Mecky Maxime atajwa Mtibwa Sugar

LICHA ya kuipambania Dodoma Jiji kujihakikishia nafasi ya kucheza ligi msimu ujao 2025/26, Kocha Mecky Maxime hatakuwa sehemu ya benchi la ufundi la timu hiyo akitajwa kurudi Mtibwa Sugar.

Maxime alijiunga na Dodoma Jiji, Juni 19, 2024 akitokea Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars na anatajwa kurudi timu aliyoicheza na kuifundisha kwa muda mrefu baada ya kupanda daraja msimu huu.

Chanzo cha kuaminika kutoka Mtibwa Sugar ambayo inaendelea kusuka kikosi chao tayari kwa mapambano ya ligi kuu, kilisema klabu hiyo ipo katika hatua za mwisho za mazungumzo ya kumrudisha Maxime.

“Tunafahamu uwezo wake, pia anaifahamu vizuri timu na tayari mazungumzo kati yetu yanaenda vizuri na mambo yakienda kama tulivyopanga, basi atakuwa sehemu ya benchi letu la ufundi msimu ujao,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza;

“Kila kitu kinaenda kama kilivyopangwa, mikakati tuliyonayo siyo kuimarisha benchi tu, hata kikosi tunakiandaa kiwe bora na cha ushindani. Tunataka kurudi na nguvu na kuonyesha ushindani baada ya kuteleza.”

Kocha huyo ambaye anatajwa bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Dodoma Jiji, hilo halitakuwa na pingamizi kwake kwani tayari waajiri wake hao wapo kwenye mchakato wa kumvunjia mkataba.

Mtibwa Sugar iliyoshuka daraja msimu uliopita sambamba na Geita Gold imerejea ikiwa imetwaa taji la Championship na tayari imeanza kufanya usajili ikizingatia nyota wenye uzoefu.

Related Posts