Unguja. Katika kutatua changamoto za watu wenye ulemavu kuhusu upatikanaji wa mikopo inayotolewa na Serikali, Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) na Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar wamesaini hati ya makubaliano yenye lengo la kuhakikisha watu hao wanapata fursa bila vikwazo.
Akizungumza leo Ijumaa, Julai 11, 2025, katika utiaji saini huo, Katibu wa baraza hilo, Ussi Khamis Debe amesema awali watu wenye ulemavu hawakuwa wakiipata mikopo hiyo kwa urahisi kutokana na muongozo uliokuwepo wa kuunda vikundi.
Amesema kundi hilo lilikuwa likiipata mikopo hiyo kwa shida, kwani vikundi vilivyokuwepo vilikuwa na watu wenye ulemavu tofauti, jambo lililowanufaisha wachache.
“Kwa niaba ya kundi hili la watu wenye ulemavu, naomba kuchukua nafasi hii kutoa shukrani kwa kusikiliza kilio chetu cha muda mrefu ambacho kilikuwa kikirudisha nyuma jitihada za wajasiriamali wenye ulemavu,” amesema Debe.
Amesema hati hiyo iliyosainiwa ni kwa ajili ya kutoa mkopo kwa mtu mmoja mmoja na si kwa vikundi ili kila mtu afikiwe kwa wakati wake.
Amesisitiza kuwa mkataba huo utafungua ukurasa mpya na faraja kwa kundi hilo, kwani kwa wengine hilo linatokea kwa mara ya kwanza upande wa Zanzibar.
Kwa upande wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Shariff Ali Shariff amesema mkataba huo utawanufaisha wananchi 160,000 wenye ulemavu ambao wamejiajiri.
Amesema lengo la kutolewa mikopo hiyo kwa mtu mmoja mmoja ni kujikwamua kiuchumi kwa kufanya biashara ambazo zitawaingizia kipato na si kwa lengo lingine.
Shariff amesema Serikali kupitia ZEEA imetenga Sh570 milioni kwa ajili ya watu wenye ulemavu, ambapo hadi kufikia sasa Sh66 milioni pekee ndizo zilizochukuliwa, hivyo kundi hilo lijitokeze kuchukua fedha hizo kwa sababu ni zao.
Waziri Shariff amefafanua kuwa fedha zilibaki, si kwamba hawazitaki, bali miongozo na taratibu zilizowekwa si rafiki kwao.
“Baada ya kuona changamoto hiyo, Serikali tumeichukua na kulifanyia kazi. Na sasa wanaweza kupata fedha hizo, badala ya kuja kwa vikundi, sasa itatolewa kwa mtu mmoja mmoja,” amesema Shariff.
Hivyo, ametoa wito kwa kundi hilo lijitokeze kwa wingi kuzichukua fedha hizo, kwani wasipofanya hivyo zitatolewa kwa makundi mengine ambayo yataonekana kuwa na uhitaji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA), Juma Burhan Mohamed amesema sababu kuu mbili zilizochangia kundi hilo kukosa fursa ya mikopo ni pamoja na changamoto ya muongozo wa kuweka vikundi, na asilimia ya vikundi hivyo wanufaika hawakuwa watu wenye ulemavu.
“Kabla ya utiaji saini huo, watu wenye ulemavu walikuwa wanatakiwa kuunda vikundi kwa ajili ya kupata mikopo hiyo, jambo lililokuwa likiwaia vigumu, na fursa hiyo kuchukuliwa na wengine ambao si walemavu kujinufaisha wao,” amesema Burhan.
Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa mikopo hiyo itatolewa bila ya kuwa na riba, kwani itadhaminiwa na Baraza la Watu Wenye Ulemavu ili kuwapa ahueni wajasiriamali watakaochukua mikopo hiyo.
“Udhamini wa mikopo hii ya mtu mmoja mmoja utabebwa na Baraza la Watu Wenye Ulemavu, na tayari limeweka Sh100 milioni kwa kuanzia ambayo itakuwa ndiyo dhamana kwao, na hilo litakuwa chachu kwa wajasiriamali walemavu,” amesema