Siku 170 za Mbowe nje ya siasa

Dar es Salaam. Zimetimia siku 170, tangu Freeman Mbowe alipowekwa kando kwenye uenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) baada ya nafasi yake kuchukuliwa na Tundu Lissu huku maswali yakitawala likiwemo anakwenda wapi?

Mbowe aliyeiongoza Chadema kwa miaka 21 kwa nafasi ya uenyekiti, uongozi wake ulitamatika asubuhi ya Januari 22, 2025 baada ya wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi waliokutana jijini Dar es Salaam kumchagua Lissu kuendeleza gurudumu.

Mwanasiasa huyu nguli wa siasa za upinzani, alikubaliana na matokeo ya uchaguzi huo kwa kumpongeza aliyekuwa makamu wake mwenyekiti bara, Lissu kwa kukabidhiwa kijiti cha uongozi wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Kwa mujibu wa katiba ya Chadema, Mbowe aliyewahi kuwa mwenyekiti, anakuwa mjumbe wa kudumu wa kamati kuu.

Hata hivyo, kukoma kwa wadhifa wake siku hiyo ndani ya Chadema, umekuwa mwisho wa sauti yake kusikika kisiasa.

Tangu wakati huo hadi leo ni siku 170 zimetimia huku Mbowe akiwa haonekani katika shughuli zozote zile za kisiasa ndani ya Chadema.

Hata hivyo, mwanasiasa huyo amekuwa akionekana katika baadhi ya matukio mengine ya kijamii mathalani misiba, sherehe na kanisani.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa, ukimya wa Mbowe ni uamuzi sahihi ili kuendeleza heshima aliyojijengea katika siasa za upinzani na hata kwenye medani za biashara na uwekezaji kwa kipindi kirefu.

Maswali na minong’ono imekuwa ikisikika maeneo mbalimbali kutoka ndani na nje ya Chadema kwamba, Mbowe aliyeijenga Chadema kimtandao kutoka ngazi ya chini hadi taifa amekuwa anatajwa tajwa huenda akabadili upepo wa kisiasa.

Duru za siasa zinamtaja Mbowe huenda akafanya uamuzi wa kwenda kujiunga na Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).

Minong’ono hiyo inasema, anaweza kupitishwa na wajumbe wa mkutano mkuu unaotarajia kukutaka wiki za mwisho za mwezi ujao kuwa mgombea urais.

Mbali na hiyo, kuna makada ambao ataungana nao kwenye safari hiyo mpya ya kisiasa.

Katika kipindi cha siku 170 Mbowe akiwa nje ya uongozi, mambo mengi yametokea Chadema. Ni kuondoka kwa makada wake ambao wamehamia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).

Mengine ni kusitishiwa ruzuku iliyofanywa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kufunguliwa kwa kesi dhidi ya baraza la wadhamini wa chama hicho, Msajili kutowatambua viongozi wa Chadema waliodhibitishwa na baraza kuu la chama hicho kwa madai akidi haikutimia pamoja na kukamatwa kwa Lissu.

Vilevile baadhi ya mali za chama zilichukuliwa na makada kwa madai wanakidai chama hicho, kuzuiwa kwa muda na Mahakama kwa chama hicho kufanya shughuli za kisiasa kutokana na kesi ya migogoro wa rasilimali inayoendelea mahakamani.

Mmoja wa viongozi wa kamati kuu aliyeomba hifadhi ya jina lake amesema: “Unajua ukimya wa mtu ni jibu tosha, mwenyekiti alitukanwa sana, akaitwa amelamba asali, sasa akisema azungumze si anaweza zungumza yale ambayo alikuwa nayaamini, si itakuwa shughuli? Kwa hiyo mimi naona sawa tu bora aendelee kukaa kimya.”

Kiongozi huyo ameongeza: “Mbowe ni hazina ya kisiasa nchini, amekwepa mishale mingine na anaweza kubadilika. Naamini siku moja ataibuka ndani ya chama au kwingineko kwani nguvu ya kuendeleza mapambano bado anayo.”

Hata hivyo, mara kadhaa, Mbowe ametafutwa na Mwananchi kwa simu pasipo mafanikio.

Katika kuonesha amekaa kimya kisiasa, hata katika kurasa zake za kijamii hususan wa X (zamani Twitter) ambao alikuwa akiutumia mara kwa mara, mara ya mwisho ‘ku- post’ ilikuwa Januari 23, 2025 siku moja baada ya kushindwa kutetea uenyekiti wake.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Richard Mbunda amesema tangu Mbowe kuondoka kwenye nafasi hiyo ametuhumiwa na mambo kadhaa yaliyoikumba Chadema ikiwamo kuibuka kwa kundi la G55 na makada wa chama hicho kuhamia Chaumma naye akihusishwa angeenda chama hicho.

Dk Mbunda amesema tuhuma zote hizo dhidi ya kiongozi huyo wa  zamani wa Chadema zinamsukuma angeongea watu kufahamu msimamo wake dhidi ya yanayosemwa kwani bado maswali yapo.

“Kuongea kwake ni jambo muhimu na inatarajiwa kwa ajili ya mustakabali wa chama na mustakabali wake yeye mwenyewe,” amesema.

Maoni hayo yanakinzana na alichosema Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa, Dk Conrad Masabo akieleza kuwa kuzungumza kwa kiongozi huyo hapaswi kulazimishwa.

Ni kweli alikuwa mwenyekiti na aliaga wajumbe hadharani, Lissu akasema wanaenda ‘Retreat’ na maelezo ya Lissu hakusema angetulia kwa muda gani, sisi tunaosema aongee inawekeana tusimtendee haki.

“Kwa yaliyokipata chama, Mbowe akiongea inaweza kuwa hasara na faida, anaweza kuharibu hali ilivyo au kuiboresha hali ilivyo sasa ili kujua hivyo lazima tumfahamu huyu mtu ni wa namna gani.

Dk Masabo amemuelezea Mbowe kama mwanasiasa anayeweza kutuliza hali ‘Flexible adjastment’ akitolea mfao namna alivyotoka gerezani na kwenda kuonana na Rais Ikulu.

Katika hoja yake, Dk Masabo amesema Mbowe kama atazungumza na kauli yake kutoendana na wanachama wote itaweza kumuathiri kisiasa.

“Ushauri atakaoutoa utapokelewaje na watu wengine, nahisi hiki ndicho kinamtatiza na mimi nahisi yeye hataki kutoa ushauri unaoendana na wakiowengi kwa sasa.

“Ametuhumiwa kuhusika na watu waliohama kwenda Chaumma, kundi la G55 mambo yote mabaya kahusishwa nayo sasa chochote atakachozungumza kitamweka kwenye mazingira ya kudhibitisha hayo au kukanusha,” amesema.

Katikati ya mjadala huo, Mchambuzi wa masuala ya saisa, Dk Faraja Christomus amesema miongoni mwa mambo yaliyofanya upande wa Lissu kabla ya uchaguzi wao ni madai ya Mbowe kuhodhi mali za chama na kuendelea kukidai chama kwa madai ya kuwa alikikopesha.

Mchambuzi huyo amesema haishangazi kuona Mbowe yuko kimya tangu uchaguzi wa chama chake umalizike kwani inawekana nje ya uongozi anakataka matakwa yake yatimizwe na kwa kuwa hana cha kupoteza.

Akizungumzia hilo, Mhadhiri wa Rasilimali watu na Utawala wa Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam, Dk Lazaro Swai amesema ukimya wa Mbowe unatia shaka kuhusu hatma yake kisiasa.

Ameeleza kwa inavyoonekana Mbowe sio wa kurudi ndani ya chama chake, wala kuhamia chama kingine cha siasa, hivyo pengine ameamua kutundika daruga katika siasa.

Kwa mujibu wa Dk Swai, ukimya wa Mbowe unalenga kuendeleza heshima yake katika medani za siasa, kwani uamuzi wowote wakati huu, ama utamfutia historia njema au kumuongezea.

Mwanazuoni huyo anaona ni busara kwa Mbowe kuendeleza ukimya kuhusu yanayoendelea ndani ya chama chake na hata katika medani za siasa kwa jumla wake.

“Atawashangaza wengi iwapo atasikika akuzungumzia siasa za jumla wakati ndani ya chama chake kuna mambo yanayoendelea. Ni busara akae kimya ili aendeleze heshima yake,” ameeleza.

Katika mazingira ya kisiasa aliyopitia Mbowe, amesema anadhani ukimya wake unalenga kuzishinda kauli alizoziita za kitoto dhidi yake na hiyo ndiyo maana ya ukomavu.

“Ametukanwa sana, amesemwa sana, kukaa kimya ni chaguo sahihi kwake. Aliijenga heshima ndani ya chama chake, ana heshima ya fedha kutokana na biashara, ukimya unaendeleza heshima yake,” amesema.

Kada wa Chadema, Yeriko Nyerere akizungumza na Mwananchi amesema suala la mwenyekiti huyo wa zamani kuzungumza au kutozungumza ni uamuzi wake.

“Mtazamo wangu mwenyekiti akishaondoka madarakani anawaacha wengine waliochaguliwa kufanya kazi, kuzungumza ni kuwaingilia na pengine hiyo ndio busara inayomuongoza kuwaacha waliochaguliwa waendelee kufanya kazi, ameheshimu maoni ya wanachama wa Chadema ya kumtaka apumzike,” amesema.

Related Posts