WAKATI vurugu za mastaa wa Simba kuaga baada ya makubaliano ya pande zote mbili, Rais wa heshima na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, Mohammed ‘Mo’ Dewji amewatuliza mashabiki na wanachama wa Msimbazi na kuahidi neema msimu ujao.
Baadhi ya mastaa wa klabu hiyo, wameshaaga akiwamo Fabrice Ngoma, Valentino Nouma, Awesu Awesu na Augustine Okejepha hali iliyowapa presha mashabiki, lakini Mo Dewji amevunja ukimya na kutoa kauli ya kibabe kuwatuliza Wanamsimbazi.
Kupitia ukurasa wa mtandao wa kijamii Instagram, Mo Dewji ameandika; “Najua mioyo yenu imebeba maswali mengi. Kama Rais wenu, msione nimekaa kimya wakati tumepitia kipindi hiki kigumu. Kupambania Simba ni wajibu wangu.”
Ameongeza; “Huu siyo wakati wa lawama ni wakati wa kusimama imara, kuwa kitu kimoja, na kuchukua hatua sahihi za kuleta mabadiliko chanya.”
Amesema katika siku chache zijazo, atazingumza na mashabiki na wanachama moja kwa moja huku akiweka wazi kuwa kuna kazi kubwa inaendelea, na kuna matumaini ya kweli.
“Simba haijapotea.Tumekuwa kwenye kipindi cha mpito tumejenga kikosi kipya, tumeimarisha benchi la ufundi, na tumeweka msingi wa mwelekeo mpya.Msimu huu tumefika mbali zaidi ya matarajio, na msimu ujao tunarudi kwa nguvu mpya.” Ameandika.
Pia amewaomba mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kuendelea kuwa wavumilivu akiwahakikishia kuwa wanatarajia kufanya marekebisho makubwa.
“Tuendelee kusimama pamoja kama familia moja. Mbele yetu kuna mwanga. Na kwa pamoja, tutarudi tukiwa imara zaidi, wenye njaa zaidi, na wa kishujaa zaidi.”
Simba inayonolewa na kocha Fadlu Davids msimu ulioisha hivi karibuni ilimaliza katika nafasi ya pili katika Ligi Kuu, huku ikifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.