Jinsi askari polisi wanne walivyonusurika kunyongwa

Dar es Salaam. Katika sehemu hii ya mapitio ya hukumu ya kesi ya mauaji iliyokuwa ikiwakabili maofisa saba wa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara, inajibu kiini cha pili iwapo washtakiwa ndio waliohusika na kifo cha Mussa Hamis.

Washtakiwa katika kesi hii ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Mtwara (OC-CID), Mrakibu wa Polisi (SP) Gilbert Kalanje na aliyekuwa Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara (OCS), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Charles Onyango.

Wengine ni aliyekuwa Mkuu wa Intelijensia wa Wilaya ya Mtwara (DCIO), ASP Nicholous Kisinza, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Marco Chigingozi; Mkaguzi wa Polisi, John Msuya; Inspekta Msaidizi Shirazi Mkupa na Koplo Salim Mbalu.

Wote walishtakiwa kwa kosa la kumuua kwa kukusudia mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis, Mkazi wa Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi Januari 5, 2022, ndani ya Kituo cha Polisi Mitengo wilayani Mtwara.

Katika sehemu iliyopita, Jaji Hamidu Mwanga kutoka Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, alihitimisha ufafanuzi wa ushiriki wa washtakiwa aliowatenga katika makundi matatu kulingana na majukumu yao katika uchunguzi wa tuhuma alizozushiwa Mussa na hatimaye mauaji yake.

Katika simulizi ya leo, Jaji Mwanga anahitimisha uchambuzi wa ushahidi unaohitimisha kwa kuwaachia huru kundi la kwanza la washtakiwa wanne na anagusia ushahidi na utetezi dhidi ya kundi la pili la washtakiwa hao.

Jaji Mwanga alisema: “Baada ya kubaini nafasi ya kila mshtakiwa katika kesi hii kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa, sasa ni wakati muafaka kuona kama wao ndio waliomuua Mussa Hamis ama la.”

“Tukianza na washtakiwa wa nne, sita na saba, ni wazi walichukua hatua kwa msingi wa taarifa potofu zilizotolewa na washtakiwa wa kwanza, wa pili na wa tatu. Kwamba marehemu (Mussa) alikuwa jambazi sugu aliyekuwa akiiba pikipiki katika mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara,” anasema na kuongeza:

“Kwa mujibu wa shahidi wa tatu wa Jamhuri, jalada (RB) la kesi iliyodaiwa ilihusu kosa la wizi wa kuvunja nyumba. Hata hivyo, washtakiwa hawa wanaonekana kutekeleza majukumu yao, yaani upekuzi, ukamataji na kumshikilia marehemu kama mtuhumiwa, kwa mujibu wa sheria.”

Anasema: “Walimkabidhi marehemu (Mussa), mikononi mwa mshtakiwa wa kwanza na wa pili, pamoja na vielelezo akiwa bado na afya njema.”

“Kwa msingi huo, ushahidi wa upande wa mashtaka hauonyeshi uhusiano wowote au ushiriki wa washtakiwa hawa katika tukio la mauaji lililotokea Januari 5, 2022, katika Kituo cha Polisi Mitengo,” anasema Jaji na kuongeza:

“Hakuna ushahidi unaoonyesha walikuwa na nia ya pamoja ya kumuua marehemu (Mussa). Katika uchunguzi wao walikamata mali za marehemu na kuzirekodi katika kielelezo PE1. Hivyo basi, ninaamini hawakushiriki katika mauaji ya Mussa.”

Anasema: “Kwa hiyo, kiini cha pili, kama mshtakiwa wa nne, wa sita na wa saba walimuua Mussa Hamis, kinajibiwa kwa kukanusha.”

Mshtakiwa wa tatu chupuchupu

Katika uchambuzi huo, Jaji anasema: “Kwa mshtakiwa wa tatu, ndiye aliyedai kuwa na taarifa kuhusu upekuzi na ukamataji uliofanyika Sadina Lodge na Kijiji cha Luponda na matokeo ya uchunguzi huo.”

“Kinachonitia wasiwasi ni kwamba, hakufichua kuwapo mlalamikaji ambaye alidai kuibiwa pikipiki huko Dar es Salaam, jambo ambalo lingehalalisha taarifa alizotumia kumkamata marehemu (Mussa),” anasema na kuongeza:

“Tena, hakuna jalada la kesi lililofunguliwa dhidi ya marehemu (Mussa). Hadi alipotoa utetezi wake, hakuonyesha uhalisia wa taarifa za kiintelijensia alizopokea. Mwenendo huo unanieleza kuwa taarifa zake za kiintelijensia kuhusu marehemu (Mussa) kuiba pikipiki zilikuwa za uongo kabisa.”

Anasema: “Huenda alianzisha mpango wa kupora mali za marehemu kwa kushirikiana na mshtakiwa wa kwanza na wa pili. Hata hivyo, hakuna mashtaka ya wizi wa mali za marehemu yaliyofunguliwa dhidi yake.”

“Hivyo basi, upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kuwa alikuwapo pamoja na washtakiwa wa kwanza, wa pili, na wa tano katika Kituo cha Polisi Mitengo, Januari 5, 2022.

“Wala haukuweza kuthibitisha kwa ushahidi wa moja kwa moja au wa muktadha kuwa alikuwa na ufahamu wowote kuhusu yaliyokuwa yanaendelea kituoni hapo siku hiyo,” anasema na kuongeza:

“Kinachoonekana ni kwamba, baada ya marehemu (Mussa) kurejeshwa kituoni Januari 5, 2022, hakuna dalili zozote zilizopatikana, iwe ni mawasiliano na washtakiwa wenzake zinazomhusisha moja kwa moja na kifo cha marehemu.”

Jaji anasema: “Kwa msingi huo, si salama kuhitimisha kuwa mshtakiwa wa tatu alihusika katika mauaji ya Mussa. Hivyo, kiini cha pili pia kinajibiwa kwa kukanusha upande wake.”

Daktari aliyechoma sindano

Kwa mujibu wa Jaji, kundi la pili ni mshtakiwa wa tano, daktari wa tiba, anayeaminika na jamii kwa kuwa na jukumu pana na lisilo na mbadala linalovuka mipaka ya hospitali na kliniki, kwa kuboresha ustawi wa mtu binafsi, afya ya umma na maendeleo ya sayansi ya tiba.

“Ni mtu anayetakiwa kutenda kwa huruma na moyo wa utu, lakini alimchoma marehemu (Mussa) sindano ya 1cc ya Ketamine akiwa mahabusu ili kumfanya aseme kwa jazba baada ya kupata fahamu,” anasema.

Jaji Mwanga anasema: “Katika utetezi wake, alikiri simulizi ya upande wa mashtaka na akaongeza kuwa hakumuua marehemu (Mussa) na alieleza kuwa aliripoti tukio hilo kwa RCO.”

“Kwa mujibu wake, sindano ya Ketamine ya 1cc haiwezi kusababisha kifo na kwa mujibu wa ripoti ya shahidi wa tisa (Mkemia wa Serikali), mabaki ya marehemu hayakuwa na sumu, hali inayodokeza kuwa hakufa kwa sumu,” anasema na kuongeza:

“Alidai alichokifanya katika Kituo cha Polisi Mitengo (kumdunga Mussa sindano) kilikuwa ndani ya wigo wa PGO (Mwongozo wa Utendaji wa Jeshi la Polisi) kwa sababu sindano hiyo ya Ketamine ilikuwa na lengo la kuzuia janga ambalo aliambiwa marehemu (Mussa) alikuwa amelifanya.”

Anasema: “Ninaamini hoja hiyo ina kasoro kubwa. Kwa mtazamo wangu, kumpa mtu Ketamine katika mazingira hayo kwa sababu zisizo za kitabibu ilikuwa hatari na inaonyesha wazi nia ya kumdhuru kwa uzito.”

Jaji Mwanga anasema: “Ni jambo la kujiuliza kwa nini raia asiye na hatia, ambaye si mgonjwa wala hajahitaji matibabu apewe dawa kali ya kulevya aina ya Ketamine akiwa mahabusu ya polisi?”

“Je, ni sababu gani halali ambayo daktari anaweza kuitoa katika mazingira haya ya kumpa mtu sindano bila dharura ya kitabibu?” anahoji.

Ana sema hoja kwamba madhumuni ilikuwa kumfanya aropoke ni batili kitabibu na ya kinyama kimaadili. Alipaswa kujua lengo halisi lilikuwa la kudhuru.

“Hakika, hakukuwa na uhalali wa kitabibu wala kisheria kumpa mtu dawa kali kama Ketamine akiwa chini ya ulinzi wa polisi kwa lengo la kumlemaza au kumtesa kwa sababu zisizo za kitabibu badala ya kutumia mbinu za kawaida za mahojiano,” anasema na kuongeza:

“Zaidi ya hayo, katika utetezi wake, shahidi wa tano wa utetezi, ambaye pia ndiye mshtakiwa wa tano alieleza alichofanya kilikuwa chini ya usimamizi na maagizo ya bosi wake, hivyo alihitaji kufuata maadili ya kazi yake.”

Jaji anasema: “Katika hoja yake, Felister Awasi wakili wake, alipowasilisha hoja za mwisho) alisisitiza hoja hiyohiyo. Alieleza mteja wake alilazimika kutii agizo la ofisa wake wa juu na kusaidia kupata taarifa za kiintelijensia kuhusu mtu aliyearifiwa kuwa mwizi sugu wa pikipiki kutoka Dar es Salaam.”

“Alinukuu PGO namba 1 (5), inayohimiza heshima kwa wakubwa ndani ya Jeshi la Polisi na PGO namba 106 (44)(e) inayoeleza athari za kukataa kutii agizo halali,” anasema.

Fuatilia sehemu inayofuata kujua namna Jaji Mwanga alivyohitimisha kuhusu mshtakiwa wa tano kwa aliyoyafanya kinyume cha maadili ya taaluma yake…

Related Posts