchi na kazi wanazotakiwa kufanya zinatarajiwa kuwa kubwa zenye maslahi mapana ya wananchi wote lakini inakuwa tofauti.

“Tunachukua raslimali za nchi tunawalipa hawa ambao wanatakiwa kuwa wataalamu wa mambo, hatuwezi kuwa na watu wanaoenda kuongea utani na kusema wanaunga mkono hoja,” anasema

Anasema wakati mwingine mtu anamaliza miaka mitano alijenga hoja siku moja pekee halafu mwisho wa siku analipwa kwa viwango vya juu huku kuna baadhi ya wafanyakazi kama walimu wanalipwa fedha kidogo.

“Tunahitaji kupata watu wenye upeo wa kusimamia mikataba mikubwa ya kisheria iliyoandikwa na wataalamu waliobobea, tunatatizo, tunasaini mikataba na kampuni kubwa zenye wanasheria wabobevu,”anasema.

Dk Kahangwa anasema kigezo cha kujua kusoma na kuandika kiliifaa Tanzania wakati ule ambao nchi haikuwa na wasomi wengi na haikuwa na namna na ilikuwa vigumu kupeleka yeyote tu.

“Wakati ule wa uhuru kiliwekwa kigezo kile angalau mtu ajue kusoma na kuandika, mazingira ya wakati ule na sasa ni tofauti, Watanzania wenye elimu ya juu wako wengi waliomaliza kidato cha nne ni wengi huwezi kusema wanajua kusoma na kundika,” anasema.

Ataka elimu kidato cha nne

Kwa upande wake, Hamduni Maliseli, mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii, anasema hata mtu aliyehitimu kidato cha nne anastahili kuingia kwenye chombo hicho ingawa bado inahitajika mjadala mpana wa kitaifa.

“Bunge, madiwani ni maeneo muhimu zaidi, kujua kusoma na kuandika hakuwezi kuwa kigezo kinachotosheleza kuwa mwakilishi wa wananchi lazima twende zaidi,” anasema mchambuzi huyo.

Anasema wakati kusoma madarasa mengi kuna kusaidia kujua mambo, kusoma Kiingereza na Kiswahili na ukafafanua mambo makubwa kwa kufuatilia kwenye vyombo vikubwa.

“Unakuwa na upana wa kuchanganua mambo kutokana na elimu uliyoipata darasa la saba halitoshi au kusoma na kuandika hakutoshi kukufanya uwe na uwanja mpanga wa uchanganuzi wa mambo,” anasema.

Anasema mbunge lazima awe na uwezo mwingine zaidi na wanaozungumza kuongeza vigezo wako sahihi kulingana na ulimwengu wanaouendea.

“Lakini kuna wabunge ambao hawana elimu kubwa hata za kidato cha nne lakini michango yao ni mizuri na yenye tija na wanatoa mifano kuwashinda waliosoma nalo pia linahitaji mjadala,” anasema.

“Hata elimu ya kidato cha nne inatosha kwa sababu mikataba hii inakuja bungeni baada ya kupitiwa na majopo ya wataalamu wa wizara,” anasema Maliseli.

Mchambuzi mwingine, Profesa Ambrose Kessy anasema kuwa kiongozi kunahitaji zaidi ya kujua kusoma na kuandika kwa sababu ukishika wadhifa huo unatakiwa kuonyesha njia ili wengine wafuate.

“Sasa kama unajua kuandika na kusoma usiweze kuendesha gurudumu tafsiri yake wanaokufuata watapotea, ni muhimu tuangalie vyote ingawa tumeweka kikatiba walao tujue kusoma na kuandika,”anasema

Profesa Kessy anasema ni muhimu kuwepo na nafasi ya wananchi wenyewe kuangalia kujua kama kweli anajua kuandika na kusoma anauwezo wa kwenda kutatua matatizo yao.

“Je ni mtu anayeweza kusikiliza watu ,anaweza kuchambua kinachoendelea ni kweli ni mtu ambaye ana maono ya muda mrefu na muda mfupi ya kutatua matatizo yao,”anasema

Anasema kuna sifa nyingi ambazo zinahitaji ili mtu awe kiongozi mzuri “Ingawa kila mtu anaweza kuwa kiongozi lakini si kila mtu anaweza kuongoza,”anasema

Anasema unaweza ukawa kiongozi na umekaa kwenye nafasi lakini si kuongoza ile nafasi huku akisema dunia ya sasa unaongoza watu ambao wanajielewa.

“Watu wameelimika wanajua mambo yanavyoenda ni vuzuri kuangali vyote lakini kusoma na kuandika ni jambo la kikatiba, isipokuwa ni jukumu la wananchi wenyewe kuamua kupitia uchaguzi ni kiongozi wanayemtaka kwa muda waliopo nao,”anasema Profesa Kessy.

Kwa upande wake, Mwanazuoni wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Matrona Kabyemela, anatofautiana wengine katika suala la kuongeza vigezo kwa kile anachodai kila mtu ni mwanasiasa, awe amesoma au hajasoma.

“Sidhani tunaitaji kuongeza kigezo cha elimu kwa wana siasa,kwa maana siasa maana yake ni wananchi wanapokutana na kushiriki kufanya uamuzi unaohusu maisha yao na kukubaliana namna bora ya kuendesha maisha yao katika eneo lao,” anasema Dk Matrona nakuongeza

“Hii ina maana kila mtu ni mwanasiasa na awe amesoma au la anajua changamoto na fursa zilizo kwenye eneo lake, sasa ili kutengeneza sera na mikakati mizuri ndo tunaitaji wasomi ili waweze kuziandaa na kuzitekeleza,” anasema.

Kulingana na Dk Matrona anasema “ndo maana tuna executive ambayo ina professionals who implement what has been dicided in the parliament,”

“Sasa tukisema vigezo viongezwe tutakuwa tunawatenga wananchi wengi wenye maarifa ya maeneo yao, mimi naona vigezo vibaki vile vile lla nguvu iongezwe kwenye maadili ya viongozi,”anasema

Anasema uongozi uwe kama utumishi au dini kama ilivyokuwa enzi za Mwalimu Julis Nyerere huku akiongeza shida za uongozi hazitaondolewa kwa kuongeza vigezo vya elimu “vigezo vibane kwenye maadili basi.”

Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi anasema watu wengi wanakimbilia bungeni kutaka kuridhisha riziki zao na matumbo yao.

“Raia anaongezewa kikokotoo, mbunge anaongezewa posho na mashahara, alafu anaridhika ndiyo maana Profesa anakimbia chuo kikuu hata kufundisha, mwalimu anakimbia, daktari naye anakimbia hata majambazi nayo yanakimbia kila mmoja una mkuta bungeni,” anasema.

Anasema bungeni kuna kuwa na mkusanyiko wa watu mbalimbali ambao hawana majukumu ya kuiwajibisha serikali ni muhimu kubadilisha sheria badala ya kufurahia ibaki kama ilivyo.

“Maisha yetu ni yakuunga unga mtu anatumia zaidi ya Sh40 hadi Sh50 milioni unakuja kwenye kituo ni mtu wa kwanza unaambia matokeo yameshahesabiwa na umeshindwa,” anasema Mwabukusi.

Related Posts