Afrika yaonyeshwa njia ya kukuza uchumi wake

Capetown. Mataifa ya Afrika yametakiwa kubadili mtazamo wa kutegemea kusaidiwa na mataifa yaliyoendelea na badala yake, yajikite katika kukuza ujasiriamali kwa kuwa na mikakati thabiti na sera zinazovutia ukuaji wa biashara ili kukuza uchumi wake.

Pengine kwa rasilimali za asili Afrika inaongoza lakini bara hilo la pili kwa idadi ya watu duniani, siyo miongoni hata mwa mabara matatu kwa utajiri duniani.

Wachambuzi wa mambo wanadai kuwa kinachokosekana ni mikakati mizuri na usimamizi thabiti.

Akizungumza leo Julai 10,2025  Capetown nchini Afrika Kusini katika kongamano la biashara lililoandaliwa na Benki ya Standard Group, Makamu wa Rais wa Botswana, Ndaba Gaolathe anasema ili kubadilisha hali iliyopo ni lazima mataifa ya Afrika yabadili mtazamo wake na kukumbatia zaidi ujasiriamali.

Kiongozi huyo ambaye alikuwa mgeni rasmi katika siku ya kwanza ya kongamano hilo lililokutanisha magwiji wa biashara barani Afrika, amesema bara hilo lina hazina kubwa ya fursa ambazo hazijachangamkiwa, hivyo kinachotakiwa ni mabadiliko ya kubadili hali.

“Makadirio yanaonyesha ifikapo mwaka 2050 idadi ya watu Afrika itakuwa bilioni 2.5 na hivi sasa kati ya watu zaidi ya bilioni 1.5 waliopo, asilimia 60 ni vijana tena sio vijana tu, bali wenye uwezo uthabiti lakini kiwango cha mitaji binafsi kinachovutiwa barani Afrika ni asilimia moja ya kiwango chote cha ulimwengu. Tunapaswa kubadili hili,” amesema.

Gaolathe amesema Bara la Afrika halihitaji kusaidiwa bali linahitaji miundombinu, mitaji na utekelezaji wa mipango endelevu.

“Tufikirie fursa zilizopo, Bara la Afrika kwa ukubwa wake, tusiwaze mabilioni tuwaze matrilioni na sekta binafsi ina nafasi ya kutufikisha kwenya mafanikio hayo,” amesema.

Miongoni mwa wafanyabiashara waliohudhuria kongamano hilo ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Ona Safari, Julias Mkondo ambaye anasema kongamano hilo ni jukwaa muhimu kwake kupata uzoefu wa namna wenzake katika Bara la Afrika wanaendesha na kusimamia biashara.

“Changamoto kubwa kwa tuliowengi (wajasiriamali) ni mitaji. Tukiweza kupata mitaji kwa urahisi tutakuza biashara zetu na kutimiza malengo ya kuongeza mchango wa sekta tuliyopo,” amesema Mkondo ambaye kampuni yake inahusika na huduma za utalii nchini Tanzania.

Mkuu wa Idara ya Biashara wa Benki ya Stanbic Tanzania ambayo ni benki tanzu ya Benki ya Standard Group, Charles Mishetto amesema kwa Tanzania kinachofanya kwa benki hiyo ni kurasimisha shughuli za ujasiriamali ili iwe rahisi kuzipatia mitaji.

“Benki nyingi zinakopesha kwa kuangalia dhamana, kwetu sisi dhamana ni miamala yako, lakini lazima tukuwezeshe kuwa rasmi ili kukidhi mahitaji ya kibenki,” amesema Mishetto huku akisisitiza kuwa wanafanya urasimishaji kupitia kampeni zao mbalimbali.

Related Posts