UCHAGUZI MKUU 2025: Dk Biteko asema tuvumiliane, tuheshimiane

Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati nchini Tanzania, Dk Doto Biteko amewataka waandishi wa habari kuhimiza uvumilivu wa kisiasa na utamaduni wa watu kuheshimu maoni na mtazamo wa wengine:”Hata kama hukubaliani nayo, lakini kuna dogo la maana la kuchukua.”

Amesema uchaguzi ni tukio la kupita lakini Tanzania itabaki hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha anailinda kwani ikivurugika kuirejesha ni kazi kubwa.

Naibu Waziri Mkuu,Dotto Biteko akizungumza kabla ya kufungua mkutano wa wadau kujadili mchango wa sekta mbarimbari katika kufanikisha uchaguzi mkuu 2025.



Dk Biteko ameyasema hayo leo Jumatano, Julai 9, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa wadau wa kujadili mchango wa sekta ya habari katika kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Miongoni mwa wadau ni viongozi wa dini, wanahabari, wahariri na Makamanda wa Polisi wa Mikoa (RPC) yote nchini, wakuu wa vikosi vya Polisi wakiongozwa na Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, David Misime ambaye atatoa mada isemayo ‘Wajibu wa waandishi wa habari na Jeshi la Polisi katika kulinda usalama wakati wa uchaguzi’.

Dk Biteko amesema mtu yeyote anayeweza kudhani unaweza kufanya kazi bila vyombo vya habari anajidanganya:”Muhimu hapa tusivilaumu vyombo vya habari bali tuvipe taarifa rasmi ili vihabarishe jamii.”

Akijenga hoja kuelekea uchaguzi huo, Dk Biteko amesema:”Tuhimize maelewano, uvumilivu wa kisiasa na utamaduni wa kuheshimu maoni, mtu kuheshimu mtazamo wa mtu mwingine.”

Ametolea mfano, anayeamini Yanga ni timu bora, aheshimiwe sawa na yule anayesema Simba ni timu bora.

“Hata kama mtu anasema jambo hulipendi, msikilize kwani kuna jambo dogo zuri lichukue,” amesema Dk Biteko.


Kwa vyombo vya habari, Dk Biteko ameaema:”Mnapaswa kuwa zaidi ya vyombo vya habari. Walinzi wa kweli, wajenzi wa amani na wachochezi muwabaini na kuwawajibisha ninyi kwa ninyi.”

Aidha, Dk Biteko amesema Serikali itahakikisha vyombo vya habari na waandishi wa habari wanakwenda na kurudi nyumbani wakiwa salama. Anayetoka na kamera yake irudi ikiwa salama, sawa na anayetoka nyumbani akiwa na kalamu yake arejee salama pasipo kupotea.

“Tutahakikisha kunakuwa na mazingira huru na haki na Jeshi la Polisi linawalinda ili mtekeleze wajibu wenu ipasavyo,” amesema Dk Biteko huku akipongezwa kwa makamanda wa polisi kushirikishwa kwenye majadiliano hayo.

“Nimefurahi sana mmewaleta makamanda wa polisi ili tujadili kwa pamoja ili tukiingia kwenye uchaguzi tutoke salama na tusukume ajenda ya uchaguzi ili tuingie na tutoke salama,” amesema Dk Biteko.

Naibu Waziri Mkuu huyo amewataka waandishi wa habari kutumia lugha za staha, mripoti kwa usawa, akitokea mtu akampongeza aheshimiwe kwa maoni yake, akitokea mtu akamponda basi aheshimiwe yaani tuheshimiane.

Awali, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi amesema leo ni siku ya kipekee kwa wadau mbalimbali wa habari wanapokutana kujadiliana namna bora ya kwenda kwenye uchaguzi mkuu.

Amesema mwelekeo wa Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeboresha vyema mazingira ya vyombo vya habari kutekeleza wajibu wake ipasavyo.

“Vyombo vya habari vina umuhimu mkubwa sana kwenye maendeleo ya nchi. Ndio maana tumekutana hapa ili tujadiliana namna bora ya kwenda na kutoka salama katika uchaguzi huu ili tutoke tukiwa wamoja wakati, kabla na baada ya uchaguzi,” amesema Profesa Kabudi.

Amesema hadi sasa, usajili wa waandishi katika mfumo wa kidijiti ambao umezindukiwa rasmi leo na Dk Biteko umefanikiwa kusajili waandishi 2,900 akiwemo yeye mwenyewe Profesa Kabudi ambaye amepata ‘Press Card’ mpya. Waziri huyo kitaalamu ni mwandishi wa habari.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema mada mbalimbali zitawasilishwa kwenye majadiliano hayo.

Miongoni mwa mada hizo zitatolewa na matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii na teknolojia ya Akili Unde (AI), wajibu wa waandishi wa habari katika kuzingatia maadili na sheria za huduma za habari na kuripoti migogoro na maafa kipindi cha uchaguzi mkuu.

Endelea kufuatilia Mwananchi

Related Posts