Tanzania, China zabainisha mikakati kuimarisha elimu ya ufundi stadi

Dar es Salaam. Tanzania na China zimeeleza mikakati ya kuendelea kuimarisha ushirikiano baina yao katika maeneo matatu ikiwemo ubadilishanaji wa wakufunzi, wanafunzi na kuimarisha elimu ya kidigitali.

Katika elimu ya kidigitali, China imesema itashirikiana na Tanzania kuandaa vitabu vya kidigitali vyenye lugha mbalimbali pamoja na kuhamasisha matumizi ya teknolojia hizo.

Eneo la tatu la ushirikiano ni taasisi za China kushirikiana na kampuni za Tanzania kukuza vipaji katika matumizi ya teknolojia kuwezesha matumizi ya nishati safi kupunguza hewa ya ukaa kabla yam waka 2030.

Mambo hayo yamebainishwa leo Julai 11, 2025 na wawakilishi wa Tanzania na China katika semina iliyoratibiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Nactvet).

Akifungua semina hiyo ya tano ya kuimarisha ushirikiano wa elimu kati ya China na Afrika katika nyanja za elimu ya ufundi stadi (TVET), Mkurugenzi wa Elimu na Ufundi Stadi kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Dk Fredrick Salukele amesema ushirikiano na China ni namna ya kupeleka elimu ya Tanzania mbele.

“Sera yetu ya Elimu iliyofanyiwa maboresho 2023 inasisitiza elimu na ujuzi wenzetu kutoka Sichuan Provincial Committee (Kamati ya Mkoa wa Sichuan ya Chama cha Kikomunisti cha China—CCP) wameahidi kuendelea kushirikiana nasi kubadilishana wanafunzi na walimu kwenda kupata mafunzo.

“Dunia inaelekea kwenye akili mnemba, hivyo wameahidi tutashirikiana nao katika utengenezaji wa mitambo ya ufundishaji na ujifunzaji,” amesema.

Dk Salukele amesema watashirikiana na china katika maandalizi ya mitaa ya ufundi stadi ili ziendane na mahitaji ya soko la dunia.

Kwa upande wake, kiongozi mkuu anayesimamia masuala ya elimu mkoa wa Sichuan, chini ya CCP, Profesa Yu Xiaoqi amesema nchini China, elimu ya ufundi sio chaguo bali ni lazima, lengo kuliletea taifa hilo maendeleo.

“Mafanikio ya elimu ya ufundi nchini China yanaonyesha ujuzi wa vitendo na ubunifu ni msingi wa nguvu kazi imara na ya kisasa, tuna wanafunzi zaidi ya milioni moja katika taasisi za ufundi, hivyo mustakabali wa wafanyakazi wenye ujuzi kwetu ni nguzo yetu imara,” amesema.

Profesa Xiaoqi amesema mikakati ya ushirikiano kati ya China na Tanzania inaonyesha nguvu ya ushirikiano katika ujuzi wa kidijitali na maendeleo ya walimu.

Amesema mabadilishano ya walimu na wanafunzi baina ya nchi hizo mbili huimarisha ujuzi na kuhamasisha kujifunza kwa pande zote, hivyo kuongeza ubora wa elimu ya ufundi baina ya wataalamu wan chi hizo.

Semina hiyo imehusisha wataalamu mbalimbali wa vyuo vya ufundi stadi Tanzania na China lengo kuangalia namna ya kuimarisha ushirikiano katika kuboresha elimu ya ufundi stadi nchini.

Mwenyekiti wa Bodi Nactvet, Bernadetta Ndunguru amesema katika kufanikisha upatikanaji wa ujuzi kwa vijana,Serikali imeanzisha programu ya elimu ya amali.

“Hii inasaidia vijana kujifunza ujuzi zaidi wakati wakiwa shuleni na kuwafanya kuanza kujitengemea na kukuza ubunifu miongoni mwao, sisi kama Nactvet tutaendelea kuhakikisha Watanzania wanapata ujuzi utakaowawezesha kuendana na soko la ajira,” amesema.

Related Posts