Kilio cha mama wa pacha fedha yakwamisha matibabu ya kichanga

Kilolo. Kwa sauti ya majonzi huku machozi yakimtoka na kushindwa kujizuia, Redigunda Kimaro ameeleza namna anavyoishi kwa tabu na mwanawe Delvin Magova (wiki mbili) mwenye tatizo la kichwa kikubwa, baada ya kukosa fedha za kwenda Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa matibabu zaidi.

Mgongo wazi na kichwa kikubwa ni ulemavu ambao mtoto huzaliwa nao, chanzo kikiwa ni ukosefu wa madini ya foliki asidi kwa mjamzito.

Mtoto huyo ambaye alizaliwa Juni 21, 2025 katika Hospitali ya Dabaga wilayani Kilolo, mkoani Iringa, ameshindwa kufikishwa BMH kutokana na hali ya kiuchumi ya familia yake.

‎Redigunda amesema tangu azaliwe, Delvin amekuwa akilia muda wote kwa maumivu, hali inayomfanya ashindwe kunyonya huku shingo yake ikiwa haina nguvu kama pacha wake wa kike.  

‎ Jumatano Julai 9, 2025 Mwananchi Digital imefunga safari ya takribani kilomita 67 kutoka Iringa mjini hadi Kijiji cha Ilamba, Kata ya Dabaga, wilayani Kilolo mkoani Iringa kufika katika familia hiyo iliyogubikwa na huzuni pamoja na wasiwasi juu ya maisha ya mtoto wao.

‎Redigunda amesema alijifungua mtoto huyo katika Hospitali ya Udzungwa akiwa na pacha mwenzake wa kike, lakini furaha ya kupata watoto hao ilizimwa ghafla alipofahamishwa kuwa mtoto wa kiume ana tatizo la maji kichwani yaani kichwa kikubwa.

‎Baada ya hali hiyo, alielekezwa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, ambapo vipimo vilithibitisha hali hiyo na ushauri ukatolewa kwamba aende Hospitali ya Taifa Muhimbili au Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma kwa matibabu ya kibingwa.

‎“Baada ya maelekezo hayo, tulishindwa kabisa kuendelea na safari kwa sababu hatuna uwezo wa kifedha,” amesema Redigunda na kuongeza;

‎“Tulilazimika kurudi nyumbani bila huduma yoyote na sasa tumeendelea kumuangalia tu mtoto akiwa nyumbani.”

‎Redigunda anaendelea kusema kuwa hali ya mtoto inazidi kuwa mbaya kwani analia kila wakati, mara nyingine bila sauti, hali inayoashiria maumivu makali.

‎“Ni vigumu hata kumshika kichwani kwani ukimshika kichwa chake hubonyea na macho yake huonyesha hali ya maumivu.

‎”Tunaomba kwa mtu ambaye anaweza kutusaidia kwa chochote namba ya kutuma fedha au mawasiliano na familia yetu ni 0741161580 jina ni Redigunda Kimaro,” amesema.

‎Baba wa mtoto, Valentino Magova mkazi wa kijiji hicho cha Ilamba wilayani Kilolo mkoani Iringa, ameeleza kuwa hali ya mwanaye ni mbaya kwani hapati usingizi, hajiwezi na kilio chake ni cha maumivu ya ndani.

‎“Hakuna huduma yoyote ambayo tumepata mpaka sasa. Tunaishi kwa matumaini kwamba kuna mkono wa msaada utanyanyuka na tunaomba Serikali, mashirika ya kiraia na watu binafsi wasikie kilio hiki,” amesema Magova kwa sauti ya kukata tamaa.

‎Magova ameongeza kuwa kutokana na ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu ugonjwa huo, familia imejawa na hofu kubwa kuhusu mustakabali wa maisha ya mtoto wao.

‎Vilevile Magova ameiambia Mwananchi Digital kuwa changamoto nyingine ni umbali wa hospitali na gharama za usafiri hadi kufika Dar es Salaam au Dodoma, jambo linalofanya hata kufikiria matibabu kuwa mzigo mkubwa kwao.

‎Mjumbe wa Mtaa wa Udzungwa, Kata ya Dabaga, Jenifer Fuluge, amesema kuwa kijiji chao hakijawahi kukumbwa na tukio la aina hiyo na kwamba hali hiyo imeleta simanzi miongoni mwa wakazi wote.

‎“Hali hii tunayoiona kwa familia hii ni ya kusikitisha. Tumezoea kusikia kwenye vyombo vya habari au mitandaoni. Lakini sasa imetufikia moja kwa moja hivyo tunaomba Serikali iingilie kati kwa haraka,” amesema Jenifer.

‎Jenifer ameeleza kuwa hata kijiji chao hakina uwezo wa kuchangia gharama kubwa za matibabu na hivyo msaada kutoka nje ni muhimu ili kunusuru maisha ya mtoto huyo.

‎Jenifer ameongeza kuwa kama kiongozi wa mtaa, tayari ameanza kuzungumza na baadhi ya wadau ili kuona kama kuna namna ya kusaidia familia hiyo japo kwa hatua za awali.

‎ Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kupitia Chama cha Mapinduzi CCM Kata ya Dabaga Wilayani Kilolo mkoani Iringa, Juliana Msigala, amesema kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kushiriki kusaidia katika shida mbalimbali za wananchi akitaka wenye uwezo huo wajitokeze.

‎Juliana amesema kuwa wanawake wa UWT kata hiyo wameguswa na wanapanga kuchangishana japo kiasi kidogo kama sehemu ya kuonyesha mshikamano wa kijamii.

‎“Lakini ukweli ni kwamba kiwango kinachohitajika kwa matibabu haya ni kikubwa. Serikali na mashirika binafsi nguvu yao ni ya muhimu,” amesema Juliana.

‎“Maisha ya mtoto huyu ni vyema kusaidiwa na hili siyo jambo la kupuuzia ni wakati sasa wa kuonyesha ubinadamu wetu kwa vitendo,” amesema.

Hata hivyo, Chama cha Wazazi wa Watoto wenye Vichwa Vikubwa na Mgongo Wazi (ASBAHT) kinasisitiza kuwa ni muhimu kwa wazazi watarajiwa kuhakikisha wanapata vyakula vyenye madini hayo ili kuepuka kupata watoto wenye ulemavu.

Related Posts