Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linamshikilia Isaya Kastam, mkulima na mkazi wa Kwa Mfipa, kwa tuhuma za mauaji ya aliyekuwa mpenzi wake, Faraja Lumanus Chafu (35), mkazi wa eneo hilo.
Tukio hilo limetokea mnamo Julai 7, 2025, majira ya saa 3:45 usiku, katika Mtaa wa Simbani, Kwa Mfipa, wilayani Kibaha, ambapo inadaiwa mtuhumiwa alimsababishia majeraha makubwa Faraja kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali katika maeneo mbalimbali ya mwili wake, kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni wivu wa kimapenzi.
Faraja alifariki dunia akiwa njiani kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Tumbi kwa ajili ya matibabu.
Baada ya tukio hilo, mtuhumiwa alitoroka na kufanikiwa kukamatwa na Polisi katika eneo la Kigamboni, Dar es Salaam, ambapo alikutwa akiwa amejaribu kunywa kitu kinachodhaniwa kuwa ni sumu kwa nia ya kujiua. Hivi sasa anaendelea kupatiwa matibabu, na mara baada ya kupona, atachukuliwa hatua za kisheria.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limeeleza kuwa uchunguzi wa daktari kwa mwili wa marehemu unaendelea katika Hospitali ya Rufaa ya Tumbi.
Aidha, Jeshi hilo limetoa onyo kali kwa wananchi wanaojihusisha na vitendo vya kujichukulia sheria mkononi, likiwataka kufuata taratibu za kisheria kwa kuripoti migogoro kwenye uongozi wa kijiji au vituo vya Polisi ili hatua stahiki zichukuliwe kwa wakati.