Tanga. Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT Wazalendo, Abdul Nondo amesema hakuna namna Ulaya na Jumuiya ya Kimataifa itafikiri kutoitambua Serikali yoyote, iwapo itaona maslahi yao yanatimizwa.
Kauli ya Nondo inajibu msimamo wa Chadema wa kuwataka wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali kupitia chama hicho, watafute saini milioni 15 za wananchi kupinga mifumo ya uchaguzi nchini.
Kufanya hivyo, kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche kutapeleka ujumbe kwa jumuiya ya kimataifa kuhusu changamoto zilizopo nchini, na kwamba hatimaye jumuiya hiyo haitaitambua Serikali iliyopo madarakani.
Kinachoelezwa na Nondo ni mwendelezo wa majibizano ya vyama hivyo, vikitofautiana misimamo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, Chadema ikilenga kuuzuia huku ACT Wazalendo ikiapa kushiriki na kulinda kura zake.
Nondo amesema hayo leo, Ijumaa Julai 11, 2025, alipozungumza katika kikao cha ndani na viongozi wa chama hicho ngazi ya kata na Jimbo la Mkinga, ikiwa ni sehemu ya ratiba ya ziara ya Operesheni Majimaji, Linda Kura.
Katika kauli yake hiyo, amesema hatua ya kufikiri jumuiya ya kimataifa inaweza kutoitambua Serikali kutokana na uvunjwaji wa haki ni kujidanganya.
Uhalisia ni kile alichoeleza kuwa, jumuiya ya kimataifa haiingilii au kutoitambua Serikali yoyote iwapo itaona maslahi yake yanatimizwa.
“Hakuna namna jumuiya ya kimataifa inaweza kutoitambua Serikali iwapo maslahi yao yanatimizwa. Tusijidanganye, kama unataka haki jawabu lake ni kujipambania,” amesema.
Katika hoja hiyo, Nondo amesema suala la changamoto za kisheria katika michakato ya uchaguzi halipaswi kukabiliwa kwa kuacha kushiriki mchakato huo, bali kwa kushiriki na kuwa na mbinu za mapambano.
Ameeleza uzoefu unaonesha nyakati zote ambazo wapinzani wamesusa kushiriki uchaguzi, watawala waliendelea na mchakato na kujichukulia ushindi katika viti vyote na kuitumia fursa hiyo kutunga sheria kandamizi.
Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Issihaka Mchinjita amesema kila mtazamo uliopo kuhusu uchaguzi una mantiki na unatokana na watu kuchoshwa na mifumo iliyopo.
Amesema mifumo inayomnyima haki mwananchi kuamua kiongozi anayemtaka, imefanya miongoni mwa wanasiasa waivuke na mikakati tofauti kuelekea uchaguzi ikiwemo kupanga kuuzuia na wengine kulinda kura.
Katika mazingira hayo, amesema kuacha kushiriki uchaguzi inaweza isiwe mbinu sahihi kwa sababu uzoefu unaonesha anguko zaidi kuliko mafanikio.
Kwa sababu hiyo, amesema ACT Wazalendo imeamua kuja na mkakati tofauti wa kushiriki uchaguzi na kulinda kura.
“Kwa kuwa tuna uchaguzi wenye changamoto hizo, jambo muhimu ni kujadiliana kwa namna gani tunajipanga kushinda,” amesema Mchinjita.