Dar es Salaam. Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Stephen Nindi amezitaka nchi za Afrika kushirikiana na mataifa mengine kutengeneza suluhisho la utoshelevu wa chakula na kutafuta fursa za biashara.
Kiongozi huyo amesema mustakabali wa kilimo cha Afrika utategemea Waafrika huku akitaja sekta hiyo kuwa inachukua nafasi muhimu katika uchumi.
Kiongozi huyo wa Wizara ya Kilimo ameyasema hayo leo Julai 11, 2015 wakati akifungua mkutano wa ushirikiano wa nchi za kusini kwa kusini (SSTC) kwa ajili ya mageuzi ya kilimo barani Afrika lengo likiwa ni kuimarisha ushirikiano kati ya nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Akifungua mkutano huo ulioandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO), Nindi amesema ushirikiano baina ya mataifa ya kusini kwa kusini unatoa fursa kubwa kwa nchi za Afrika kubadilishana maarifa, rasilimali na teknolojia ili kufikia malengo ya maendeleo ya kilimo.
“Tunataka si tu kuwa na uwezo wa kujilisha, bali pia kuhakikisha uhuru wa chakula, ustahimilivu wa chakula na uunganishaji wa biashara katika maeneo ya kanda. Tunataka Afrika iwe na uwezo wa kujilisha yenyewe na kuwa na uhuru wa chakula na mtandao wa biashara,” amesema.
Katika hatua hiyo, Nindi amesema mikakati ya Tanzania katika kukuza sekta ya kilimo kufikia 2030 ni kuongeza mchango wa sekta hiyo katika Pato la Taifa kutoka asilimia 5 hadi 10, uzalishaji wa kwa asilimia 50, mapato ya wakulima wadogo kwa asilimia 25 na kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno.
Akieleza mafanikio yaliyopatikana sekta ya kilimo nchini, Nindi amesema uzalishaji wa chakula kutoka tani milioni 17.7 hadi tani milioni 23.7.
Mwakilishi Mkuu wa FAO Kanda ya Afrika, Habebe Haile amesema ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya kilimo ni muhimu kwa kuhakikisha usalama wa chakula na maendeleo ya kilimo barani Afrika.
Haile amesema ushirikiano wa kusini kwa kusini (South-South Cooperation) ni chombo muhimu katika kufanikisha mageuzi ya kilimo na kuhakikisha usalama wa chakula barani Afrika.
Amesisitiza ushirikiano huo unachangia kuboresha kilimo, hasa katika nyanja za uzalishaji wa chakula, utekelezaji wa mifumo endelevu ya kilimo na ustahimilivu wa chakula.
“Afrika imekuwa mtetezi mkuu wa mfano wa ushirikiano wa Kusini kwa Kusini, ambapo nchi za Afrika hushirikiana na kujifunza kutoka kwa nchi nyingine ambazo zimefanikiwa,” amesema Haile.
Ameongeza kuwa ili kufikia malengo ya FAO ya kuwa na kilimo cha kisasa, chakula cha kutosha, na mazingira bora, ni muhimu kupima matokeo ya miradi ili kuthibitisha thamani yake na kupata uwekezaji zaidi.
Mkurugenzi wa South South Triangular Cooperation Division (PST), Anping Ye amesisitiza kwamba ni muhimu kwa nchi za kusini mwa Afrika kuongeza uzalishaji wa kilimo ili kuendana na mwenendo wa ukuaji wa idadi ya watu unaoshuhudiwa kila siku.
“Kwa sasa, idadi ya watu inaongezeka kwa kasi, na ni lazima tuhakikishe kwamba uzalishaji wa mazao unakua ili kukidhi mahitaji ya chakula. Hii ni changamoto lakini pia ni fursa kwa wakulima na wawekezaji kuwekeza zaidi katika kilimo cha kisasa,” amesema.