Dar es Salaam. Biashara kati ya India na Tanzania imeongezeka hadi kufikia Sh20.64 trilioni mwaka 2024, kutoka Sh20.13 trilioni mwaka uliotangulia huku ikiwa kinara kwa uwekezaji nchini kwa miaka mitano mfululizo.
Kwa mujibu wa Balozi wa India nchini Tanzania, Bishwadip Dey, ongezeko hilo limetokana na kuimarika kwa uhusiano wa pande mbili na sera bora za uwekezaji.
Akizungumza katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) wakati wa maadhimisho ya Siku ya Haryana, Day amesema biashara kati ya mataifa hayo mawili imeongezeka kwa Dola za Marekani 700 milioni (Sh1.8 trilioni) ndani ya kipindi cha miaka miwili ya 2022/23 na 2023/24.
“Tuna uhusiano imara katika sekta mbalimbali uchumi, siasa, afya na elimu na tumeshuhudia maendeleo makubwa ya ukuaji wa mazingira ya biashara Tanzania ambayo yamekuwa ya kuvutia zaidi, ndiyo maana wawekezaji kutoka jimbo la Haryana wamefika hapa kutafuta fursa,” amesema.
Ushirikiano huo wa kiuchumi unaoendelea kukua ni matokeo ya juhudi thabiti za kidiplomasia.
Mwaka 2016, Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi alitembelea Tanzania na mwaka 2023, Rais Samia Suluhu Hassan alifanya ziara ya kurudisha mkono nchini India.

Ziara hizi za viongozi wa juu zimetajwa kuleta mafanikio katika sekta kama uwekezaji, biashara, na elimu.
Akifungua maadhimisho ya Siku ya India, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza), Giliad Teri amesema India imekuwa kinara wa uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDI) nchini Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.
“Tanzania inakaribisha wawekezaji kutoka Haryana na maeneo mengine. Kuna fursa nyingi za uwekezaji katika sekta mbalimbali, na sisi Tiseza tuko tayari kutoa msaada wote unaohitajika kufanikisha miradi yao,” amesema.
Teri aliwahimiza wajumbe waliotembelea nchini kutumia maonesho haya kama jukwaa la kujenga ushirikiano na wafanyabiashara wa hapa nchini pamoja na kushirikiana katika miradi ya pamoja.
“Uhusiano kati ya nchi zetu mbili ni wa muda mrefu na wenye mafanikio. Kwa kuendeleza ushirikiano huu, tunatarajia biashara kuongezeka zaidi mwaka ujao,” ameongeza.
Wakati huo huo, jimbo la Haryana nchini India limeonyesha nia thabiti ya kuwekeza nchini Tanzania hasa katika sekta za kilimo, teknolojia, na ardhi/mali isiyohamishika.
Wawekezaji wa Kihindi ambao tayari wanafanya biashara nchini Tanzania walishiriki uzoefu wao, wakihamasisha wengine kutoka Haryana kufuata nyayo zao.
Mmoja wa wawekezaji hao, Samrat Chanana ameielezea Tanzania kama nchi inayokaribisha watu na yenye mazingira mazuri kwa uwekezaji wa muda mrefu.
“Ninaishi Tanzania kama nipo nyumbani. Mazingira ni rafiki kwa biashara na ni ya amani na nawashauri wafanyabiashara wenzangu kutoka Haryana waje kuwekeza hapa,” amesema.
Chanana alisisitiza juu ya uwazi wa Tanzania kwa wawekezaji wa kimataifa na utayari wake wa kukumbatia maendeleo ya kiteknolojia.
“Watanzania wanapokea teknolojia mpya kwa haraka. Ndani ya miaka mitano ijayo, nchi hii ina uwezo wa kuwa moja ya mataifa yaliyoendelea zaidi.”
Ameongeza kuwa japokuwa alifika nchini Tanzania bila kuwa na mawasiliano yoyote ya karibu, aliweza kujenga uhusiano imara na kufanikiwa kwa haraka.
“Wawekezaji wa Kihindi hawapaswi kuwa na hofu ya kupoteza mitaji yao hapa. Kinyume chake, wanaweza kunufaika kwa kiwango kikubwa,” amesema.
Wawekezaji pia walitoa wito wa kuanzishwa kwa makubaliano ya biashara huru kati ya India na Tanzania, wakisema mkataba huo utaongeza fursa za kuuza bidhaa nje na kusaidia malengo ya uwekezaji wa muda mrefu.