Juma Mgunda nje, Mzambia anaingia Namungo

UONGOZI wa Namungo FC umeachana rasmi na aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Juma Mgunda, baada ya kufikia makubaliano ya kusitisha mkataba kwa pande zote mbili, huku Mzambia Hanour Janza aliyewahi kuifundisha akitajwa kurithi mikoba hiyo kwa msimu ujao wa mashindano.

Mbali na Mgunda, Namungo pia imeshawapa ‘thank you’ wachezaji watatu waliokuwa na kikosi hicho akiwemo Erick Kapaito, Emmanuel Charles na Abderson Solomon, huku ikielezwa panga linaendelea ili kupisha mashine mpya zilizoanza kuingia kwa fujo Kwa Wauaji  hao wa Kusini.

Akizungumza na Mwanaspoti Mratibu wa Namungo, Ally Suleiman, aliliambia Mwanaspoti kama kuna taarifa juu ya suala hilo, watazitolea ufafanuzi kwa mashabiki zao, japo kwa sasa wanaendelea na maboresho ya nyota wapya kwa ajili ya msimu ujao.

“Taarifa yoyote inayohusu klabu huwa tunazitoa pale inapobidi kuzitoa au kuzitolea ufafanuzi, kama ni kweli tumeachana naye tutatangaza na kuweka wazi na mashabiki zetu watafahamu, ingawa kwa sasa tuwe na subra kwanza,” alisema Suleiman.

Licha ya kauli hiyo, ila mmoja wa kiongozi wa timu hiyo aliyeomba kuhifadhiwa jina lake aliliambia Mwanaspoti ni kweli Mgunda ameachana na kikosi hicho, huku mabosi wakiwa katika harakati za kumrejesha Janza aliyewahi kufanya nao pia kazi.

“Janza aliondoka Namungo kwa heshima na uongozi unaona kama mbadala sahihi wa Mgunda, mazungumzo yanaendelea vizuri na ikiwa tutafikia makubaliano atakuwa ndiye kocha wetu mkuu wa kikosi chetu kuanzia msimu ujao,” kilisema chanzo hicho.

Related Posts