Unguja. Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salumu Mwalimu amesema namna pekee ya kukiondoa Chama cha Mapinduzi (CCM) madarakani siyo kusubiria mabadiliko ya mifumo ya sheria, badala yake ni kupambana nao katika uwanja wa siasa.
Mwalim ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Julai 10, 2025 katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Madukani Daraja Bovu, ikiwa ni awamu ya pili ya operesheni ya chama hicho ya C4C.
“Usitegemee kwamba kuna siku mtu atakulegezea kamba kukuandalia mazingira mazuri ya kupambana naye kwa wepesi, hilo sahau,” amesema na kuongeza.
“Tukisubiri CCM wakututungie sheria za kuwaondoa madarakani kwa wepesi tutachelewa sana na hilo haliwezi kutokea kwahiyo ndio maana tukasema twende Kupambana nao kwa kutumia nguvu ya Umma na siyo wao kutuonea huruma,” amesema.
Kwa mujibu wa Mwalimu, huo ndio ulikuwa msimamo wake tangu alipoamua kuachana na vitu vyote kuingia kwenye siasa lakini aliamua kuondoka kwenye chama chake cha zamani baada ya kuona wamebadili mfumo na kutaka kususia uchaguzi kisa kuogopa mifumo ya uchaguzi.
Amesema nia ya kukiondoa chama hicho kwenye utawala sera zake zimeshindwa kuleta mabadiliko kwa wananchi na umasikini kwa Wazanzibari unazidi kuongezeka.
“Tunapaswa twende nao mguu kwa mguu ipo siku watang’oka na sisi Chaumma tunakwenda kuwaondoa madarakani,” amesema.
Amesema katika utawala wa miaka mitano ya Serikali ya awamu ya nane hakuna ubishi kwamba imejenga miradi lakini umasikini unaendelea kutawala miongoni mwa Wazanzibari hivyo chama hicho kikipata madaraka kitashughulika na maisha ya watu kuonda umasikini huo.
Amesema Zanzibar ilikuwa ikizalisha tani 20,000 za karafuu kwa mwaka lakini kwasasa inazalisha tani tisa, hivyo badala ya kuongezeka angalau kufikia uzalishaji wa tani 50,000 ila zinapungua.
“Hizi karafuu Mungu hakuzileta Zanzibar kwa Bahati mbaya bali alikuwa na makusudi yake kuwaondolea wananchi wake umasikini lakini mifumo na mipango ya utawala imefeli,” amesema.
Amesema kama kuna dhambi kubwa itafanywa “Ni kuogopa uchaguzi Mkuu eti tutaibiwa na hili ndio njia oekee ya kuingia CCM.”
Amesema Chaumma hakina dhamira ya kubomoa misingi ya harakati za mabadiliko Zanzibar badala yake wanatakakuongeza nguvu katika maeneo ambayo wanaona kuna watu wanaweza kufanya.
Mwenyekiti wa Chaumma, Hashimu Rungwe amesema chama hicho kina mpango wa kuleta mabadiliko kwahiyo ikifika Oktoba mwaka huu wakichague chama hicho.
“Mimi ninataka niwaambie jambo moja, ikifika Oktoba kichague Chaumma ili mpate sera za ubwabwa,” amesema.
Naibu Katibu Mkuu wa Chaumma Zanzibar, Mohamed Masoud amesema CCM wametawala zaidi ya miaka 61 lakini wameshindwa kuwaondolea wananchi umasikini.
“Chama cha Umma kimekuja hapa siyo kuangalia majengo ila ni kuangalia afya ya mtu, apate elimu, maisha bora na isiwe mtu anayenufaika awe na kadi ya chama fulani,” amesema.
Amesema wanataka afya ziwe imara, ajira ziongezeke na hawataki kuona hospitali linakuwa jengo la utalii bali liwe jengo la kutoa huduma za afya kwa ukamilifu
Makamu Mwenyekiti Chaumma Zanzibar, Issa Abbas Hussein amesema nchi inadidimia hivyo wananchi wajiunge na Chaumma wasaidiane katika kusukuma mbele gurudumu la mendeleo.
“Tunakuombeni mjiunge na wananchi tuondoe hali ya ukandamizaji, tupate Maendeleo, huu ndio mwaka wa mabadiliko na hayawezi kuja kwenye sahani, bali ni kupambana njoo msidharau wala kupuuza hii Chaumma ya leo siyo ya jana,” amesema.
Mwenyekiti wa Vijana Taifa, Masoud Mambo amesema vijana wana nafasi kubwa kupambania haki hivyo wanapaswa kuwa mstari wa mbele kupigania haki zao na za taifa lao.