UCHAMBUZI WA MJEMA: Profesa Kitila, umezunguka sana lakini jawabu ni Katiba mpya

Jumanne ya Julai 8, 2025 nilipata bahati ya kufuatilia mkutano wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), akielezea mchakato mzima wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Kuna hoja iliyoibuliwa na mwandishi mkongwe, mzee Salim Said Salim kuhusu kuwa na bunge imara, ambayo ninathubutu kusema, waziri alizunguka sana bila kutoa majawabu ya hoja ile na ukweli jawabu lilipaswa kuwa Katiba mpya.

Huwa naisoma Rasimu ya Pili ya Katiba ya Jaji Warioba na wenzake, nairudia na kuirudia kuhusu eneo linalohusu sifa za kuwa mbunge na nguvu ya wapiga kura kumwajibisha mbunge hata kabla ya miaka mitano, sielewi kwanini tulifuta.

Kwanini nasema hivyo? Ni kwa sababu kama tungekuwa na Katiba Bora inayowawajibisha wabunge wanaokwenda bungeni kuwasilisha mawazo yao na ya wake zao na sio ya wapiga kura, basi wapiga kura wangeweza kuwafuta kazi.

Badala yake, wapiga kura wanabaki na tai shingoni hadi kipindi cha miaka mitano kimalizike, hata kama mbunge wao anaongea pumba bungeni, haonekani jimboni hata zaidi ya mwaka, hapatikani kwenye simu wala hachangii ipasavyo bungeni.

Dira ya Taifa inayoitwa ‘Dira 2050’ inakwenda kuzinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Alhamisi ya Julai 17, 2025 Jijini Dodoma, imepitia hatua 12 zinazotakiwa huku ikiwa ni Dira ya pili ya Taia ambayo haina uelekeo wa Kiitikadi ya chama.

Pamoja na taarifa nzuri ya waziri iliyotokana na kazi nzuri iliyofanywa na timu iliyoshughulikia ‘Dira 2050’, binafsi sikuridhishwa na maelezo ya waziri wakati akijibu mchango wa mwandishi mkongwe nchini, mzee Salim Said Salim.

Katikati ya mjadala uliohusu umuhimu wa kuwa na Bunge imara ambalo litawashawishi wananchi kuwa wanawakilishwa ipasavyo, mzee Salim alionyesha kusikitishwa na kauli ya waziri na hapa ninamnukuu ili upate muktadha wake.

“Mheshimiwa waziri, nasikitika, tena sana. Umesema wananchi wakiwa na masuala yao ya kuiwajibisha serikali, basi wapitie kwa wabunge. Utaona anasema (mbunge) kwa niaba ya wananchi wangu naunga mkono mia kwa mia”

“Lakini ukifanya utafiti, kwamba bill (muswada) ile imepelekwa hajafanya kikao hata kimoja cha jimbo lake.  Inakuwa yale ni maoni yake,”alisema na kuongeza;-

“Aende na orodha ya vikao alivyofanya, wapi  na tarehe  ngapi ili tuone umma wa watanzania kweli unawakilishwa na wabunge. Kwa sababu kinachofanyika bungeni ni mawazo ya mtu, mke wake na rafiki yake. Hawafanyi vikao (na wananchi)”.

Akijibu hoja ya mwandishi huyo Guru (Nguli) katika tasnia ya Habari, Profesa Mkumbo alisema moja ya eneo la kuwasikiliza ni waandishi wa Habari lakini wabunge huwezi kuwapuuza kwa kuwa ndio wawakilishi wa wananchi.

“Iwe kama wanafanya mikutano au hawafanyi hicho ni kitu kingine. Lakini mbunge anawakilisha wananchi wake, jimbo lake, chama chake na anawakilisha nchi yake na anajiwakilisha mwenyewe,”alieleza Profesa Mkumbo katika majibu yake.

“Kwa hiyo haya mambo ya mbunge, hilo sasa ndio tunakwenda kwenye uchaguzi, napenda niwahakikishie kwamba sisi wabunge ambao bunge limeisha juzi , tulibeba maoni ya wananchi tukayapeleka  kwa serikali na Serikali iliyasikiliza”

“Mengi yamefanyiwa kazi ndio maana tumepiga hatua kubwa ya maendeleo. Kwa hiyo sisi kama wabunge tunajivunia sana kazi tuliyofanya na tutaendelea kufanya hivyo”alisisitiza na kusema hata hivyo wamepokea ushauri wa mzee Salim.

Nimejaribu kuandika kwa kirefu utangulizi wa nini kilitokea ili kukupa picha ya nini ilikuwa hoja ya mzee Salimu na yapi yalikuwa majibu ya waziri, lakini kwa vyovyote vile iwavyo au itakavyokuwa, hoja ya mzee Salim inawakilisha maoni ya wengi.

Wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilipokuwa ikizunguka kukusanya maoni, moja ya hoja iliyokutana nayo ni hiyo aliyoisema mzee Salim, kwamba wapo wabunge wanaingia bungeni na kutoa mawazo yao wakiyaita ni ya wapiga kura wao.

Kwa hiyo, wananchi wengi walitaka kuwapo kwa kipengele katika Katiba mpya, kitakachowapa wananchi haki na mamlaka ya kuwawajibisha wabunge wao, Tume ya Mabadiliko ikawasikiliza lakini bahati mbaya sana, mchakato uliishia njiani.

Kuna utofauti mkubwa kati ya jibu na jawabu kwani jawabu ni uponyaji wa jumla wakati jibu ni kama kituliza maumivu kwa hiyo alichokisema Profesa Kitila Mkumbo kwangu mimi nakichukulia ni jibu, lakini jawabu ni Katiba mpya.

Nataka nimwambie Profesa Kitila Mkumbo kuwa akitaka kufahamu namna wananchi hawajaridhishwa na utendaji wa bunge la 12 katika kuwasemea wananchi wa kawaida, afungue kura ya maoni tu mtandaoni aone majibu.

Nakipongeza Chama cha Mapinduzi (CCM) kwamba katika ilani yake ya uchaguzi mkuu (2025-2030), chama kitaielekeza Serikali kuimarisha demokrasia na utawala bora kwa kuhuisha na kukamilisha mcahakato wa Katiba mpya uliokwama 2014.

Sina hakika kama katika kufufua mchakato huu, serikali itaenda na Rasimu ya Jaji Warioba niliyoitaja, lakini rasimu hiyo ilikuwa na ibara 125(2)(a) ambayo iliweka ukomo wa ubunge kuwa ni vipindi vitatu vya miaka mitano mitano na si zaidi.

Lakini ilikuwa na ibara ya 129(1) ambayo iliwapa wapiga kura haki ya kumuondoa bunge wao madarakani endapo ataunga mkono sera ambazo zinaenda kinyume na maslahi ya wapiga kura au kinyume na maslahi ya Taifa.

Si hivyo tu, ibara hiyo iliwapa wapiga kura haki ya kumuondoa madarakani mbunge wao endapo atashindwa kuwasilisha au kutetea kwa dhati hoja zinazotokana na kero za wapiga kura wake au pia kuacha kuishi jimboni.

Tungekuwa na Ibara hizo katika Katiba yetu ya sasa ya mwaka 1977, haya anayoyasema mzee Salim pengine tusingeyaona bungeni kwa sababu wabunge wetu wangekuwa na adabu kwa wapiga kura kwamba ukiwakosea ni nje.

Naamini, kama tungekuwa na ibara hiyo na namna watanzania hawakuridhishwa na namna bunge la 12 lilivyoshughulikia suala la utekaji, kupotea kwa watu na mauaji ya raia, nina uhakika wabunge wengi wasingefika uchaguzi mkuu 2025.

Kuna mambo ambayo tukiwauliza leo wabunge waliomaliza muda wao kama walishughulikiaje tatizo la ajira kwa vijana, matumizi makubwa ya Serikali, kupanda kwa gharama za maisha na ukiukwaji wa haki hawatakuwa na majibu.

Juni 26,2025 nilimsikiliza Spika wetu wa Bunge la 12, Dk Ackson, litakalovunjwa Agosti 3 na Rais Samia Suluhu Hassan,akisema katika uhai wa bunge hili, maswali ya msingi 5,057 na ya nyongeza 15,000 yaliulizwa na wabunge wetu.

Mbali na maswali hayo, lakini maswali ya papo hapo kwa waziri mkuu,Kassim Majaliwa ambayo huulizwa kila siku ya Alhamisi yalikuwa 260 hivyo ukijumlisha maswali yale ya msingi, ya nyongeza na ya waziri mkuu unapata maswali 20,317.

Tuwaulize wabunge wetu, ni maswali mangapi kuhusu matukio ya utekaji, kupotea kwa watu na mauaji, yaliulizwa katika bunge hilo. Je hawaguswi nayo? Wanafurahishwa na ugumu wa maisha walionao watanzania?

Lakini tumeshuhudia baadhi ya wabunge wakifanya mizaha bungeni, wakijibu maswali kwa niaba ya Serikali ili kudhalilisha tu upinzani, tumeshuhudia michango isiyo na tija hadi mtu unatamani uingie chini ya uvungu wa kitanda usione.

Kwa hiyo majawabu ya hoja ya mzee Salimu sio hayo ambayo Profesa Kitila Mkumbo aliyatoa, bali ni kuwa na Katiba mpya itakayowapa wapiga kura mamlaka na haki ya kumwajibisha mbunge anayekwenda bungeni na kujiwakilisha binafsi.

Mbunge analipa mshahara, posho na marupurupu kibao kwa kutumia fedha za walipa kodi masikini, hivyo tunataka Katiba mpya itakayowafanya wabunge kwanza wawaheshimu wapiga kura na pili walifanye bunge letu liwe imara.

Tunahitaji Bunge ambalo kweli litaisimamia na kuishauri Serikali kwa mujibu wa Ibara ya 63 ya Katiba, na tunahitaji bunge ambalo mbunge akiingia katika mlango wa Bunge, anaacha uanachama wa chama chake na anaingia kama mbunge.

Lakini kubwa zaidi, tunataka mbunge akisimama bungeni kuwasilisha hoja za wapiga kura wake, awe kweli alikutana na wananchi wake siku kadhaa kabla ya bunge na kumtuma hicho anachokisema, sio alizojadiliana na mkewe au marafiki.

Ukweli hatuhitaji baadhi ya wabunge tuliowaona Bunge la 12, hawakusimama kabisa upande wa wananchi hata pale walipokuwa wakitoa machozi ya damu katika suala la watu kutekwa, kupotea na wengine kuuawa. Huo ndio ukweli.

Tunawahitaji wabunge wa aina ya Zitto Kabwe ambaye aliwahi kutafuta saini zaidi ya 70 ili kumpigia kura ya kutokuwa na imani, waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushindwa kuwawajibisha mafisadi Serikalini.

Tunataka wabunge ambao watakwenda bungeni kupigania kupelekwa kwa muswada wa kulisuka upya Jeshi la Polisi na Taasisi nyingine za Haki Jinai, tunataka mbunge atakayepigania uwepo wa sheria bora na maisha bora kwa mtanzania.

Kwa hiyo, Profesa Kitila Mkumbo ulizunguka sana katika kujibu hoja ya mzee wetu Salim, lakini jawabu lake ni kuwa na Katiba bora kama ile ya Jaji Warioba ambayo itawafanya wabunge wasione bunge ni kijiwe kwa ajili ya maslahi binafsi.

Related Posts