Dodoma. Wakati serikali na wadau wa afya wakiendelea kutoa elimu ya afya kwa wananchi namna ya kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, Mkoa wa Dodoma umetwajwa kuwa kinara wa magonjwa matatu ambayo ni macho, magonjwa ya akili na selimundu.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na wizara ya afya kwa kushirikiana na Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma mwaka 2024 kuona hali ya tatizo la macho ilionyesha kuwa asilimia 4.7 ya wakazi wa mkoa huo wana ulemavu wa kutokuona.
Aidha asilimia 80 ya watu hao walikuwa na uwezekano wa kupona macho lakini kutokana na kutokuwa na elimu ya matibabu ya macho waliishia kuwa vipofu asilimia 55 kati yao ni wanawake.
Pia asilimia 20 ya wakazi wa mkoa wa Dodoma wana matatizo mengine ya macho ikiwemo uoni hafifu na kutokuona karibu.
Akizungumza na Mwananchi leo ijumaa Julai 11,2025 Jijini Dodoma, Ofisa kutoka mpango wa Taifa wa huduma za macho wa wizara ya Afya, Dk Eunice Kamnde amesema mkoa wa huo ndiyo unaoongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi wanaosumbuliwa na ugonjwa wa macho ukifuatiwa na mikoa mingine ambayo ina kiwango kidogo.
Amesema sababu za watu kupata upofu ni kuwa na mtoto wa jicho, umri mkubwa na ugonjwa wa kisukari, pazia la jicho, shinikizo la jicho, makovu kwenye kioo cha jicho uliotokana na sababu mbalimbali ikiwemo ajali na ulemavu wa kutokuona tangu utotoni.
“Tunashauri ili kujikinga na ulemavu wa kutokuona mtoto achunguzwe macho na wataalam tangu siku anayozaliwa hadi anapofikisha umri wa miaka mitano kila anapokwenda kliniki ili akigundulika kuwa na tatizo lolote aweze kusaidiwa na wataalam kabla hajafikia hatua ya kutokuona kabisa,” amesema Dk Kamnde.
Amesema kwa takwimu za kitaifa inaonyesha takribani watu milioni 2.4 wana ulemavu wa kutokuona au upungufu wa kutokuona ambao ni sawa na asilimia moja ya Watanzania wote.
Dk Kamnde ameshauri watu kulinda afya ya macho kwa kujiepusha kufanya vitu vinavyohatarisha afya hiyo kwa kutotumia vifaa vya kieletroniki kwa muda mrefu kama vile simu za mkononi, kompyuta na runinga.
“Pia ili kujenga uwezo wa watoto kuona wazazi wanashauriwa kuwaacha watoto watumie muda mrefu kucheza nje ya mazingira ya nyumbani ili kuwawezesha macho yao kuangalia mbali zaidi kuliko kuwafungia ndani na kuchezea vifaa vya kieletroniki ambavyo havijengi uwezo wa macho kuona mbali,” amesema.
Kwa upande wa daktari bingwa wa magonjwa ya akili kutoka hospitali ya Taifa ya magonjwa ya akili Mirembe, Dk Sadick Mandali amesema wagonjwa wengi wa akili wanaopokelewa kwenye hospitali hiyo ni kutoka mkoa wa Dodoma ikifuatiwa na mikoa ya Singida, Morogoro, Manyara, Dar es salaam, Iringa, Tabora, Arusha, Tanga, Shinyanga, Mbeya na Kilimanjaro.
Ametaja sababu kubwa ya watu kupata magonjwa ya akili ni kuugua ugonjwa wa kifafa, usonji na matumizi ya madawa ya kulevya aina ya heroin, bangi na pombe kupita kiasi.
Amesema asilimia 31 ya wagonjwa wanaopokelewa kwenye hospitali hiyo wana matatizo ya akili, asilimia moja wanahitaji huduma za kisaikolojia kutokana na changamoto mbalimbali wanazozipitia na asilimia nne ni makundi ya vijana na watoto ambao wanafikishwa kupata matibabu.
“Magonjwa yanayoongoza ni sonona, kuchanganyikiwa, kiwewe, kifafa na matumizi ya dawa za kulevya, ulevi kupitiliza na wale ambao walipata changamoto za kuugua mara kwa mara wakati wa utoto kwa hiyo inafika mahali wanapata magonjwa ya akili.” Amesema Dk Mandali.
Dk Mandali amesema hivi sasa hospitali hiyo imejikita kutoa elimu zaidi kwa jamii kuhusu magonjwa ya akili badala ya kutibu hali iliyopunguza msongamano kwenye wodi za wagonjwa na hivyo wagonjwa wengi kutibiwa wakitokea nyumbani na kurudi.
Amesema mbali na hospitali hiyo kutoa huduma za matibabu ya magonjwa ya akili lakini pia wana kitengo cha Isanga ambacho kinahudumia watu waliofanya makosa kisheria na kugundulika kuwa wakati wanafanya makosa hayo walikuwa na matatizo ya akili ambao jumla yao wapo 350.
Amesema kituo kingine ni cha waraibu wa madawa ya kulevya aina ya heroine ambao wanahifadhiwa kwenye kituo kilichopo Image Jijini Dodoma ambao wapo 500 na 200 kati yao wapo kwenye dozi ya Methadone ambapo idadi kubwa ni kutoka mkoani Dodoma.
Kwa upande wake mtalaam wa magonjwa ya selimundu (Sickle cell) kutoka Wizara ya Afya, Dk Deogratias Soka amesema Mkoa wa Dodoma pia unaongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi wa selimundu kwa kuwa unapatikana kwenye ukanda wa mikoa yenye maabukizi makubwa ya ugonjwa wa malaria.
Amesema ugonjwa wa selimundu siyo wa kuambukiza bali unatokana na watu wenye vinasaba vya ugonjwa huo ambapo endapo baba na mama wana vinasaba vya ugonjwa huo wana uwezekano mkubwa wa kupata mtoto mwenye ugonjwa wa selimundu.
Dk Soka amesema mikoa yenye hatari ya kupata wagonjwa wa selimundu ni mikoa ya Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kati na kanda ya Pwani kutokana na mikoa hiyo kuwa na mbu wengi wanaoeneza ugonjwa wa malaria.
Hata hivyo ili kupunguza idadi ya wagonjwa wa selimundu daktari huyo ameshauri wanandoa kupima vinasaba kabla ya kuoana ili kama wote wana vinasaba vya ugonjwa huo wasioane kwani wanakuwa na uwezekano mkubwa wa kuzaa watoto wenye ugonjwa wa selimundu ambao ni hatari na unasababisha vifo vya watoto wenye ugonjwa huo kabla ya kufikisha miaka miwili.
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za kinga kutoka Wizara ya Afya, Dk Otilia Gowele amesema ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza nchini ni tishio kwani magonjwa hayo yanachangia asilimia 35 ya vifo vyote vinavyotokea nchini ikiwa ni wastani wa kifo kimoja kati ya vifo vitatu vinavyotokea kila siku.
Amesema hiyo inatokana na watu kutozingatia mazoezi na lishe, kutumia mafuta mengi yasiyo ya lazima, unywaji pombe kupindukia na uvutaji wa sigara.
Amesema kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Hospitali ya Taifa ya magonjwa ya akili Mirembe imeonyesha kuwa asilimia 10 ya Watanzania wana matatizo ya afya ya akili hali ambayo siyo nzuri kwa ustawi wa Taifa.
Amewataka Watanzania kuzingatia mazoezi, kunywa maji kwa wingi, kulala kwa masaa nane kila siku, kupunguza msongo wa mawazo, kuacha uvutaji wa sigara na kupima afya mara kwa mara ili kama watagundulika kuwa matatizo yatibiwe mapema.