Lissu aibuka kivingine, Mahakama ikitupa shauri lake

Dar es Salaam. Wakati Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam ikitupilia mbali maombi ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, kiongozi huyo leo Julai 11, 2025 amefiki mahakamani kivingine.

Tofauti na alivyozoeleka kuingia mahakamani akiwa amevaa fulana yenye ujumbe wa No reforms No election, leo ameingia akiwa na fulana yenye ujumbe ‘One love, One heart’ ambao ni wimbo wa mwanamuziki maarufu wa reggae dunia, Bob Marley.

Tangu kuanza kwa shauri hilo Lissu amekuwa akifika mahakamani akiwa amevaa fulana yenye ujumbe wa No reforms No election akikazia msimamo wa chama chake wa kupinga uchaguzi kama hakuna marekebisho ya sheria.


Japokuwa hakueleza sababu za kuvaa fulana yenye ujumbe wa One love One heart, lakini Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, John Heche ameieleza Mwananchi kuwa wamedhamiria kupeleka kwa Taifa ujumbe kuwa: “Wanahitaji nchi yenye upendo na isiyo na visasi.”

Bob Marley aliandika wimbo huo kwa mara ya kwanza mwaka 1965 akaurudia wakati wa machafuko ya uchaguzi nchini Jamaica Desemba, 1976 wakati Taifa hilo lilipokuwa limegawanyika kati ya Chama cha Kitaifa cha Watu kilichoongozwa na Michael Manley na Chama cha Kazi cha Jamaica kilichoongozwa na Edward Seaga.

Wimbo huo unatambulika kwa wito wa amani, hata mwanasiasa nguli wa Kenya Raila Odinga amekuwa akiutumia kwenye kampeni zake za uchaguzi kuhimiza amani na upendo.

Wimbo wa One love One heart umekuwa ukijulikana kwa kubeba ujumbe wa umoja na amani.

“One Love mara nyingi huonekana kuwa wimbo maarufu zaidi wa Bob Marley. Upendo ndiyo jibu la matatizo yote,” amenukuliwa Stephen Marley, mtoto wa Bob kwenye kitabu chake cha Anthems we love.


Wimbo huo una ujumbe mzito wa kisiasa unaozungumzia amani na mshikamano wa pamoja.

Kwa mujibu wa Stephen wimbo huo una wito wa umoja ukisema: “Tukutane pamoja na tujisikie vizuri.”

Ni wimbo unaoakisi muktadha wa siasa, hasa katika jamii zinazokumbwa na mgawanyiko, machafuko au ukandamizaji.

Heche amesema ujumbe wa Lissu kupitia fulana unajieleza kama alivyoimba Bob Marley.

“Ujumbe unajieleza, ujumbe wa Mwenyekiti kwa Watanzania ni kwamba tunahitaji nchi yenye upendo na isiyo na visasi. Wimbo wa Bob Marley tumekuwa tukiutumia kwenye ziara zetu,” amesema na kuongeza:

“Kuvaa kwake leo fulana yenye ujumbe wa One love One heart haimaanishi tumebadilisha msimamo wetu wa No reforms No Election.”

Heche amesema: “One love ni zaidi ya kutaka mshikamano, ni wito wa kututaka kuamka na kujikomboa kutoka kwenye mifumo mibaya inayoendelea kutufanya mateka.”

Mahakama imetupilia mbali maombi hayo kutokana na kukiuka sheria.

Lissu alifungua shauri la maombi mahakamani hapo akiiomba mahakama iitishe mwenendo wa Juni 2, 2025 wa kesi ya jinai inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Katika mahakama hiyo, Lissu alikuwa akiomba nafuu sita, ikiwamo kutengua amri ya Mahakama ya Kisutu kuahirisha kesi ya msingi, Juni 2, 2025.

Jamhuri iliweka pingamizi la awali ikiiomba mahakama ilitupilie mbali shauri hilo bila kulisikiliza ikitoa sababu tatu. Shauri hilo lilisikilizwa Juni 27 na Jaji Elizabeth Mkwizu.

Katika uamuzi wake leo Julai 11, Jaji Mkwizu ametupilia mbali maombi ya Lissu kwa kuzingatia sababu moja pekee ya pingamizi la Jamhuri akisema inatosha kuyaondoa mahakamani.

Sababu ambayo mahakama imekubaliana nayo ni maombi hayo kuwasilishwa kinyume cha sheria.

Lissu aliwasilisha maombi hayo chini ya vifungu vya 372(2) na 392A vya Sheria ya Mwenendo wa Mashtaka (CPA).

Jamhuri katika pingamizi ilidai maombi hayo yanakiuka kifungu cha 372(1) na (2) cha CPA.

Wakati wa usikilizwaji wa pingamizi hilo jopo la mawakili wa Serikali lilifafanua kuwa, uamuzi ambao Lissu anaupinga (amri ya Mahakama ya Kisutu ya Juni 2) kuahirisha usikilizwaji wa kesi ya msingi haukatiwi rufaa wala kufanyiwa mapitio.

Walifafanua kuwa hiyo ni amri ambayo haihitimishi shauri la msingi, ambayo kwa mujibu wa kifungu hicho haifanyiwi mapitio.

Wakijibu hoja hiyo, jopo la mawakili wa Lissu pamoja na mambo mengine walipinga wakidai kifungu hicho kinaipa mahakama mamlaka hayo, wakirejea kesi mbalimbali zilizowahi kuamuliwa na Mahakama ya Rufani.

Pia walidai katika maombi hayo hawapingi amri ya Mahakama ya Kisutu kuahirisha kesi bali kwamba walikuwa wanahoji kitendo cha mahakama hiyo kukataa hoja yao ya kuiomba iwasilishe Mahakama Kuu hoja ya ukatiba wa kifungu cha 188 cha CPA ambacho upande wa mashtaka ulikitumia kuomba ahirisho.

Jaji Mkwizu katika uamuzi amesema miongoni mwa nafuu sita alizoziomba Lissu ni kupitia amri ya Mahakama ya Kisutu ya ahirisho la kesi ya msingi ya Juni 2, 2025.

Jaji Mkwizu amesema amri iliyokuwa inalalamikiwa na Lissu haimalizi shauri, hivyo ni kinyume cha kifungu cha 372(2) cha CPA.

“Kwa hiyo sababu ya pili ya pingamizi inakubaliwa. Shauri hili linatupiliwa mbali,” amesema Jaji Mkwizu.

Amesema sababu hiyo pekee inatosha kuliondoa mahakamani shauri lote.

Jaji amesema iwapo mwombaji ataona inafaa anaweza kufungua upya maombi yake kwa mujibu wa sheria.

Baada ya uamuzi kutolewa na watu kutoka katika ukumbi namba moja uliopo mahakamani hapo, kulitokea mvutano kati ya askari Magereza, Lissu na mawakili wake.

Mvutano huo ni baada ya Lissu kutaka kuzungumza na mawakili lakini askari Magereza waliokuwa wanamlinda walimueleza muda umekwisha anatakiwa kurudishwa rumande.

Baada ya sekunde kadhaa za mvutano huo, askari waliwaeleza mawakili wa Lissu kama wana jambo wanataka kuzungumza naye wafuate tararibu za kisheria.

Hata hivyo, Lissu alikubaliana na maelezo ya askari akaondolewa kizimbani akiwa chini ya ulinzi wao hadi kwenye gari, kisha wakaondoka kuelekea mahabusu ya Gereza la Ukonga.

Lissu anakabiliwa na kesi ya kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni katika Mahakama ya Kisutu, inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini.

Kesi hiyo ilikuwa imepangwa kuanza kusikilizwa ushahidi Juni 2, 2025 lakini mahakama hiyo iliahirisha usikilizwaji kutokana na ombi ya upande wa mashtaka la kutaka ahirisho kusubiri shauri la maombi madogo ya kuwalinda mashahidi katika kesi hiyo.

Lissu hakuridhika na uamuzi huo, ndipo akafungua shauri la maombi ya mapitio Mahakama Kuu akiiomba iitishe jalada la kesi hiyo ya msingi na kupitia mwenendo wa siku hiyo kujiridhisha na usahihi na uhalali wake

Katika kesi hiyo Lissu anakabiliwa na mashtaka matatu ya kuchapisha taarifa za uongo katika mtandao wa Youtube kinyume cha Sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015, kifungu cha 16.


Katika mashtaka hayo  anadaiwa kumhusisha Rais wa Jamhuri ya Muungamo wa Tanzania na kuenguliwa wagombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika maeneo mbalimbali wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024.

Pia anadaiwa kuwatuhumu askari polisi kuhusika katika wizi wa kura kupitia vibegi na majaji kutokutenda haki kwa madai ya kutaka wapate uteuzi wa Rais kuwa majaji wa Mahakama ya Rufani.

Anadaiwa kutenda makosa hayo Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam, kwa nia ya kulaghai umma.

Nyongeza na Baraka Loshilaa

Related Posts