UONGOZI wa Singida Black Stars umevunja mkataba nyota wake wawili wa kigeni kupisha usajili mpya tayari kwa kujiweka witi na msimu mpya wa 2025/26.
Singida iliwavunjia mikataba viungo washambuliaji wawili, Emmanuel Bola Lobota raia wa DR Congo na Mganda Matthew Odongo ambao wameachwa kutokana na kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara katika timu hiyo.
Chanzo cha kuaminika kutoka Singida BS kililiambia Mwanaspoti uongozi ulifikia uamuzi huo ili kufanya sajili nyingine mpya ambazo zitakuwa na tija kutokana na timu hiyo kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao.
“Ni kweli tumevunja mikataba na nyota hao lengo ni kufanya sajili nyingine ambazo zitaleta chachu ya ushindani, msimu ujao tuna nafasi ya uwakilishi kimataifa, hivyo tunataka kuwa na wachezaji ambao watakuwa bora na wataonyesha ushindani.”
Mwanaspoti lilifanya jitihada za kumtafuta Ofisa Habari wa timu hiyo, Hussein Masanza ambaye alithibitisha taarifa hizo ni kweli wamefikia makubaliano ya kuvunja mkataba na wachezaji hao.
“Ni kweli tumefikia makubaliano ya pande zote mbili kuvunja mkataba lengo ni kuona tunafanya sajili nyingine bora tayari kwa ajili ya ushindani kwenye michuano ya ndani na kimataifa tukiwa na nafasi ya uwakilishi wa Kombe la Shirikisho.”
Singida ambayo imefanya maboresho ya benchi la ufundi kwa kumuongeza aliyekuwa kocha wa Yanga, Miguel Gamondi inaendelea na maboresho kwenye usajili wa wachezaji pia na hadi sasa imenasa saini ya beki Kelvin Kijili ambaye amejiunga na timu hiyo kwa mkataba wa miaka miwili.