Maajabu ya parachichi kwa afya ya binadamu

Dar es Salaam. Parachichi  ni miongoni mwa matunda yenye faida kubwa mwilini, na moja wapo ya faida hiyo ni kuimarisha usagaji wa chakula tumboni.

Utafiti mwingi unaonesha kuwa watu wenye mazoea ya kula tunda hilo kwa wingi, huwa na afya njema na uzito unaokubalika kiafya.

Tunda hilo lenye mafuta mengi, linasaidia kupunguza hatari ya mtu kupatwa na kiharusi au ugonjwa wa moyo.

Dk Edwin Kidegwa ni mshauri na mtoa huduma ya matibabu kwa kutumia virutubisho tiba kutoka Nutritional Health Care( NH- Care),  anasema moja ya faida ya parachichi mwilini ni kudhibiti shinikizo la damu, kushusha kiwango cha lehemu, kudhibiti ugonjwa wa kisukari , kupunguza maumivu ya viungo na magonjwa ya kuvimba pamoja na kuimarisha uwezo wa kuona vizuri.

Anasema faida nyingine ni pamoja na kuimarisha mifupa ya mwili, kuimarisha usagaji wa chakula tumboni, lakini pia parachichi ni moja ya matunda ambayo hufaa zaidi kuliwa na wajawazito.

Pia, tunda la parachichi lina virutubisho vya aina mbalimbali, ambavyo ni pamoja na vitamin C, B6, E, K pamoja na madini ya ‘copper’ na ‘potassium.’

Pia mbegu ya tunda la parachichi nayo huwasaidia wale wenye shida ya kupata maumivu na kukwama kwa haja ndogo.

Ili mbegu hiyo ya parachichi iwe tiba ya tatizo hilo ni lazima kwanza isagwe hadi iwe unga kabisa na kisha kukaangwa kidogo.

Baada ya zoezi hilo kukamilika mhusika (mgonjwa) atakuwa akitumia unga huo kwa kuchanganya kwenye maji ya moto na kunywa.

Pamoja na faida mbalimbali, bado parachichi linaendelea kuonekana kuwa na umuhimu kwa maisha yetu,  kwani husaidia pia kwenye masuala ya urembo hususan urembo wa ngozi pamoja na kukuza nywele na kuzifanya kukua vizuri bila kuzuia kukatika.

Mbali na hayo, tunda hilo ni muhimu kwa watoto kwani huwasaidia  kuwa na ngozi nzuri na kukua vizuri huku wakiwa na afya bora.

Miongoni mwa faida za parachichi kwa mtoto kuanzia umri wa miezi sita na kuendelea ni pamoja na kumpatia vitamini nyingi pamoja na madini na miongoni mwa vitamin hizo ni pamoja na vitamin C, A, E na vitamin B-6 pamoja na madini kama vile ‘calcium,’ madini ya chuma, ‘magnesium,’ ‘potassium’, ‘zinc’, ‘phosphorous’ na ‘sodium’ ambayo yote hayo ni muhimu sana kwa maendeleo ya afya ya mtoto.

Aidha, matumizi ya tunda la parachichi kwa mtoto husaidia sana kuboresha afya ya macho na akili ya mtoto.

Pia matumizi ya parachichi husaidia kuimarisha mmeng’enyo wa chakula kwa mtoto na hivyo kumuepusha dhidi ya tatizo la kukosa choo, lakini pia husaidia kuondosha maumivu madogomadogo ya tumbo na ili kupata faida zaidi ni nzuri akasagiwa na kunywa juisi yake.

Matumizi ya mara kwa mara ya parachichi husaidia kulinda afya ya ini kwa watoto mwenye umri zaidi ya miezi sita na kuendelea, na hivyo kumuepusha dhidi ya magonjwa ya ini pamoja na moyo.

Related Posts