SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limewekeza shilingi bilioni 8.4 katika uanzishaji wa vituo sita vya kujaza gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG) vinavyohamishika, ikiwa ni hatua ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi katika sekta ya usafiri.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 12, 2025 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Biashara ya Gesi wa TPDC, Mhandisi Emmanuel Gilbert, amesema mradi huo utafanyika kwa muda wa miezi sita na unatekelezwa na kampuni binafsi iliyopatiwa zabuni Julai 11.
Mikoa itakayonufaika na mradi huu ni Dar es Salaam (vituo 3), Dodoma (vituo 2), na Morogoro (kituo 1).
“Hii ina maana watumiaji wa gesi asilia wataweza kupata huduma ya kujaza magari kuanzia Dar es Salaam hadi Dodoma. Hili litaongeza hamasa kwa wamiliki wa magari na bajaji kufunga mifumo ya CNG,” amesema Mhandisi Gilbert.
Hata hivyo, alieleza kuwa maeneo ya mbali kama ya machimboni hayatanufaika na vituo hivyo vya CNG kutokana na umbali na gharama kubwa za usafirishaji. Alisema kibiashara, CNG inapaswa kutumika ndani ya km 500, na ikizidi hapo, hulazimika kubadilishwa kuwa gesi ya kimiminika (LNG) ambayo inaweza kusafirishwa hadi km 1,500.
Kwa sasa, Tanzania ina vituo sita vya kujaza gesi asilia, na vituo vingine vinne vinaendelea kujengwa. Miongoni mwa miradi hiyo mikubwa ni kituo mama kinachojengwa na Puma Energy eneo la IPTL, Tegeta, pamoja na vituo vya mabinti vinavyojengwa Mabibo, Tanki Bovu, Barabara ya Coca-Cola, Mbezi Beach, na Barabara ya Nyerere.
Mhandisi Gilbert aliongeza kuwa kampuni nyingi binafsi zimewasilisha maombi ya kuanzisha vituo zaidi vya CNG jijini Dar es Salaam, kutokana na kuongezeka kwa mahitaji.
Takwimu zinaonyesha kuwa magari yanayotumia gesi asilia yaliongezeka kutoka magari 4,000 mwaka 2024 hadi zaidi ya magari 5,000 na bajaji 5,000 mwaka 2025.
Uwekezaji huu wa TPDC ni sehemu ya juhudi za serikali kuendeleza matumizi ya nishati safi na nafuu katika sekta ya usafiri nchini.