AZAM imepania. Baada ya kufanikiwa kumnasa kocha mwenye cv kubwa barani Afrika, Florent Ibenge, kisha kuwanasa kipa Aishi Manula na viungo Himid Mao na Muhsin Malima sambamba na beki Lameck Lawi, mabosi wa klabu hiyo sasa wameamua kufanya fujo isiyoumiza kwa Msimbazi.
Inadaiwa, wakati Simba ikirudi kwa klabu ya AS Union Maniema ya DR Congo ili kutaka kuinasa saini na kiungo mshambuliaji, Agee Basiala, Azam kwa upande mwingine wameamua kutumia turufu ya kuwa na Ibenge, ili kumlainisha nyota huyo kutua kwa matajiri hao kwa kuweka mkwanja wa maana.
Taarifa zinasema kuwa, Azam imetua rasmi Maniema ikimtaka kiungo huyo pamoja na mshambuliaji matata anayekipiga katika klabu hiyo iliyoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliomalizika.
Simba ilitangulia kumtaka Basiala mapema tu, lakini haikufanya maamuzi ya mwisho kisha juzi, ikarudi na dau la Dola 70000 wakimtaka kiungo fundi.
Hata hivyo, wakati Maniema wakiweka ngumu kumuachia kiungo huyo kwa dau hilo, Azam inadaiwa imejitosa jana ikitaka huduma ya Mkongomani huyo msimu ujao.
Inaelezwa kwamba kocha Florent Ibenge, ndiye aliyependekeza usajili wa kiungo huyo anayeweza kucheza nafasi ya kiungo mshambuliaji.
Mbali na Basiala, Azam pia imeonyesha nia ya kumtaka mshambuliaji Japhet Kitambala, aliyesajiliwa Maniema akitokea TP Mazembe ya DR Congo.
Wawili hao, wanatakiwa na Ibenge ambaye ameanza hesabu za kuboresha kikosi chake hicho mara baada ya kuingia mkataba wa mwaka mmoja.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Maniema, Guy Kapya amelithibitishia Mwanaspoti juu ya ujio wa Azam akisema mazungumzo yanaendelea vizuri.
“Tulikuwa na mazungumzo na kiongozi mmoja wa Simba alileta ofa yao akimtaka Agee, lakini bado tulikuwa tunapambana nao, hawakufika tunapotaka,” alisema Kapya.
“Leo (jana) tumepokea ofa nyingine ya Azam kutoka hapo Tanzania, wanamtaka Agee na wanamtaka mchezaji mwingine pia, tunaendelea nao na mazungumzo, ile timu itakayofika ambako tunataka tutafanya nao biashara hakuna tatizo.”
Mwanaspoti iliwahi kuandika kuwa; “Simba ilipewa dau la kumpata kiungo huyo, huku ikitakiwa kumnunua kwa Dola 150,000 (zaidi ya Sh 380 milioni) licha ya wao kuwatoa kiasi walichotoa sasa.”
Lakini kiungo huyo aliwahi kutakiwa na Yanga kabla ya Simba, kama mbadala wa Jean Charles Ahoua kama atatimkia Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, baada ya dili la Feisal Salum ‘Fei Toto’ kutua kwa Wekundu hao kukosa tumaini.
Baada ya msimu kumalizika mastaa waliomaliza mikataba, huku wengine wakipewa mkono wa kwa heri, lakini katika upande wa eneo la kiungo lina vichwa vya maana licha ya Fabrice Ngoma na Awesu Awesu kuaga mapema, kuna Mzamiru Yassin, Jean Charles Ahoua, Debora Mavambo na Augustine Okejepha anayedaiwa aatolewa kwa mkopo au kuuzwa jumla nje ya nchi.