::::::::
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, ameiagiza Idara ya Uhamiaji kuwekeza nguvu zaidi katika kuimarisha doria na misako usiku na mchana nchi nzima katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, kwa kuhakikisha hakuna mgeni au makundi ya wageni wenye nia ovu ya kuhamasisha au kuchochea uvunjifu wa amani nchini.
Pia, ameitaka Idara ya Uhamiaji kutatua kwa haraka mapingamizi ya uraia kwa wagombea wa nafasi mbalimbali kwa umakini na kufuata sheria na taratibu, pamoja na kushirikiana na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya uraia.
“Nitumie nafasi hii kuielekeza Idara ya Uhamiaji kuwekeza nguvu zaidi katika Kuimarisha doria na misako muda wote, ndani ya nchi yetu katika Mikoa yote usiku na mchana hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu na hata baada ya Uchaguzi kwa kuhakikisha hakuna mgeni au kundi la wageni mwenye nia ovu kuhamasisha au kuchochea uvunjifu wa amani ndani ya nchi yetu” amesisitiza Bashungwa.
Bashungwa ametoa maelekezo hayo leo, tarehe 11 Julai 2025, wakati akizindua na kupokea jengo jipya la Ofisi za Uhamiaji za Wilaya ya Busega mkoani Simiyu, lililofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM).
Bashungwa amesema Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika mwaka wa fedha 2025/2026, imetenga jumla ya shilingi bilioni 3.8 kwa ajili ya kuendeleza na kukamilisha miradi ya Idara ya Uhamiaji, ambapo Mkoa wa Simiyu umetengewa bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Uhamiaji la mkoa.
Aidha, Bashungwa ameipongeza Idara ya Uhamiaji kwa kuendelea kutoa huduma nzuri za kiuhamiaji kwa wananchi na wageni, ikiwa ni pamoja na kudhibiti wahamiaji haramu, pamoja na kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kuwezesha wageni na watalii kuendelea kuongezeka nchini.
Bashungwa ametoa rai kwa wananchi kuendelea kuwa raia wema kwa kuishi kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi, na kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama wanapokuwa na mashaka juu ya mgeni au matendo ya uvunjifu wa amani.
Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji (CGI), Dkt. Anna Makakala, amesema ujenzi wa jengo la Uhamiaji Wilaya ya Busega ulianza Oktoba 28, 2024, na kukamilika Juni 20, 2025, ambapo umegharimu kiasi cha shilingi milioni 628 ambazo zimetokana na ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha, amesema ujenzi wa jengo hilo la Uhamiaji Wilaya ya Busega litakuwa msaada mkubwa katika kukabiliana na wahamiaji haramu kutoka nchi jirani, kwani eneo hilo limepakana na Ziwa Victoria upande wa Kenya na Uganda.