Uchunguzi wabaini chanzo ndege iliyolipuka, kuua abiria 260

India. Ofisi ya Uchunguzi wa Ajali za Ndege ya India (Aircraft Accident Investigation Bureau) imetoa taarifa ya awali ya uchunguzi ajali ya ndege iliyoua abiria 260 na kuua wengine 19 ardhini leo Jumamosi Julai 12, 2025, ikibainisha kuwa injini za ndege ziliishiwa mafuta muda mfupi baada ya kuruka kisha kulipuka kutokana na hitilafu.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa kuwa marubani wote wawili walichanganyikiwa kuhusu mabadiliko ya mpangilio wa swichi hizo za mafuta, hali iliyosababisha kupungua kwa nguvu za injini muda mfupi baada ya kuruka.


Ndege hiyo ya Air India, aina ya Boeing 787-8 Dreamliner, ilipata ajali Juni 12, 2025 na kuua watu wasiopungua 260, wakiwemo 19 waliokuwa ardhini, katika jiji la Ahmedabad, kaskazini-magharibi mwa India.

Abiria mmoja pekee ndiye aliyenusurika kwenye ajali hiyo, ambayo ni mojawapo ya ajali kubwa za angani kuwahi kutokea nchini humo.

Ndege hiyo ilikuwa imebeba abiria 230: Wahindi 169, Waingereza 53, Wareno saba na Mkanada mmoja, pamoja na wafanyakazi wa ndege 12.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, safari ya ndege hiyo ilidumu takriban sekunde 30 kati ya kuruka na kuanguka. Ilieleza kuwa mara baada ya ndege kufikia kasi ya juu iliyorekodiwa, “swichi za kukatiza mafuta kwa Injini 1 na Injini 2 zilihamishwa kutoka nafasi ya RUN hadi CUTOFF mfululizo ndani ya sekunde moja.”

Ripoti hiyo haikueleza jinsi swichi hizo zilivyoweza kubadilika hadi kwenye nafasi ya cutoff wakati wa safari ya ndege. Uhamishaji wa swichi hizo huruhusu au kukatiza mtiririko wa mafuta kwenda kwenye injini za ndege.

Ripoti ilisema kuwa swichi hizo zilirejeshwa katika nafasi ya run, lakini ndege haikuweza kupata nguvu kwa haraka ya kutosha kuzuia kushuka kwake baada ya kuanza kupoteza mwinuko.

“Mmoja wa marubani alirusha ujumbe wa dharura: ‘MAYDAY MAYDAY MAYDAY,’” ripoti ilisema. Pia ilionyesha kuwepo kwa mkanganyiko ndani ya chumba cha rubani muda mfupi kabla ya ajali. Katika sekunde za mwisho za ndege hiyo, rubani mmoja alisikika kwenye kinasa sauti cha chumba cha rubani akimuuliza mwenzake kwa nini alikatiza mafuta.


“Rubani mwingine alijibu kuwa hakufanya hivyo,” ripoti ilisema. Ripoti hiyo ya awali haikutoa mapendekezo yoyote kwa kampuni ya Boeing.

Air India katika taarifa yake ilisema inashirikiana kikamilifu na mamlaka zinazochunguza ajali hiyo. “Air India inafanya kazi kwa karibu na wadau, wakiwemo wasimamizi wa sekta,” taarifa hiyo ilisema.

“Tunaendelea kushirikiana kikamilifu na AAIB na mamlaka nyingine kadri uchunguzi unavyoendelea.”

Vifaa vya kuhifadhi kumbukumbu vya ndege hiyo vinavyounganisha kinasa sauti cha chumba cha rubani na kinasa data cha safari vilipatikana siku chache baada ya ajali na baadaye kuchambuliwa nchini India.

Mamlaka za India pia ziliagiza ukaguzi wa kina kwa ndege zote za Dreamliner 787 zinazomilikiwa na Air India ili kuzuia matukio ya aina hiyo kujirudia. Air India ina jumla ya ndege 33 za Dreamliner katika meli yake ya usafiri.

Related Posts