Babati. Mwanasiasa mkongwe nchini, Mateo Qares, ambaye amewahi kuwa mbunge wa Babati mkoani Manyara na waziri katika wizara mbalimbali nchini, amefariki dunia jana Julai 9, 2025.
Akizungumzia kifo hicho leo Julai 10, 2025 msemaji wa Umoja wa wanaManyara (Norivada), Mikael Aweda amesema Qares alifariki dunia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es salaam jana.
Aweda ameeleza kuwa msiba upo nyumbani kwa marehemu maeneo ya Salasala, jijini Dar es salaam na misa ya kumuaga imefanyika hapohapo mchana wa leo.
Amesema baada ya misa hiyo, mwili wa marehemu utasafirishwa kwenda Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es salaam, tayari kwa safari ya kuelekea Babati kupitia Uwanja wa Ndege wa Arusha.
Ameeleza kwamba mazishi yake Qares yatafanyika Jumamosi Julai 12, 2025 nyumbani kwake katika eneo la Nakwa kata ya Bagara, mjini Babati.
“Kwa niaba ya wanaNorivada wote, ninatoa pole nyingi kwa wenzetu Anthony Qares na mama yake mzazi, pamoja na ndugu, jamaa na marafiki wote waliofikwa na msiba huu,” amesema Aweda.
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amefika nyumbani kwa marehemu Qares, maeneo ya Nakwa, kata ya Bagara mjini Babati.
Sumaye ametoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa eneo hilo na na kuwafariji waombolezaji.
Naye mbunge mstaafu wa Babati Vijijini, Vrajilal Jituson ametoa pole kwa wakazi wote wa Babati walioguswa na msiba huo.
Mkazi wa eneo la Nakwa, James Clet amesema marehemu Qares atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika uongozi kwa nafasi alizoshika.
Clet ameeleza kwamba eneo la Nakwa halijabahatika tena kupata kiongozi mwingine mkubwa zaidi ya Qares ambaye alikuwa mbunge, waziri na mkuu wa mkoa.
Marehemu Qares atakumbukwa kwa msimamo wake mkali kwani kitu au jambo akiliamini huwa anabaki kwenye msimamo wake huohuo bila kubadilika wala kuogopa chochote.