AG, IGP kujitetea kesi ya waumini Kanisa la Gwajima

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma imetoa siku 10 kwa wajibu maombi kuwasilisha utetezi wa maandishi katika shauri la Kikatiba lililofunguliwa na baadhi ya waumini wa Kanisa la Glory of Christ Tanzania Church.

Shauri hilo la maombi mchanganyiko namba 16408 limefunguliwa na Dinali Mbaga na wenzake 51 dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP).

Waombaji ambao kanisa lao lililoko Ubungo, Dar es Salaam limefungwa wanapinga kitendo cha Jeshi la Polisi kuwazuia kukusanyika kufanya ibada.

Shauri hilo linalosikilizwa na jopo la majaji Cyprian Mkeha, Ephery Kisanya na Zahra Maruma, katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, limetajwa kwa mara ya kwanza leo Ijumaa, Julai 11, 2025.

Kiongozi wa jopo la mawakili wa wajibu maombi, Wakili wa Serikali Mkuu, Vivian Method ameieleza mahakama walipewa nyaraka za shauri hilo jana Julai 10, 2025.

Amesema kwa mujibu wa Kanuni za Uendeshaji Mashauri ya Kikatiba, Kanuni ya 6(1) mjibu maombi anatakiwa kuwasilisha majibu ndani ya siku 14 tangu alipoyapokea.

“Kwa hali hiyo tunaomba kuwasilisha majibu yetu ndani ya siku 10 kwa kuzingatia shauri hilo limeletwa chini ya hati ya dharura na kwa kuzingatia mjibu maombi wa pili yuko Dodoma na shauri liko Dar na tunahitaji kupata taarifa kutoka kwake, tukutane naye tuweze kuandaa majibu,” amesema.

Wakili wa waombaji, Peter Kibatala ameomba wajibu maombi wapewe siku saba ili kuwasilisha utetezi wao kwa kuwa shauri hilo limewasilishwa chini ya hati ya dharura na suala lenyewe linagusa haki muhimu. 

Mahakama imekubali ombi la wajibu maoni na kutoa siku 10.

Kiongozi wa jopo, Jaji Mkeha ameelekeza wajibu maombi wawe wamewasilisha utetezi huo Julai 21, 2025. Shauri litatajwa Julai 22.

Katika shauri hilo, waombaji wanaomba mahakama itamke kuwa: Mosi, wana haki ya uhuru wa kuabudu kama ilivyowekwa wazi na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 kama ilivyowekwa wazi katika Ibara ya 19(1) na (3).

Pili, wana haki ya uhuru wa binafsi kama ilivyowekwa chini ya Ibara ya 15(1) na (2)(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.

Tatu, kitendo cha polisi chini ya maelekezo na amri za mjibu maombi wa pili (IGP) kuwakamata eneo la Ubungo Maji, wilayani Ubungo, Dar es Salaam siku ya Jumapili Juni 29, 2025 walipokuwa wamekusanyika kwa amani na utulivu kwa ajili ya ibada, hakukuwa na sababu ya kisheria na kinakiuka haki zao za uhuru wa kuabudu.

Nne, kwamba askari polisi kwa maelekezo ya IGP kuzuia shughuli zao za ibada, kuwakamata na kuwaweka rumande katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay, Dar es Salaam ni ukiukaji wa haki zao za uhuru wa kuabudu, hivyo ni kinyume cha Katiba.

Tano, kwamba, polisi chini ya maelekezo na amri za mjibu maombi wa pili hawana mamlaka ya Kikatiba chini ya Ibara ya 19(1) na (2) ya Katiba kuzuia kwa nguvu shughuli za kidini za waombaji waliokusanyika kihalali kwa sala za kidini Juni 29, 2025 eneo la Ubungo Maji, wilayani  Ubungo, Dar es Salaam.

Shauri hilo limefunguliwa chini ya hati ya dharura wakiomba usikilizwaji wale ufanyike kwa haraka.

Kibatala anaeleza katika hati hiyo kuwa, usikilizwaji wa shauri hilo ni wa dharura kwa kuwa linagusa haki nyeti ya uhuru wa kuabudu, ambayo waombaji wadai imekiukwa kwa matendo ya mjibu maombi wa pili na itaendelea kuwa hatarini mpaka shauri hilo litakapoamuliwa.

Msingi wa madai waombaji wanadai Ibara ya 19(1) na (2) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 inatoa haki za uhuru wa kuabudu kwa wananchi.

Wanadai kwa maelekezo na amri za IGP walifyatuliwa mabomu ya machozi, kupigwa, kukamatwa na kuwekwa rumande katika Kituo cha Polisi Oysterbay, Dar es Salaam, bila sababu yoyote ya kisheria na  hawajawahi kuonyeshwa amri yoyote ya Mahakama au amri nyingine ya kisheria inayowapa Polisi haki ya kuingilia haki zao za uhuru wa kuabudu.

Related Posts