Kinyerezi III sasa kuingiza megawati 1,000 gridi ya Taifa

Dar es Salaam. Kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya umeme kila siku, Serikali imetangaza kuanza kutekeleza mpango wa ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme wa gesi cha Kinyerezi III, kitakachozalisha megawati 1,000.

Kituo hicho kinajengwa eneo la Kinyerezi, jijini Dar es Salaam.

Pia, imeelezwa kuwa mashine zote tisa za kuzalisha umeme katika Bwawa la Kufua Umeme wa Maji la Julius Nyerere (JNHPP) zimekamilika na zimeanza kuzalisha jumla ya megawati 2,115.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya kuwashwa rasmi kwa mashine ya tisa na ya mwisho kwenye bwawa hilo Aprili 5, 2025, na sasa kila mashine kati ya hizo tisa inazalisha megawati 235.

Hii inathibitisha kuwa kuna uhakika mkubwa wa upatikanaji wa umeme nchini, huku hatua zilizobaki zikilenga kukamilisha miundombinu ya usambazaji katika baadhi ya maeneo ili kuhakikisha huduma hiyo muhimu inawafikia wananchi wote.

Hayo yamebainishwa leo, Alhamisi, Julai 10, 2025, na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, alipotembelea mitambo ya uzalishaji umeme ya Kinyerezi I na II pamoja na kituo cha kupokea na kusambaza gesi itokayo Mtwara cha GASCO.

Dk Biteko amesema Serikali imezindua mpango huo wa uzalishaji wa megawati 1,000 katika kituo hicho cha Kinyerezi III.

Akizungumza katika ziara hiyo, Naibu Waziri Mkuu huyo na Waziri wa Nishati amesema mpango wa awali ulikuwa ni kuzalisha megawati 600 kutoka kituo hicho cha Kinyerezi III.

“Lakini kutokana na ongezeko la mahitaji, Serikali imeamua kupanua uzalishaji zaidi. Kuna hitaji kubwa la umeme kila siku, Tanesco sasa imekuja na hatua ya kimkakati ya kupanua uzalishaji wa umeme kwa megawati 1,000 hapa Kinyerezi,” amesema.


Amesema Mkoa wa Dar es Salaam ulikuwa na maeneo korofi, akitolea mfano Kigamboni, Mbagala na Gongolamboto, lakini kwa sasa Serikali inaboresha na kuiimarisha miundombinu ya umeme iliyopo ili kumaliza tatizo hilo.

“Tulikuwa na transfoma hapa Kinyerezi ya MVA 50, kwa hiyo tumebadilisha, tumeweka transfoma mbili za 175-MVA, moja tayari inafanya kazi, nyingine inakamilishwa.

“Gongolamboto tunabadilisha, Mbagala tumebadilisha transfoma, na kituo cha Dege kwa upande wa Kigamboni tunaendelea nacho kukiimarisha,” amesema Dk Biteko.

Amesema kuwa kwa sasa kuna umeme mwingi unaozalishwa kutoka Bwawa la Julius Nyerere pamoja na umeme wa gesi, na kwamba Tanesco imechukua hatua mpya za kuongeza uzalishaji katika kituo cha Kinyerezi.

“Awali tulipanga kuzalisha megawati 600 pekee kwenye kituo hiki cha Kinyerezi III, lakini sasa tumeamua kuongeza angalau tufikie chanzo cha megawati 1,000,” amesema Dk Biteko.

Amefafanua kuwa, kwa kuchanganya chanzo hicho cha megawati 1,000 na vyanzo vingine vya umeme wa maji na jua, wanaamini Watanzania wataendelea kupata umeme wa kutosha ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka kila siku.

Aidha, amesema kuna mradi mkubwa wa ujenzi wa laini ya umeme kutoka Chalinze hadi Kinyerezi umbali wa kilomita 135, ambao baadaye utaunganisha pia eneo la Mkuranga lenye viwanda vingi.

Vilevile, amesema mikoa ikiwamo Katavi na Kigoma, ambayo awali ilikuwa inategemea mitambo ya majenereta kuzalisha umeme, sasa mitambo hiyo imezimwa baada ya kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa.

“Miradi yote hii inatekelezwa kwa kasi chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan. Sekta ya nishati ilitengewa Sh2.3 trilioni kwenye bajeti iliyopita, yote hii ikiwa ni kuhakikisha Watanzania wanapata umeme wa uhakika,” amesema Naibu Waziri Mkuu huyo.

Aidha, ameipongeza Tanesco kwa maboresho makubwa kwenye utoaji wa huduma, hasa katika kushughulikia changamoto na malalamiko ya wateja.

“Ninapokea mrejesho chanya kuhusu jinsi Tanesco mnavyoshughulikia kwa ufanisi malalamiko ya wateja kwa sasa, na tunatarajia kuona maboresho zaidi,” amesema.

Akitoa mfano wa Ripoti ya Hali ya Uchumi ya mwaka 2024, Dk Biteko amesema sekta ya nishati kwa sasa ni ya pili kwa kasi ya ukuaji nchini, ikiwa imekua kwa asilimia 14, jambo alilosema kuwa ni muhimu kwa maendeleo ya nchi.

Awali, akizungumza katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo ameishukuru Serikali kwa kazi kubwa inayofanya kuhakikisha umeme unapatikana bila kero.

Mpogolo amesema changamoto nyingi za umeme jijini Dar es Salaam zimepatiwa ufumbuzi, na sasa nishati hiyo inapatikana kwa uhakika, hali inayochangia chachu ya maendeleo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Lazaro Twange amemshukuru Dk Biteko kwa kutembelea mradi huo na kuwapongeza wafanyakazi wote wa shirika hilo wanaofanya kazi bila kuchoka kuhakikisha huduma ya umeme inapatikana.

“Ziara kama hizi husaidia kuhakikisha kuwa wananchi, kupitia vyombo vya habari, wanapata taarifa sahihi kuhusu maendeleo na juhudi zinazofanywa na shirika letu,” amesema Twange.

Naye Dk Mwinuka Lutengano, mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), alipozungumza na Mwananchi, amesema mkakati wa kuongeza uzalishaji wa nishati ya umeme ni muhimu kwa sababu unalenga kupunguza changamoto za upatikanaji wake kwenye maeneo ambayo bado hayajafikiwa ipasavyo.

Related Posts