Kutokana na dunia kupiga hatua za kimawasiliano kupitia mitandao, ni kawaida kuzagaa kwa taarifa za afya ambazo zinaweza kuwa za kweli na hata zile potofu.
Moja ya tatizo la kiafya ambalo ni kawaida kulisikia na kuona matangazo yake sana mtandaoni na mitaani, ni tatizo la kiafya la PID kwa wanawake.
Kirefu cha PID ni ‘Pelvic Inflammatory disease’, yaani maambukizi ya via vya uzazi vya juu kwa wanawake. Ni tatizo linalomwathiri yeyote, lakini zaidi ni wale wanaojamiiana wakiwa na umri wa miaka 20 na zaidi.
Inakadiriwa kitakwimu wanaougua PID ni asilimia 85 sababu, na sababu ikitajwa kuwa ni vimelea wanaoenezwa kwa njia ya kujamiiana bila kinga, hasa bakteria jamii ya ‘Neisseria Gonorrhoeae’ pamoja na ‘Chlamydia trachomatis’.
Vimelea hawa huingia kupitia ukeni mpaka katika nyumba ya uzazi, mirija ya uzazi ama kokwa za kike au kiwanda cha vijiyai vya kike na viungo jirani vilivyopo kiunoni.
Ni maambukizi yanayoweza kusababisha maumivu sugu chini ya tumbo au kiunoni, homa na madhara ya muda mrefu kama vile ugumba, mimba kutunga nje ya kizazi na uharibifu wa mfumo wa uzazi. Hii hutokea endapo hatua sahihi za mapema hazitachukuliwa.
Uzoefu unaonyesha wanawake wengi huchelewa kufika katika huduma za matibabu, hali inayochangiwa na taarifa potofu ambazo zinawavutia na kuwaaminisha wagonjwa kuwa, wanaweza kutibiwa kwa dawa za mitishamba au tiba mbadala.
Tofauti na huduma za afya za tiba zilizo chini ya Serikali, huwezi kukuta bango la kibiashara au tangazo linalokuvuta kwenda kununua dawa au kupata tiba za kutatua tatizo fulani la kiafya.
Hii ni kwa sababu fani ya tiba ina maadili na miiko yake, ikiwamo kukataza kumvutia mgonjwa kwa matangazo ya biashara. Hii ina maana kuwa huduma ya afya siyo biashara.
Hata hivyo, baadhi ya huduma nyingine za tiba mbadala, hazina miiko ya kuzuia kumvutia mgonjwa kuja kumtibu kupitia matangazo. Na hapo ndipo wanawake wengi wenye tatizo la PID wanapojikuta wakiangukia kwa wataalamu, ambao kimsingi wameweka maslahi ya kifedha mbele.
Kibaya zaidi viwango vya elimu vya matabibu hao, havilingani na changamoto za PID zinazohitaji huduma za kibingwa au bobezi, ikiwamo kuziba kwa mirija ya uzazi au mimba kutunga nje ya kizazi.
Linganisha ujuzi wa kutibu PID pamoja na madhara yake kwa aliyesoma tiba mbadala miezi sita hadi 12 na daktari bingwa wa kinamama mwenye shahada ya kwanza ya miaka mitano, ubingwa miaka mitatu hadi minne na ubobezi wa miaka miwili hadi mitatu.
PID inapocheleweshwa kutibiwa mapema, inaweza kusababisha maumivu ya muda mrefu eneo la kiunoni kwa baadhi ya wanawake, wakati kwa wengine, dalili zinaweza kuwa ndogo au zisionekane kabisa.
Ndio maana baadhi huwa hawajui kuwa wana PID., ambayo hutokea katika hatua tatu ikiwamo kuanzia kwenye kizazi, ikifuatiwa na tando nyororo ya nyumba ya uzazi na kisha mirija ya uzazi.
Ni muhimu wanawake kuchunguza afya mara kwa mara na kupimwa magonjwa yanayotokana na kujamiana angalau mara moja kwa mwaka. Hii inasaidia kubaini tatizo hili kwa wale wenye PID lakini hawana dalili zozote.
Dalili za PID zinaweza kujumuisha maumivu ya chini ya tumbo au uchungu ambao unaweza kuwa mbaya zaidi unapojongesha mwili, matatizo ya hedhi kama vile hedhi yenye maumivu makali yasiyovumilika, maumivu makali wakati kijiyai kinapopevuka na kutokwa na uchafu mwingi ukeni.
Vile vile harufu mbaya ukeni au harufu ya shombo la samaki, kutokwa uchafu wenye rangi kijivu au mchanganyiko kijani njano na usaha, kutoka damu kiasi baada ya kujamiana, maumivu wakati kujamiana, homa, kichefuchefu na kutapika.
Ni kawaida kukuta tatizo la PID likihusishwa mara mwa mara na maambukizi ya mfumo wa mkojo yaani U.T.I na magonjwa yanayoenea kwa kujamiana yaani kwa kifupi S.T.I au STDs. Ukweli ni kuwa vimelea wanaosababisha PID kwa kiasi kikubwa ni walewale wanaosababisha STI.
Kwa upande wa UTI, kwa uchache vijidudu vinavyosababisha STI vinaweza kusababisha UTI kwa asilimia 2-4. Na hasa panapokuwepo na vimchubuko eneo la uzazi la wanawake.
Vimelea wanaweza wakapata mazingira hayo, baadaye wakaingia njia ya mkojo na kusababisha maambukizi katika mfumo wa mkojo.
Ingawa UTI inasababishwa zaidi na vimelea waliopo kwenye njia ya haja kubwa. Ujirani wa eneo hili na uke, na umbile la mrija wa mkojo wa mwanamke unawaweka katika hatari ya kupata UTI.
Uzaagaji wa taarifa potofu zinazovuma huweza kusababisha mifarakano kwa wenza wawili wenye uhusiano wanaoshiriki tendo bila kinga. Ni kawaida kudhani mwenza fulani sio mwaminifu.
Upo uvumi kuwa PID daima huwa na dalili, ukweli ni kuwa wanawake wengi wenye PID hawana dalili zinazoonekana, jambo ambalo linaweza kuchelewesha utambuzi na matibabu.
Daktari anapobaini tatizo hushauri mhusika afike na kuchunguzwa yeye na mwenza anayejamiana naye. Hii ni muhimu ili kuzuia maambukizi lakini haimaanishi kila PID ni lazima chanzo kiwe kujamiiana.
Ingawa ni kweli chanzo kikubwa ni hilo, PID inaweza pia kutokana na mambo mengine kama vile wakati wa kujifungua, kuharibika kwa mimba au upasuaji wa viungo vilivyopo ndani ya pango la kiuno.
PID haienei kwa kugusana, ukweli ni kuwa PID haiambukizwi kwa njia sawa na homa za mafua au upele kama wa tetekuwanga. Ukweli ni kuwa huenea zaidi kwa njia ya kujamiana.
Vipo vimelea rafiki waliopo juu ya ngozi wakipata nafasi na kuingia njia ya uzazi, wanasababisha tatizo hili ingawa ni mara chache.
PID inaweza kutibiwa kwa dawa za dukani, dawa maarufu zinazonunuliwa kiholela ni sindano za powercef na tembe za azithromycin.
Ukweli ni kuwa PID inahitaji uchunguzi kwanza na baadaye kutibiwa kwa dawa mchanganyiko za antibiotiki. Hi ni kwa sababu baadhi ya vimelea wa tatizo hili wana usugu wa dawa.
Hata kama utapata matibabu ya mafanikio mtaani au mtandaoni, PID inaweza kusababisha maumivu ya muda mrefu eneo la kiuno au chini ya tumbo.
Inaweza kusababisha kovu kwenye tishu, hatimaye kusababisha matatizo kama vile mimba nje ya kizazi au ugumba.
Utambuzi wa mapema na matibabu ni muhimu, kwasababu unaweza kusaidia kuzuia uharibifu wa muda mrefu wa mfumo wa uzazi.
Aidha, kondomu inaweza kusaidia kuzuia PID kwasababu inazuia kuenea kwa magonjwa yanayoenea kwa kujamiana ikiwa itatumiwa kwa usahihi.
Kufika katika huduma za afya ni muhimu, kwasababu ugunduzi wa tatizo kwa usahihi unahusisha mambo mengi ikiwamo historia ya ugonjwa, matibabu aliyopata, dalili, uchunguzi wa mwili, tumbo na viungo vya uzazi, vipimo vya damu na mkojo.
Hii inakupa picha sahihi, kuwa hakuna tiba ya mtaani inayoweza kukutibu kwa usahihi, ndio maana tunawasihi wanawake kuepuka matibabu yasiyo rasmi ya mtaani na mitandaoni.
Ni muhimu kwa wanawake kula lishe bora ili wawe na miili yenye kinga imara. Lakini unapobainika kuwa na PID , ni lazima upata dawa rasmi ili kuepusha madhara zaidi ya vimelea.