YALIYOPITA si ndwele na kijiwe kinatembea na kauli hiyo muda huu mfupi ambao umebakia kabla ya kuanza kwa Fainali za Mafaifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) 2024.
Ni mashindano yatakayofanyika katika ardhi yetu kwa maana Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu wenyeji wa mashindano hayo ambayo kwa mara ya kwanza yalifanyika mwaka 2009 na tulishiriki.
Na Tanzania tumepata bahati kubwa ya kupewa mechi ya ufunguzi wa mashindano hayo ambayo itachezwa Agosti 2, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na timu yetu ya taifa ‘Taifa Stars’ itacheza na Burkina Faso.
Ukiondoa kupewa mchezo wa ufunguzi, Tanzania kuna bahati nyingine ambayo tumeipata ambayo ni makundi mawili ya timu zinazoshiriki mashindano hayo, mechi zake kuchezwa ndani ya Tanzania huku Kenya na Uganda zenyewe zikipata kundi moja moja.
Mechi za kundi B ambalo linaundwa na timu Tanzania, Mauritania, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Madagascar na Burkina Faso zitachezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na mechi za kundi D ambalo lina timu za Senegal, Sudan, Congo na Nigeria zitachezwa katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Tunakumbushana hapa kijiweni mashindano ya CHAN yana faida kubwa kwa nchi kuanzia kwa timu yenyewe ya taifa na hata watu wa kawaida mmoja mmoja ikiwa fursa hiyo itatumika vizuri.
Siku zote mafanikio hayajawahi kumfuata mtu mvivu hivyo fursa hizo za CHAN 2024 hatuwezi kuzipata kama tutajifungia ndani na kungoja zije ila tunatakiwa kuzifuata popote zilipo kuanzia mashindano yanapoanza hadi kumalizika.
Lakini wakati tukipeana michongo ya fursa za CHAN, tunatakiwa kupeleka nguvu na akili zote katika kuhakikisha timu yetu ya taifa inafanya vizuri ili ifike hatua za juu za mashindano hayo ya pili kwa ukubwa kwa ngazi ya timu za taifa barani Afrika.
Nguvu hiyo isiishie kwa maandalizi ya timu pekee bali pia katika maeneo mengine ya msingi ambayo ndio yanawezesha mashindano kufanyika kwa ufasaha.